Uchaguzi unaoendelea katika ngazi mbalimbali ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), unapaswa kuwa funzo maridhawa kwa makada, viongozi na wafuasi wa chama hicho kikongwe.
Tangu uanze katika ngazi ya shina, nimejitahidi kuufuatilia ili kubaini mwitikio wa wanachama wanaoomba nafasi mbalimbali.

Hali inakatisha tamaa. Nadiriki kusema kuwa kwa mara ya kwanza nafasi kama ya wajumbe wa mashina imetoa picha ya wapi CCM inakoelekea. Watu hawataki kujitokeza kuwania uongozi ndani ya chama hicho!

Katika mashina, wagombea wamepita bila kupingwa! Hata pale kulipojitokeza ushindani, haukuwa na mashamshamu tuliyoyazoea.

Katika ngazi za matawi na kata hali imekuwa hiyohiyo. Kuna matawi na kata zilizokosa wagombea! Baadhi ya maeneo uchaguzi umeshindikana kwa sababu hakuna wagombea. Hili ni somo zito.

Nimejaribu kuzungumza na wafuasi na viongozi kadhaa wa CCM katika maeneo kadhaa nchini. Karibu wote majibu yao yanafanana. Wanasema hawaoni sababu ya kuhangaika ndani ya chama ambacho kinazidi kupoteza mvuto siku hadi siku, hasa kwa vijana.

Nasema hizi ni salaamu maridhawa kwa wafuasi na viongozi wa CCM. Pamoja na ukweli huu, bado wapo wahafidhina watakaoendelea kubeza hali hii. Wanajipa matumaini hewa. Wanajidanganya.

CCM imekuwa ikipoteza mvuto kila siku. Zipo sababu nyingi zinazoelezwa na wachunguzi wa masuala ya kisiasa. Lakini zipo nyingine ambazo mtu wa kawaida kabisa anaweza kuzieleza bila wasiwasi wowote.

Kwa mfano, wananchi wanaamini kuwa hali ngumu ya maisha inayowakabili sasa ni matokeo ya uongozi mbovu wa CCM na Serikali yake. Pamoja na utetezi wa Serikali kwamba ugumu wa maisha unasababishwa na hali ya mambo duniani, maelezo hayo hayawaingii wananchi akilini.

Hayawaingii kwa sababu wakati wakipewa hadaa hizo, ripoti ya CAG inaibua wizi wa ajabu kabisa unaofanywa na walioshika hatamu ya uongozi katika taifa letu. Kweli kumekuwapo wizi wa mali za umma kwa awamu zote, lakini huu wa sasa umepitiliza. Watu wanajiuzia majengo, viwanja, viwanda, aradhi kana kwamba walio madarakani wamewasiliana na Mungu na kuhakikishiwa kuwa mwisho wa dunia umeshawadia.

Wanauza na kutapanya mali za umma kana kwamba Watanzania wote wametiwa ugumba ambao hauwawezi kupata watoto wala wajukuu watakaoishi katika taifa hili baada ya kizazi cha sasa.

Wanaimbiwa wimbo wa ugumu wa maisha. Wanapata mlo wao wa maana ukikolezwa kwa mapanki, ilhali minofu ikipelekwa Ulaya ili iboreshe afya za Wazungu.

Wanakosa matibabu ya maana katika zahanati, vituo vya afya wakati Serikali imeruhusu kila aina ya madini katika taifa letu yachimbwe na kupelekwa Ulaya. Wanakosa dawa, huku wakisoma kwenye taarifa kuwa dawa za Sh bilioni tano zimeozea maghalani!

Sasa mitaa na vijiji vyote Tanzania vimepambwa kwa matangazo ya waganga matapeli; wale wanaojitambulisha kuwa ni mabingwa wa kusafisha nyota na kuleta bahati! Wameshatujulia. Biashara yao kubwa ni ya dawa eti za kuleta bahati! Maelfu kwa maelfu ya Watanzania wanawafuata kupata dawa hizo za uwongo kwa sababu tu ya imani ya kuondokana na umasikini.

Makanisa ya kitapeli yanafunguliwa kila mahali. Usajili unafanywa karibu kila mwezi. Kila mahali ni kanisa. Matapeli makanisani wamebuni hadi njia ya SMS ili kupata sadaka. Bila kutoa sadaka, hakuna kuombewa! Hakuna mibaraka! Wenye ukwasi ndiyo wanaopewa heshima ya kuketi viti vya mbele kanisani! Sijui ni Mungu gani huyu asiyewapenda masikini!

Wananchi wanadanganywa, na wao wanadanganyika kwa sababu wanaamini kuwa matatizo yao yanaweza kumalizwa kwa kuombewa tu! Wanaamini kwa kupata upako, basi mambo yatawanyookea hata kama ni wagumu wa kuwahi kuamka asubuhi, na wepesi wa kuwahi kulala.

