Isri Mohamed

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt Damas Ndumbaro amemsimamisha Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa nchini (TPBRC), Chaurembo Palasa, pamoja na Katibu mkuu George Silas na viongozi wengine wote wa kamisheni hiyo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka.

Waziri Ndumbaro ametoa maamuzi hayo akiwa kwenye kikao na viongozi wa kamisheni na vyama vinavyounda kamisheni hiyo kilichofanyika jijini Dodoma, Mei 5, 2024.

Baada ya uamuzi huo Waziri Ndumbaro amemteua Bw Emmanuel Salehe kuwa mwenyekiti wa kamati ya mpito ya kuongoza kamisheni hiyo akisaidiana na makamu wake Alex Galinoma.

Mbali na hao, amewateua pia wajumbe watatu wa kamati hiyo, Patrick Nyembera kutoka Azam TV, Shafii Dauda wa Clouds Media na Irene Mwasanga.

Aidha waziri Ndumbaro ameunda kamati ya kufanya uchunguzi kwa kamisheni iliyosimamishwa kuhusu tuhuma mbalimbali zilizoibuliwa na wanachama ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka, ukiukwaji wa katiba ya kamisheni hiyo na mgongano wa maslahi.

Kamati ya uchunguzi itafanya kazi kwa muda wa mwezi mmoja kuanzia Mei 8, 2024 na itaongozwa na mwenyekiti Bw Christopher Kamugisha, katibu Ingridy Kimario na wajumbe wawili Mariam Faki na Sophia Alponary.

By Jamhuri