Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila leo Oktoba 4, 2023 amepokea vifaa tiba toka Shirika la DKT international ambavyo amevielekeza katika Wilaya ya Kigamboni na Ubungo Jijini Dar es Salaam.

Akipokea msaada huo wa vifaa tiba RC Chalamila amelishukuru shirika hilo kwa kuunga mkono juhudi za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya afya hapa nchini, mchango uliotolewa ni wa thamani kubwa, ametoa rai kwa wadau wengine wa Afya katika Mkoa kuiga mfano na kuunga mkono juhudi za Serikali katika katika Mkoa.

“Rais Dkt Samia Suluhu amekua akitoa pesa nyingi na anaendelea kutoa katika kuboresha sekta ya Afya, ujenzi wa vituo vya Afya, zahanati na Hospitali unaendelea kujengwa kila kona hivyo kuunga mkono juhudi hizi ni kumpa nguvu aendelee kupambana zaidi kwa masilahi mapana ya Watanzania” amesema RC Chalamila.

Aidha RC Chalamila amewataka Wilaya ya Ubungo na Kigamboni kuhakikisha wanatunza vifaa tiba walivyopatiwa ili viweze kutumika kwa muda mrefu

Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt Rashid Mfaume ameanisha vifaa tiba vilivyotolewa na Shirika la DKT International ikiwemo vitanda kwa ajili ya operesheni, makabati, na viti mwendo pia amewaomba kuendeleza ushirikiano na Mkoa katika kutekeleza afua mbalimbali za kukabiliana na magonjwa ya ngono, uzazi wa mpango na UKIMWI

Mwisho ifahamike kuwa DKT International ni shirika lisilo la Kiserikali ambalo linajishughulisha zaidi na upangaji uzazi, kuzuia VVU/UKIMWI na uzuiaji mimba kwa njia salama