Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako amewataka wote wanaodaiwa mikopo ya Elimu ya Juu kuirejesha mikopo hiyo mara moja pasipo kungoja kuchukuliwa hatua za kisheria.

Katika mahojiano aliyoyafanya na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Waziri Ndalichako alisema kuwa kil aliyepata mkopo wa Elimu ya Juu ana wajibu wa kuulipa ili wanafunzi wanaoomba mikopo nao waweze kupata na kwamba serikali haitosita kuchukua hatua stahiki kwa wale ambao hawatozirejesha ikiwamo kushtakiwa mahakamani.

Waziri Ndalichako alisema kwa wale waliokuwa wakinufaika na mikopo hiyo na kwa sasa wamejiajiri wenyewe na ambao bado hawajapata ajira wanapaswa kufika katika Ofisi za Bodi ya Mikopo ili wapewe utaratibu wa namna gani ya kuanza kurejesha.

Hata hivyo Prof. Ndalichako alisema kwamba, idadi ya wanufaika wa mikopo waliojitokeza kwa hiari kuanza kurejesha mikopo yao imeongezeka na kuwataka ambao bado hawajaanza kufanya hivyo wawaige wenzao walioanza tayari.
Novemba 2016, Bodi ya Mikopo ilitoa orodha ya majina ya wadaiwa sugu takribani 20,000 ambao walitakiwa kuanza kurejesha mikopo yao ndani ya siku 30.

Hapo awali Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Abdulrazaq Badru alieleza kuwa watachapisha orodha ya majina ya wadaiwa sugu takribani 142,470, wanaodaiwa jumla ya kiasi cha shilingi za kitanzania 239.3 billioni.

Hata hivyo Prof Ndalichako aliwataka wale wote watakaoanza kurejesha mikopo yao kwa Bodi ya Mikopo, kulipa fedha hizo kupitia akaunti ya benki ya Bodi na siyo kulipa fedha taslimu kwa mtu yeyote yule. Alisisitiza hilo ili kuepusha usumbufu ikiwemo utapeli ambao unaweza kufanyika wakati wa ufanyaji wa malipo hayo.

Please follow and like us:
Pin Share