Ndimo kwenye kundi hilo la watu walioingiwa na mazonge ya maisha tunawakuta wengine wakipiga kambi kando ya uwanja wa ndege wakiamini kuwa hata bila pasipoti, bado wanaweza kusafiri kwenda Ulaya kueneza injili! Haya ni matokeo ya athari za ugumu wa maisha. Hakuna kitu kingine.

Serikali imepuuza kuhamasisha vijana wapende kazi. Imebaki kuwapa bodaboda. Katika jamii ya aina hii, jamii isiyokuwa na usawa wa mgawo wa rasilimali za nchi, ni rahisi sana kwa chama kinachoongoza kuchukiwa. Tena chuki inazidi pale wanyonge wanapoona wanaumizwa, ilhali wachache wakineemeka ndani ya kundi kubwa la masikini.

Matokeo ya hali hii ndiyo haya sasa yanayoanza kujionyesha kwenye uchaguzi ndani ya CCM. Wanachama wamekata tamaa. Viongozi wameona ahadi zote tamutamu walizopewa kwa miaka mingi hazitekelezeki. Chuki imewaingia, matamanio ya kujaribu mbinu nyingine yamewajaa, na sasa wanaona ni bora wasipoteze muda kwenye siasa zisizo na tija, badala yake watafute njie nyingine.

Kundi la watu waliokata tamaa kama hawa, lipo tayari kujiunga katika chama chochote ambacho linadhani kitabadili maisha yao. Na kwa sasa kundi hilo halioni mkombozi mwingine zaidi ya Chadema. Lakini kundi la aina hii, hasa vijana, ndilo linaloweza kushawishiwa na kuibua uasi.

Kasi ya viongozi na wanachama wa CCM kukihama chama hicho na kujiunga katika vyama vya upinzani, haipaswi kupuuzwa na CCM. Na pia haipaswi kuchukuliwa na Chadema kama jambo la kawaida tu. Lazima Chadema watayarishe makazi ya ujio huu. Wasipojiandaa sasa watajikuta wakishindwa kuhimili idadi ya wanachama wapya.

Kama nilivyosema wiki iliyopita, naomba nirejee leo kusema kwamba matarajio ya Watanzania sasa kwa Chadema ni makubwa mno. Wanapojitokeza watu kama kina Mzee Sabodo kuwapa misaada Chadema hadharani, bila woga, ni lazima watu wenye utashi watafakari hali hii na hatima ya CCM.

Chama Cha Mapinduzi kikiendelea na dharau zake, ni wazi kuwa kitabaki kuwa ni chama cha hawa hawa waliomo pamoja na watoto wao, ingawa hata baadhi ya watoto wamekuwa na mawazo tofauti. Kuna watoto wengi ambao wamewaacha wazazi wao ndani ya CCM na wao kwenda kwenye vyama vya mageuzi.

Pamoja na juhudi zote za kuundwa kwa Baraza la Mawaziri, hakuna dalili kwamba mabadiliko hayo yanaweza kuzuia kasi ya vijana na wananchi kuichukia CCM.

Kama nilivyopata kusema, nadharia ya uhai ina misingi yake isiyoyumba. Kila chenye uhai huzaliwa, hukua, huzeeka na hufariki dunia. CCM imefikia ngazi ya uzee, na sasa kilichobaki kwa kweli ni kifo tu.

Lakini kifo kinaweza kusogezwa mbele, japo kwa mbinu tu za kiungwana za kuongeza siku za kuishi. Katika maisha kuna miiko ambayo mtu akiifuata, huambiwa anaweza kuongeza siku za kuishi, ingawa hiyo haiondoi ukweli kwamba siku ya kifo itafika tu.

Lishe ya CCM ya kuiwezesha kuongeza siku za kuishi ni kuyasikia haya inayoambiwa. Irejee kwa wananchi masikini waliokosa sauti katika uchumi wa taifa lao. Serikali yake ipambane na wezi wanaotapanya mali za umma kana kwamba nchi haina mwenyewe.

Serikali ya CCM itende haki kuanzia polisi, katika mahakama, hospitali na katika huduma zote za umma. Ipambane na rushwa kwa dhati. Isisubiri Kamati Kuu ibariki kuwafukuza wazembe na wezi wa mali za umma. Isimamie sheria halali zilizotungwa kwa manufaa ya taifa letu. Hii ndiyo lishe pekee inayoweza kuongeza siku zake za kuishi. Kwa kupuuza sauti ya wenye nchi, CCM inajiharakishia kifo chake. Siku si nyingi, CCM itabaki kuwa ya viongozi na watoto wao!

1216 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!