Na Mussa Augustine,JamhuriMedia

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), kwa kushirikiana na Taasisi ya Nafasi Arts Space linatarajia kufanya toleo la pili la wiki ya sanaa lijulikanalo kama”Tukutane Dar” kuanzia Februari 1 hadi 5 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari katika makao Makuu ya BASATA Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Nafasi Arts Space ambao ni waandaaji wa toleo hilo Lilian Mushi amesema kwamba lengo ni kujenga ushirikiano kwa wataalamu na wadau wa sanaa ndani na nje ya Tanzania.

Aidaha amesema kuwa Tukutane Dar itawaleta watu pamoja kujenga mfumo mahiri na mtandao wa sanaa na utamaduni,na kwamba itafanyika katika maeneo saba ya Sanaa na kitamaduni kote Jijini Dar es Salaam.

“Maeneo hayo ni Nafasi Arts Space,Rangi Gallery ,CDEA ,Ajabu Ajabu ,ASEDEVA,Chuo Kikuu cha Dar es salaam na MuDa Kona,sehemu hizi zitaandaa majadiliano ya paneli asubuhi na warsha na maonyesho ya wasanii jioni” amesema Liliani.

Amebainisha kuwa warsha hizo zitajumuisha darasa la utunzaji kazi za sanaa litakaloendeshwa na watunzaji wa Sanaa wa Kimataifa,kutakuwepo na warsha ya uandishi wa filamu,warsha ya ‘Threatre’ kwa maendeleo ya jamii, na warsha ya kuchora ramani za maeneo ya ubunifu kote Tanzania.

Amesema kuwa Siku ya Ijumaa Februari 3,mwaka huu, pamoja na wataalamu wa sanaa kutoka Afrika kusini,Uingereza,Zambia na Uganda,watafanya mjadala wa hadhara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam( UDSM) ,ambapo siku ya Jumamosi ya Februari 4 Mkurugenzi Mtendaji wa BASATA Dkt.Kedmon Mapana ,Katibu Mtendaji wa BASATA wataelezea sera mpya ya baraza hilo na namna ambavyo wasanii wanaweza kunufaika na sera hizo.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa BASATA Kedmon Mapana amesema kuwa baraza hilo litaendelea kuweka mazingira mazuri kuwawezesha wasanii kukuza na kuendeleza vipaji vya sanaa ili kufikia malengo wanayotamani kufika.

“Taasisi ya Arts Space ni muhimu sana kwenye kuibua vipaji na kuviendeleza,imeandaa tukio hili kubwa kwa ajili ya kukutana wadau wa sanaa na kujadili kwa pamoja changamoto na mafanikio ya sanaa,lengo ni kukuza tasnia ya sanaa hapa nchini” amesema.

Naye Mkurugenzi Mstaafu wa Naface Arts Space Rebecca Corey amesema kwamba taasisi hiyo imefanikiwa kushirikiana vizuri na Serikali nakwamba itaendelea kushirikiana na wadau wengine wa sanaa katika kuibua,kukuza na kuendeleza kazi za wasanii mbalimbali hapa nchini.

Hata hivyo Nafasi Arts Space imewaomba wapenzi wote wa sanaa na utamaduni kushiriki na kuungana kwa pamoja na wasanii na wataalamu wa sanaa kutoka ndani na nje ya Tanzania ,pamoja na kufurahia shughuli za kitamaduni zitakazofanyika kuzunguka Jiji la Dar es Salaam na kutambua maeneo mengine Tanzania yanayojihusisha na shughuli za sanaa na utamaduni kupitia wawakilishi wa mikoa.

“Ratiba kamili ya matukio inaweza kupatikana kupitia mitandao ya kijamii ya Nafasi Art Space na tovuti na kurasa za mitandao ya Kijamii za washirika wenzetu” imesema taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Nafasi Arts Space Lilian Mushi.

By Jamhuri