Nianze kwa salamu za mwaka mpya kwa wasomaji wetu wote, najua tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kutuvusha mwaka huu, mwaka jana ulikuwa na mambo yake, yapo yaliyokuwa ya heri kwetu na yapo ambayo kwa kweli yalizikera nafsi zetu, lakini pamoja na yote tuna kila sababu ya kushukuru.

Nilikuwa sijui kama miaka inakimbia kiasi hiki, mara mwaka jana imekuwa historia, ina mema yake, tumeona mambo mengi, vifo na kuzaliwa waja wengine, tumeona ndoa na kuvunjika kwa ndoa, tumeona maendeleo ya muda mfupi na matarajio ya muda mrefu, siku chache zijazo tutaanza maandalizi ya kuupokea mwaka mpya, miaka inakimbia tofauti na zamani.

Katika utabiri wangu wa kinabii kuna mdau alinikumbusha kwamba katika baadhi ya majiji kutakuwa na upungufu wa watu, na watu hao wengi watahamia vijijini na huenda ile dhana ya vijiji vya zamani ikarejea, inawezekana tukarahisisha huduma za jamii kwa wananchi kwa kukaa pamoja na kupunguza msongamano wa watu mijini, hili kama nabii nilikwisha kulitabiri kwamba kuna siku mjini watabaki wa mjini na wale waliokuja kupambana na ujanja wa kizamani watasalimisha maisha katika kilimo.

Hivyo basi, natabiri kuongezeka kwa wakulima na wafugaji, natabiri wakulima wengi ambao ni Watanzania halisi wataingia kubomoa mapori katika kipindi hiki, natabiri kuwepo mifugo ya kutosha, natabiri kutenguliwa kwa baadhi ya viongozi wa sekta hiyo ambao watabweteka bila kujua kwamba mambo yamebadilika, ili wasitenguliwe wajitahidi kuangalia mahitaji ya wakulima na wafugaji, waangalie masoko na bei halisi ya bidhaa zao.

Bado natabiri uwepo wa chakula  cha kutosha na nchi kutoingia katika baa la njaa, natabiri kuuza nje zaidi iwapo mipango mikakati itafanywa na wahusika kwa wakati bila kufanya kazi kimazoea, mifano tumeiona, hivyo jitihada zao zitakuwa kumkomboa mkulima, ukimkomboa mkulima na mfugaji katika nchi hii hautaulizwa kuhusu suala la ajira na kipato cha mwananchi, ndiyo sekta pekee ambayo inaweza kuajiri kila mtu kwa wakati.

Natabiri shule za binafsi kususha ada katika miaka michache ijayo, hii itakuwa sanjari na kufunga mambo ya starehe kwa kuzingatia umuhimu wake, natabiri shule nyingi za binafsi kupata wanafunzi wachache zaidi kuliko kipindi chochote, vilevle natabiri shule za serikali kujaa pomoni kutokana na hali ya kiuchumi ilivyo, ni suala la muda tu kufikia katika miaka ile ya shule za serikali ambayo inagharamia kila kitu, yote tuyaombee heri na yafanikiwe ili kila mtu aweze kutimiza mambo muhimu kwa mahitaji muhimu kwa maisha yake.

Unabii wangu unanituma kutabiri utunzaji wa mazingira, si kwa sababu viongozi wanasisitiza, la hasha! Bali kwa sababu kila mtu atajua umuhimu wa kupanda miti na matumizi ya baadhi ya vitu vya hatari kwa maisha ya binadamu kuachwa kutumika, natabiri mvua kuendelea kuwepo kutokana na utunzaji wa mazingira, mito kujaa na ufugaji kuneemeka.

Kama unabii wangu wa wiki jana, natabiri kutumia mbadala wa takataka, sasa hivi naona jinsi ambavyo nishati ya jua ilivyo na nguvu na mashiko kwa wananchi hata wa mijini, natabiri matumizi mazuri ya takataka na umiliki wa takataka badala ya kuwa mali isiyo na mwenyewe, natabiri usafi wa maeneo hususan yale yanayokaliwa na watu wengi.

Kutokana na miaka kukimbia bila huruma na mambo ya msingi kuendelea kuwepo, natabiri watu wataanza kuchagua marafiki wa maana kwao, wale marafiki wa kupiga ‘story’ na kudanganyana mambo ya kijinga wataachwa, sasa watabaki marafiki wenye mtazamo chanya na si hasi, watabaki marafiki wavuja jasho na si marafiki wafuja mali.

Natabiri wanafiki walioshindwa kujiongeza katika maisha kuanza kujitokeza kwa wachapakazi, wataongeza unafiki wao na jamii itawatambua kwa kutofanya kazi, natabiri unafiki kuanza kupungua, kula kwa mafuta ya mgongo wa chupa itakuwa hadithi siku chache zijazo, natabiri vifo vya kiushikaji ambavyo vilikuwa kwa ajili ya watu kuendesha maisha yao.

Natabiri biashara halisi na si ya kubabaisha kwa bei, natabiri faida halisi ya asilimia kumi kutafutwa, natabiri kila mtu kufanya anachokijua na si kuwa machinga wa kila kitu, natabiri ubabaishaji kwisha, na hiyo ndiyo itakuwa mwishoni mwa mwaka 2019 kabla ya kuingia mwaka mpya.

Wasalamu,

Mzee Zuzu, 

Kipatimo.

By Jamhuri