Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassimu Majaliwa amezindua Nembo na Kauli mbiu kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 60 ya muungano huku akiagiza kuelekea uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa mwaka 2024, wapiga kura wote kuhakikisha wanajiridhisha kwa kuwachagua viongozi wenye uwezo na nia njema na muungano

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo Aprili 8,2024 Waziri Majaliwa amewataka wananchi wote kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa na kuhakikisha wanachagua viongozi wanaojua nini maana ya muungano.

“Huu ni uchaguzi muhimu kwani viongozi wa serikali za mitaa wanatakiwa wawe msingi imara wa maendeleo yetu, tuwachague wale wanaotosha, ili wasaidie kuharakisha maendeleo yetu, ” amesema Waziri Mkuu.

Ameongeza,”Nawapongeza sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Dkt. Hussein Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kwa uongozi wao makini ambao umekuwa chachu ya kudumisha muungano wetu. Watanzania wote wameendelea kuulinda na kuuheshimu muungano wetu ambao umeendelea kukuza udugu miongoni mwetu, ” amesema

Aidha amesema Watanzania wana kila sababu ya kujivunia muungano kwani umetimiza umri wa miaka 60 kwani ni ukweli usiopingika kwamba muungano umeendelea kuwa na tija kubwa na kuchagiza maendeleo ya nchi na maendeleo ya wananchi wote kwa ujumla.

Amesema Muungano umefanya Tanzania kuwaTaifa lenye utulivu, mshikamano, nguvu na mfano kwa mataifa mengi barani Afrika na duniani kwa ujumla.

“Natoa rai kwa Watanzania wote kuendelea kumwomba Mwenyezi Mungu aendelee kutujalia amani, utulivu na mshikamano, ili muungano wetu uweze kuendelea kudumu na kuimarika zaidi kwa manufaa ya vizazi vyetu, ” Amesema.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama amesema Katika miaka 60 ya muungano wetu, Jamhuri ya muungano wa Tanzania inaongozwa na Rais wa kwanza mwanamke, ni jambo la kujivunia kwani sio tu tunaongozwa na Rais mwanamke, lakini ni mwanamke mbobezi, mwenye uwezo wa hali ya juu na aliyeuthibitishia ulimwengu mzima kwamba utendaji kazi wake umetukuka kwa viwango ambavyo havina mfano.

Amesema Mwaka huu tunajivunia kwa kutimiza miaka 60 ya muungano wetu. Zipo sababu nyingi za kihistoria, kijiografia, kitamaduni, kibiashara, kisiasa na kiusalama ambazo wakati wote wa muungano wetu zimeendelea kutuunganisha kama Taifa moja la Tanzania.

“Sote tunafahamu uzito wa maadhimisho ya miaka 60 ya tukio lolote lile. Hivyo, hatuna budi kukaa pamoja kama Taifa moja kumshukuru Mungu na kuiadhimisha siku hii kwa furaha kubwa,” Amesema .

Ameekeza Sherehe za kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya muungano, zitazinduliwa rasmi na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi tarehe 14 Aprili, 2024 katika uwanja wa Maisara, Zanzibar ambapo Tukio hili litafuatiwa na uzinduzi wa miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.

Nate Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo amehakikisha kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Watanzania wote wanayafahamu yale yote ambayo walipaswa kujivunia kupitia muungano huu.

“Namshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa usimamizi wao unaofanikisha twende kifua mbele katika miaka 60 ya muungano wetu, ” .

Na kuongeza “Leo tunapoanza safari hii, tunawashukuru viongozi wetu wakuu kwa kutuheshimisha sana kwa sababu katika kipindi chao cha miaka mitatu wameweza kutatua kero 15 za muungano kati ya kero 18 zilizokuwa zimebakia, ” Amesema waziri Jafo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (Sera, Uratibu na Baraza la Uwakilishi), Hamza Hassan Juma kwa Watanzania, muungano ni tunu yetu kubwa, hivyo kuna wajibu wa kuulinda, kuutunza na kuutetea kwa hali zote.

Amesema Tukio hilo la uzinduzi wa nembo na kauli mbiu ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, linaenzi mawazo ya viongozi waasisi wa muungano wetu.

“Muungano huu kudumu kwa miaka 60 sio jambo jepesi, tayari kuna misukosuko mingi ambayo muungano huu umepitia, mathalan kwenye Bunge la Katiba, kuna watu waliukana muungano kuwa haupo kwa sababu hakuna hati ya muungano. Katika kitu ambacho ni tunu, ni hati ya muungano ambayo ipo na imehifadhiwa, ” Amesema .

Na kuongeza “Zanzibar tuko tayari kwa ajili ya kutekeleza yatakayoelekezwa katika shughuli hii, “.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule ameungana na Watanzania wengine kuendelea kuwapongeza viongozi wetu wakuu kwa kuendeleza muungano wetu ambao una historia ya muda mrefu na kuendelea kuimarisha na kuufanya muungano kuendelea kuwa imara.

“Nawapongeza pia Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa kuendelea kuratibu Muungano huu katika utulivu na amani na kufanya nchi hizi mbili zikiendelea kuimarika kwa mshikamano mkubwa, ” Amesema Senyamule.

Please follow and like us:
Pin Share