Na Mwandishi Wetu, JakhuriMedia

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa ameta kuwepo mpango wa uendelezaji katika eneo la Kongani ya Viwanda (Industrial Park) lililopo Kibaha vijijini mkoa wa Pwani.

Silaa ametoa kauli hiyo tarehe 4 Oktoba 2023 Mlandizi wakati alipokagua miundombinu ya Kongani ya Viwanda Kibaha mkoani Pwani ambapo kampuni ya KAMAKA Limited imewekeza kwenye eneo hilo.

‘’Mhakikishe sasa, kwa kuwa Pwani inakuwa na ndiyo industrial area katika Taifa letu, tuhakikishe maeneo yetu yote ndani ya Kongani hili la viwanda kunaandaliwa mpango mkubwa wa uendelezaji’’ ’’ alisema Mhe. Silaa

Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, unapokuwa mji wa viwanda lazima uwe unajitosheleza kwenye maeneo yote na kubainisha kuwa, wakati eneo la Kongani ya viwanda likifanyiwa kazi basi halmashauri ziendelee kushughulikia kijamii pamoja na kuhamasisha watu huku akisisitiza kuwa, siyo kila muwekezaji anayekuja anataka kuwekeza kwenye eneo la viwanda.

‘’Kumbe kwa uwekezaji huu mwekezaji anaweza kujenga nyumba za makazi, zikapata wateja kuliko hata nyumba zilizokuwa Dar es Salaam kwa sababu hapa viko takriban viwanda 202 vina wafanyakazi watakaohitaji makazi na hao wanaweza kupata nyumba zikawasaidia kupata maeneo ya kuishi’’ alisema

Kwa upande wake, Meneja mradi Kongani ya viwanda Kibaha Nelson Mollel amesema lengo la mradi huo ni kuitikia wito wa serikali kujenga viwanda, kukuza uchumi na kuleta maendeleo ya watu kupitia uwekezaji.

Ameweka wazi kuwa, teknolojia mpya pamoja na kuongeza fursa za kiuchumi kwenye kuongeza ajira na kulinda hifadhi ya mazingira na kujenga viwanda vingi eneo moja badala ya kuwa na viwanda vingi vilivyotawanyika maeneo mbalimbali ni sehemu ya malengo ya mradi.

Mkuu wa wilaya ya Kibaha Simon Nikson amesema, wilaya yake imetenga maeneo kwa ajili ya viwanda kwa lengo la kutaka uwekezaji sambamba na viwanda huku akibainisha kuwa, mara kadhaa watu wakipita eneo hilo wanajua ni kiwanda wakati ni miundombinu iliyoandaliwa kwa ajili ya Kongani ya uwekezaji viwanda.

Kwa Mujibu wa Nikson, eneo hilo linategemewa kuwa na takriban viwanda 200 ambapo huduma zote za msingi za viwanda zinapatikana na kubainisha kuwa, taasisi kama BRELA na TRA zitatoa huduma kwenye jengo moja.