Kila mtu aliyepo duniani ana sababu ya kwanini alizaliwa. Mungu haumbi mtumba.

Mungu anaumba vitu orijino kabisa. Hakuna aliyezaliwa aje duniani kuzurura.

Hakuna aliyezaliwa aje kusindikiza wengine duniani. Maisha ni zawadi tuliyopewa na Mwenyezi Mungu. Kuna kila sababu ya kuketi chini na kujiuliza umefanyia kazi gani zawadi hiyo?

Kila mtu tunayekutana naye ana umuhimu wake katika sehemu fulani ingawa unaweza usiuone leo.  Mheshimu kila mtu unayekutana naye. Kama ni mzazi, usiwabague wanao na kuona kwamba mtoto fulani anaweza kuwa na maisha mazuri kesho, kumbe umdhaniaye ndiye siye.

Umewahi kusikia hadithi za wazazi waliowakataa watoto wao? Mara nyingi watoto wengi waliokataliwa au kukimbiwa na wazazi ndio wamekuwa watu mashuhuri duniani.

Ben Carson akiwa na miaka minane, baba yake Robert Solomon Carson aliitelekeza familia yake. Yeye na ndugu yake walilelewa na mama yao, Sonya Carson, ambaye alikuwa hajui hata kusoma. Ben Carson akawa daktari bingwa wa masuala ya ubongo na Curtis akawa injinia.

Ben Carson amekuwa mmoja wa watu waliowahamasisha watu wengi duniani. Usimdharau usiyemjua. Kuna aliyenunua gari lake akaandika: “Jiwe walilokataa waashi…”

Baada ya Les Brown kuzaliwa  na pacha wake, Wesley Brown, mama yao aliwapeleka katika kituo cha yatima. Mamie Brown aliyekuwa akiuza kahawa akawachukua. Kilichobaki ni historia. Leo hii Les Brown ni mhamasishaji mashuhuri duniani na mwandishi wa vitabu.

Baada ya Abramu na Sarai kukosa mtoto, Sarai akakosa uvumilivu. Alikuwa na kijakazi, Mmisri, jina lake Hajiri. Sarai akamwambia Abramu azae na yule kijakazi. Hajiri akapata mimba.

Sarai alipoona hayo yametokea akaanza kumchukia na kumtesa Hajiri. Hajiri akakimbia kutoka katika nyumba ya Abramu.  Malaika wa Bwana akamwona kwenye chemichemi ya maji katika jangwa.

Akamwambia: “Hajiri wewe mjakazi wa Sarai unatoka wapi, nawe unakwenda wapi?”

Akasema: “Nakimbia kutoka kwa bibi yangu Sarai.”

Malaika wa Bwana akamwambia: “Rudi kwa bibi yako, ukanyenyekee chini ya mikono  yake.” Hajiri akamzalia Abramu mwana wa kiume, Abramu akamwita Ishmaeli. (Mwanzo 16).

Baada ya ndugu zake Yusufu kumtupa shimoni, wakakaa kitako kula chakula, wakainua

macho, wakaona msafara wa Waishmaeli wanakuja wakitoka Gileadi kuelekea Misri.

Yuda akawaambia ndugu zake: “Kwafaa nini kumuua ndugu yetu na kuificha damu yake? Haya na tumuuze kwa hawa Waishmaeli, wala mikono yetu isimdhuru, maana yeye ni ndugu yetu na damu yetu.” Ndugu zake wakakubali.

Waishmaeli walipofika wakamtoa Yusufu shimoni, wakamuuza kwa vipande ishirini vya fedha; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri.

Waishmaeli waliomnunua Yusufu ni uzao ule wa Ishameli, mtoto wa Hajiri na Abramu ambao Sarai aliuchukia. Inawezekana bila Waishmaeli kupita katika sehemu ile aliyokuwapo Yusufu, Yusufu angeweza kuachwa humo shimoni na kufa na asiweze kutimiza ndoto zake.

Nikukumbushe tu, Abramu alimzaa Isaka, Isaka akawazaa Yakobo na Esau. Yakobo ndiye baba wa Yusufu. Hivyo Yusufu alikuwa kitukuu cha Abramu. Hii ni miujiza iliyotokana na makosa.

Ishmaeli alizaliwa na kuonekana kama kosa, lakini kadiri siku zinavyokwenda Ishmaeli anageuka na kuwa baraka kwa Yusufu. Hakuna aliyezaliwa kimakosa.

Kama unapumua hadi leo hii mshukuru Mungu kwa maana uhai ni zawadi ya pekee. Siku moja nilikutana na mtu aliyekata tamaa nikamuuliza: “Maisha yanakwendaje?”

Akanijibu: “Cha muhimu uhai.” Si muhimu leo hii maisha yako ni magumu kiasi gani, si muhimu leo hii unapitia changamoto gani. Si muhimu umetupwa kwenye shimo kama Yusufu, kigezo kwamba unaendelea kuishi na kupumua hewa safi ya Oksijeni kikupe hamasa kwamba kuna sababu ulizaliwa na unaendelea kuishi.

Kuna aliyewahi kusema: “Ulipendwa siku ulipozaliwa, utapendwa tena siku utakayokufa, humo jitahidi kuvumilia.” Maisha yanahitaji uvumilivu wa hali ya juu.

Maisha bila uvumilivu hayanogi. Maisha bila uvumilivu hayana maana. Anashinda yule anayevumilia. Sungura aliposhindwa kuruka kuufikia mkungu wa ndizi akasema: “Sizitaki mbichi hizi.”

Jiulize maswali haya: Kwanini nilizaliwa? Kwanini naendelea kuishi?

Kama leo hii ingekuwa siku ya mwisho kuishi ningefanya jambo gani kwa ubora?

Please follow and like us:
Pin Share