Nasibu Abdul maarufu Diamond Platnumz ambaye ni msanii wa Bongo Fleva nchini,ametangaza kuhamia timu ya Yanga SC amedai kumfuata msemaji Haji Manara.

Awali Diamond alikuwa akishabikia Simba SC kabla ya Manara kuondoka kwa wekundu hao wa Msimbazi.

Katika sherehe ya siku ya kuzaliwa ya Manara iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Diamond Platnumz amethibitisha kuwa amehamia Yanga SC kumfuata Msemaji huyo ambaye kwa sasa yupo mitaa ya Twiga na Jangwani licha ya kuwa kwenye kifungo cha miaka miwili.

Diamond Platnumz amesema: “Haji Manara uliopo wewe na mimi nipo, niliingia kwenye kushabikia soka wakati sijui kitu chochote kwenye masuala ya soka lakini nilikufuata wewe (Haji Manara) na nikawepo pale uliopo.”

Diamond Platnumz amesisitiza kushabikia timu hiyo ya wananchi huku akiwataka kufanya vizuri katika michezo yake ili yeye na wengine waendelee kubaki kushabikia timu hiyo, amesema wanapaswa kufanya vizuri kama walivyofanya msimu uliopita wa 2021-22.

“Nampongeza sana Rais wa Klabu, Mhandisi Hersi Said kwa jitihada zake za kuifanya Yanga SC kuwa bora katika kipindi chote tofauti na zamani, ambapo mambo yalikuwa mabaya,” amesema.