*Yaliyoandikwa na JAMHURI yametimia

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, ameshitakiwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania. Mlalamikaji ni Kampuni ya raia wa kigeni inayojihusisha na uwindaji wa kitalii ya Foa Adventure Safaries Limited.

Kushitakiwa kwa Kagasheki ni kutimia kwa taarifa ambazo JAMHURI imekuwa ikiziandika kwa muda mrefu sasa, na ya mwisho ikieleza namna wafanyabiashara kadhaa wa vitalu vya uwindaji wa kitalii walivyokutana Marekani, na kwa ushauri wa baadhi ya viongozi waandamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, wafungue kesi ili wapewe vitalu vanavyovitaka kwa udi na uvumba.

 

Kesi dhidi ya Kagasheki ipo mbele ya Jaji Zainabu Mruke. Mlalamikaji anataka kampuni zilizopewa vitalu katika maeneo ya Rungwa Mwamagembe Game Reserve, Luanda Mkwambi Game Controlled Area (North), Rungwa Rungwa Game Reserve (East) na Rungwa Rungwa Game Reserves (West), ziondolewe ili apewe yeye.

 

Kufunguliwa kwa kesi hiyo, pamoja na mambo mengine, kunatokana na kile kampuni hiyo inachodai kuwa ni kwa Waziri Kagasheki kukataa kutoa uamuzi wa mwisho wa kiutawala wa ugawaji vitalu kama sheria inavyotaka.

 

Hata hivyo, kwenye maelezo yake, kampuni hiyo inaonesha kuwa Waziri alishatoa, lakini akawa ameahidi kufanya mapitio hayo baada ya kukutana naye mara kadhaa.

 

Marehemu Nyaga Mawalla, aliyekuwa mshirika mkuu wa Kampuni ya FOA na nyinginezo, anatajwa kama mmoja wa watu waliokutana na Waziri Kagasheki katika kufikia suluhu ya jambo hilo.

 

Mlalamikaji anadai kwamba Oktoba 26, 2011 alipeleka maombi kwa Waziri akitaka mapitio ya kiutawala baada ya kunyimwa vitalu alivyoomba. Anadai kuwa maombi mengine aliyapeleka Novemba 15, mwaka jana, lakini bado Waziri alishindwa kutoa uamuzi.

 

Katika kesi hiyo, washitakiwa wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kampuni za uwindaji za Bushman Hunting Safaris Limited iliyoshinda na kupewa kitalu cha Rungwa Rungwa Game Reserve (East).

 

Wengine ni Merera Lodges and Tours Limited, iliyopewa kitalu cha Rungwa Rungwa Game Reserve (West), Mwanauta Company Limited (Rungwa Mwamagembe Game Reserve), na Go Wild Hunting Limited, Luanda Mkwambi Game Controlled (North).

 

Yaliyoandikwa na JAMHURI yatimia

Miezi kadhaa iliyopita, JAMHURI iliandika habari ya uchunguzi kuhusu mkakati wa baadhi ya kampuni za kigeni, wa kuwanyang’anya wazawa vitalu vya uwindaji wa kitalii. Habari hiyo ilisomeka hivi:

 

Kundi la wafanyabiashara kadhaa wa tasnia ya uwindaji wa kitalii, limekutana nchini Marekani na kuendesha mchango wa mabilioni ya shilingi kwa ajili ya kuhakikisha yanafanikisha ugawaji upya wa vitalu vya uwindaji.

 

Habari za uhakika zilizopatikana kutoka ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii, zimesema fedha hizo zimechangwa kwa kivuli cha kusaidia shughuli za uhifadhi nchini, lakini ukweli wa mambo ni kwamba zimepangwa kutumiwa kuwarubuni baadhi ya viongozi waandamizi wa Wizara hiyo pamoja na vyombo vya dola, hasa Ofisi ya….na…..

 

Mpango huo unasukwa ilhali Ikulu, na baadaye Wizara ya Maliasili na Utalii mnamo Januari, mwaka jana, zikitoa taarifa ya kutorejewa ugawaji vitalu kwa kuwa ulifanyika kwa kufuata sheria zote.

 

Sehemu ya tangazo la Wizara ya Maliasili na Utalii kwa umma, kupitia kwa Msemaji wake, George Matiko, lilisomeka: “Wizara ya Maliasili na Utalii haina mpango wa kurudia ugawaji wa vitalu. Mchakato wa ugawaji ulikamilika mwezi Septemba mwaka jana (2011) na matokeo yake kutangazwa wazi.

