Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dodoma

Wizara ya Maliasili na Utalii imeanza maandalizi ya ujenzi wa Makumbusho kubwa ya Marais wa Tanzania Jijini Dodoma kwa lengo la kuhifadhi Urithi wa mchango mkubwa walioutoa na unaoendelea kutolewa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana alipotembelea eneo itakapojengwa Makumbusho hiyo Chisichili, jijini Dodoma ambapo amesema ujenzi huo unaenda sambamba na adhma ya Serikali ya kuiendeleza Dodoma kama Makao Makuu ya Serikali.

Aidha, Waziri Balozi Dkt Chana amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuinyanyua Sekta ya Maliasili na Utalii kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwezeshaji wa ujenzi wa Makumbusho hiyo muhimu kwa ustawi wa Taifa.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Kale Dkt. Kristowaja Ntandu ameeleza kuwa hatua mbalimbali za maandalizi ya ujenzi huo zimeshafikiwa na nyingine zinaendelea zikihusisha ukusanyaji wa taarifa muhimu za Marais pamoja na uandaaji wa michoro ya Makumbusho hiyo.

Akizungumzia faida ya Makumbusho hiyo kwa wakazi wa Chisichili na Tanzania kwa ujumla, Mwenyekiti wa Mtaa wa eneo itakapojengwa makumbusho hiyo Bw John Wami, amesema licha ya uhifadhi wa Urithi wa Historia ya viongozi hao wa juu pia vijana wengi watapata ajira na kufanya biashara zaidi kutokana na ujio wa wageni katika eneo hilo.