Sijui nianze na salamu gani katika waraka wangu huu, lakini cha msingi ni kujuliana hali kwa namna yoyote ile, kwa mujibu wa waraka wangu napenda kuwajulia hali kwa namna ya salamu zenu za itikadi ya dini na protokali izingatiwe.

Wiki jana Mheshimiwa Rais alikutana na viongozi wa dini pale Ikulu, kwa namna alivyokuwa akiongea nao akili yangu iligeuka na nikaona ni kama majadiliano ya hatima ya maendeleo ya taifa letu.

Walikuwepo viongozi ambao walibaki kimya na kuonyesha kwamba kuna mambo hawakubaliani na wenzao, wapo ambao waliibuka na hoja zao na zikapingwa hapohapo na wenzao, kwangu mimi niliona kama lilifanyika bunge la aina yake Ikulu.

Watumishi wa Mungu waliwawakilisha waumini wao, hasa ukizingatia wako jirani sana na waumini wao, wanajua matatizo yao ya kiroho na kimwili, wanajua matatizo yao ya mahitaji ya kila siku na namna ambavyo wangedhani serikali inaweza kuyatatua kwa namna yake ya kiroho na kimwili.

Sitaki kuliita lile ni bunge, lakini nashawishika kwa sababu kila kiongozi wa dini alikuwa anawakilisha kundi kubwa la watu nyuma yake, hivyo niliona kama bunge fulani ambalo lilikuwa hakuna upinzani wa hoja, kuna wakati walikuwa wakipongezana kwa makofi pale mwenzao alipotoa hoja yenye kuakisi kukubaliwa na upande wao.

Walionyesha msisitizo wa hoja kwa pamoja, kila aliyesimama alimpongeza au aliongeza pale ambapo mjumbe aliyemaliza na kuketi alitoa hoja, lilikuwa ni bunge ambalo ni kama la vyama vingi kutokana na kupishana kwa itikadi zao lakini waliheshimiana na waliweka msimamo mmoja kwamba kila mwenye itikadi yake ajali itikadi za pamoja za uzalendo, amani na upendo.

Walisikilizana na kuheshimiana sana, hawakuzomeana, wala hakuna aliyeonyesha dharau kwa mwenzake, waliweka itikadi zao mbali na majadiliano, walisimamia katika mambo ya msingi ya utu, uzalendo, upendo na maadili katika jamii ambazo wanaziongoza.

Walimuomba kiongozi wao siku hiyo ambaye alikuwa kama spika wa bunge lao kuangalia mambo yanayoisumbua jamii katika kutafuta ustawi wa pamoja bila kujali kama waumini wote wana  itikadi tofauti.

Nilichojifunza katika bunge lile ni kwamba, kumbe dini ni zaidi ya neno la Mungu, viongozi wengi kama si wote wana uwezo zaidi wa kutuombea kuhusu dhambi zetu, ni wachambuzi wazuri sana katika masuala ya utamaduni wa staha ya Mtanzania.

Ni wachumi waliobobea na washauri wazuri mno katika sekta ya fedha, vilevile ni viongozi nje ya mazingira ya madhehebu yao. Kwa hakika kulikuwa na kitu kikubwa sana ambacho Watanzania tulipaswa kujifunza kutoka katika kikao kile ambacho mimi kwa uzuzu wangu niliona kama kikao cha bunge la ghafla na ambalo halitambuliki kisheria lakini hoja zao zilikidhi viwango vya kazi za kikamati.

Kwa uzuzu wangu nilifikiri mambo ambayo ni vigumu kuthaminika mbele ya wasomi, niliona jinsi ambavyo tunaweza tukawa na vikao vya hawa viongozi wa dini vinavyotakiwa vijitegemee ili kujadili matatizo ya wananchi wengi.

Kwa wakati mmoja na kwa kufanya hivyo kutapunguza gharama ya maoni kwa kutowalipa posho na marupurupu mengine ambayo labda wengi wao wasingependa kulipwa kwa kazi wanayofanya.

Najua muundo wa serikali yetu kwamba hairuhusiwi kuwa na bunge jingine zaidi ya lile ambalo lipo kisheria, lakini sioni mahali ambapo panamzuia rais kuwa na vikao vyake vya mara kwa mara na viongozi wa dini na kuwaita viongozi waandamizi wa serikali kupokea maoni kutoka kwao kama ambavyo wanafanya katika bunge lililopo kisheria chini ya spika.

Sikuwahi kujua kama kuna vichwa vyenye mambo makubwa kwenye dini, sikuwahi kufikiria kama tuna wataalamu wa kila nyanja huko na wanatoa maoni yanayofurahisha, nikiri kwamba ningependa bunge lao lionyeshwe ‘live’.

Wale ‘wabunge feki’ walilalamikia mavazi, ndoa za jinsia moja, rushwa, ajira, baadhi ya watendaji wabovu wa serikali, ukiritimba, uwekezaji na hatima ya taifa la furaha na maendeleo baada ya kuchapa kazi. Nawapongeza sana na ninaomba Mheshimiwa Rais ikikupendeza kutana nao mara kwa mara, ni kwa manufaa ya wapigakura tuliomo katika dini.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

Please follow and like us:
Pin Share