 

Mapema mwezi Septemba 2011, Wizara ilitoa orodha ya kampuni 60 zilizofanikiwa kugawiwa vitalu. Kati ya kampuni hizo, kampuni 51 ni za kizalendo na kampuni 9 za kigeni kwa kuzingatia kifungu 39(3)(b) cha sheria ya wanyamapori Na. 5, ya 2009.

 

Hata hivyo, kumekuwa na taarifa mbalimbali zilizoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari, kuhusu kuwapo kwa harakati zinazofanywa na waombaji waliokosa vitalu, zikihusisha kuchafuana baina ya kampuni zilizopata na zilizokosa kwa nia ya kuzorotesha sekta ya uwindaji wa kitalii kwa ujumla. Vyombo hivyo vimeripoti kuwa mchakato wa ugawaji wa vitalu utarudiwa.

 

Wizara inasisitiza kuwa mchakato wa ugawaji wa vitalu hautarudiwa, na Watanzania wanahakikishiwa kuwa hatua zilizochukuliwa na serikali za kuleta mabadiliko kwenye sekta hii tangu mwaka 2008, zimesaidia sana kuimarisha usimamizi wa Sekta hii.

 

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa mkakati huo umeratibiwa na mmoja wa wadau kwenye tasnia ya uwindaji, mwenye ushawishi mkubwa ambaye anaishi mkoani Arusha.

 

Mdau huyo ambaye anashirikiana na baadhi ya raia wa kigeni, amekuwa akihaha kupata vitalu ambavyo kwenye mgawo halali uliokwishafanyika walipewa Watanzania wazawa.

 

Tangu wakose vitalu hivyo, mdau huyo ambaye kwa sasa jina lake tunalihifadhi (marehemu Mawalla), amethubutu kutumia njia mbalimbali zikiwamo za kuwaghilibu wabunge pamoja na viongozi waandamizi serikalini katika kuhakikisha anapata vitalu hivyo. Moja ya sababu zake ni kwamba kugawanywa kwa vitalu kulikofanywa na wataalamu katika maeneo kadhaa, hasa katika mikoa ya Arusha na Manyara kunaathiri ikolojia.

 

Kwa kuamini kuwa mpango wake wa kupata vitalu kutoka kwa wazawa wenzake utafanikiwa, hadi sasa kampuni nne alizo na uhusiano nazo wa karibu hazijakabidhiwa barua.

 

Chanzo cha habari kimedokeza kwamba Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, licha ya kutamka mara kwa mara, na hata kutoa taarifa rasmi kwenye vyombo vya habari kwamba ugawaji vitalu hautarejewa, sasa anaelekea kukubaliana na kundi linaloshinikiza kurejewa upya ugawaji huo.

 

Imeelezwa kwamba ameshauriwa kuwa ili kutojiweka kwenye utata na mgongano wa kauli, suala la ugawaji upya wa vitalu sasa liamuriwe na Mahakama Kuu. Wiki iliyopita kundi la wafanyabiashara hao lilikuwa, ama likutane na viongozi waandamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii mjini Dodoma, au jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuweka mambo sawa.

 

“Mikutano ya Dodoma na Dar es Salaam ililenga kuhakikisha Mahakama inatumiwa kutengua uamuzi wa awali wa ugawaji vitalu. Hawa watu wanajiamini sana. Wakiwa Marekani wakawa wanawatisha watu wasiuze safari wakisema ugawaji vitalu unarudiwa.

 

“Njia nzuri iliyoonekana ni ya kuitumia Mahakama kubadili uamuzi wa awali. Fedha zilizochangwa zimelenga kutolewa kwa viongozi kadhaa waandamizi ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii, na pia ikiwezekana zitumike kuweka mambo sawa mahakamani. Haya mambo ni ya siri sana, lakini ukweli ndiyo huo,” kimesema chanzo chetu cha habari.

 

Habari zilizovuja kutoka kwa mmoja wa viongozi wakubwa kabisa wizarani humo, zimesema kwamba kigogo huyo amewataka wafanyabiashara hao wakae kimya, wahakikishe mkakati huo hautolewi kwenye vyombo vya habari.

Please follow and like us:
Pin Share