Na Magrethy Katengu, JamhuriMedia,Dar es Salaam

Serikali imewaelekeza wadau wote ndani ya nchi ikiwemo taasisi za umma, wafanyabiashara, asasi za kiraia, mashirika ya kimataifa wenye tabia ya kuweka bei kwenye bidhaa au huduma kuuza kwa fedha za kigeni kuacha mara mara.

Imeelezwa kuwa vitendo hivyo vinachangia uhaba wa fedha za kigeni pasipo sababu hivyo kuanzia Julai 1, 2024, yeyote atakayebainika hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha bajeti ya mwaka 2024/ 2025 Bungeni Jijini Dodoma.

Amesema Watanzania pia wanalikuza tatizo la upungufu wa dola kwa baadhi ya watu kudai malipo au kufanya malipo ya bidhaa na huduma zinazotolewa ndani ya nchi kwa kutumia fedha za kigeni yaani, dollarization kwani taasisi ipo Tanzania na wakati mwingine hata taasisi ya Serikali, inamuuzia huduma Mtanzania inamwambia alipe kwa dola.

Pia taasisi zingine zinataka Mtanzania alipe ada kwa dola, alipe kodi ya nyumba kwa dola, vibali vya kazi, leseni na kadhalika kwa dola hivyo kunawafanya Watanzania wahangaike kuitafuta fedha ya kigeni kununua huduma zinazotolewa ndani ya nchi yao.

” Niseme tabia hiyo siyo nzuri kwani tunawafanya Watanzania wahangaike kuitafuta fedha ya kigeni kununua huduma zinazotolewa ndani ya nchi yao badala ya kuwafanya wageni wahangaike kuitafuta shilingi ya Tanzania wanapotaka huduma ndani ya nchi.

“Jambo hili linasababisha kuongezeka kwa mahitaji yasiyo ya lazima ya fedha za kigeni na kuwanyima fursa watu wanaohitaji fedha za kigeni kwa ajili ya kulipia bidhaa na huduma muhimu kutoka nje ya nchi hivyo kitendo cha kuuza bidhaa au huduma za
ndani kwa kutumia fedha za kigeni ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006, ambacho kinabainisha kwamba Shilingi ya Tanzania ndiyo fedha halali pekee kwa malipo ya ndani ya nchi” amesema Mwigulu.

Waziri Mwigulu ametoa rai kwa sekta husika kutekeleza mkakati huo ili kufikia matokeo yanayotarajiwa na amesisitiza, taasisi zote za Serikali kuzingatia matakwa ya kifungu cha 60 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma Namba 10 ya mwaka 2023 kinachoelekeza kutoa kipaumbele kwa bidhaa au huduma zinazotengenezwa au kuzalishwa ndani
ya nchi katika mikataba inayotolewa kwa misingi ya ushindani wa zabuni za kitaifa au kimataifa ili kupunguza matumizi ya fedha za kigeni na kukuza viwanda vya ndani ya nchi.

Sanjari na hayo amebainisha kuwa endapo mtu ana fedha za kigeni, unatakiwa kuzibadilisha kupitia benki au maduka halali ya kubadilishia fedha ndipo ufanye malipo kwa kutumia shilingi ya Tanzania hivyo Benki Kuu pamoja na vyombo vingine vinavyohusika vimeelekezwa kuendelea kudhibiti suala hilo kufuatilia kwa ukaribu ili kubaini wote wanaoendelea kufanya makosa hayo, na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.

Waziri Nchemba amebainisha kuwa pamoja na changamoto hiyo kuwa kubwa katika nchi nyingi duniani, Serikali ilifanikiwa kukabiliana nayo kwa kushirikiana na sekta binafsi na washirika wa maendeleo ili kuendelea kuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni ambapo hadi Machi 2024, akiba ya fedha za kigeni ilikuwa dola za Marekani bilioni 5.3, kiasi ambacho kinakidhi uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa miezi 4.4, kiasi ambacho kiko juu ya lengo la nchi la muda usiopungua miezi 4.0.

Aidha, Serikali iliendelea kutekeleza mkakati wa kupunguza nakisi ya urari wa biashara uliopelekea kupungua kwa nakisi hiyo kutoka dola za Marketing bilioni 5.3 mwaka 2022 hadi dola za Marekani bilioni 2.7 kwa mwaka ulioishia Februari 2024 kwa kuongeza mauzo nje na kupunguza uagizaji wa bidhaa
zinazozalishwa nchini.