Yanga, Simba, Azam usajili wa bilioni utavuna nini CAF?

DAR ES SALAAM

Na Andrew Peter

Usajili wa Yanga, Simba na Azam msimu huu hakuna shaka klabu hizo kwa pamoja zimekwisha kutumia zaidi ya Sh bilioni moja katika kuwanasa nyota hao.

Ni jambo zuri kuona klabu zetu zimeamua kuvunja benki na kununua wachezaji bora kwa lengo la kuimarisha timu kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu pamoja na mashindano ya kimataifa.

Baadhi ya wachezaji waliosajiliwa Yanga ni Azizi Ki (Ivory Coast), Joyce Lomalisa (DR Congo), Gael Bigirimana (Burundi), Bernard Morrison (Ghana), Lazarous Kambole (Zambia).

Wakati Simba imewanasa Augustine Okrah (Ghana), Victor Akpan (Nigeria), Moses Phiri (Zambia), Nassor Kapama na Habib Kyombo (Tanzania).

Huku Azam imewasajili wachezaji wawili ambao ni Kipre Junior na Tape Edinho (Ivory Coast), Isah Ndali (Nigeria), James Akaminko (Ghana) na kipa Mcomoro Ali Ahamada na Watanzania Cleophace Mkandala, Abdul Sopu na Nathaniel Chilambo.

Kwa aina hii ya usajili ni wazi viongozi wa klabu hizi tatu malengo yao hayatakuwa kuchukua ubingwa wa ligi na Kombe la FA pekee, bali ni kuona timu hizo zinafanya vizuri zaidi katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

Nasema hivyo kwa sababu katika misimu minne iliyopita Simba imetengeneza historia iliyotukuka kwa kufuzu mara mbili kwa hatua ya makundi ya mashindano ya Afrika, jambo lililoiongezea Tanzania nafasi ya kupata wawakilishi wanne katika mashindano hayo.

Rekodi hiyo ya Simba hakuna shaka nayo kwa namna moja au nyingine imewachochea viongozi wa Yanga na Azam kuona ni wazi wana wajibu wa kufanya kwa kuhakikisha klabu zao zinafanya vizuri katika msimu huu.

Naamini mashabiki wa timu hizi waliokuwa wakikesha usiku na mchana kutaka kuona timu zao zinafanya usajili wa nyota gani, ni wazi wamepata furaha kubwa kwa namna viongozi wao wanavyofanya jitihada kuwanasa nyota hao wa kimataifa na kuwawaleta nchini.

Kila shabiki kwa sasa amebeba matumaini makubwa ya kuona timu yake inachukua ubingwa na kufanya vizuri kimataifa kutokana na ubora wa wachezaji waliosajiliwa.

Hapa ndipo naiona presha kubwa kwa wachezaji hawa waliosajili pamoja na makocha katika kuhakikisha wanakata kiu ya mashabiki wao pamoja na viongozi wa klabu hizo.

Mashabiki wa Tanzania hasa wa timu hizi kubwa wana tabia ya kutoamini kwamba timu yao inaweza kufungwa na timu ndogo, kwa sababu tu wamesajili wachezaji wa kimataifa wengi bila ya kujali mazingira mengi ya mchezo.

Jambo la kutotaka timu yao isifungwe litawaweka katika mazingira magumu wachezaji wakikosea kidogo watazomewa na kutolewa lugha chafu, kitu kinachoweza kuwatoa mchezoni.

Viongozi pamoja na jitihada yao kubwa ya kusajili, lakini hawatakuwa salama kwa mashabiki wao wakiwataka wawafukuze makocha kwamba hawana uwezo, kisa tu timu imefungwa mechi moja au mbili au kupata sare.

Jambo hili tumeona likitokea kila wakati, ni vema viongozi wakajua kuna raha ya kusifiwa kusajili, lakini kuna machungu ya kutaka kutimiza ndoto za mashabiki wao, hivyo inawabidi wawape taarifa mapema wachezaji na makocha wajue hali hiyo itaanza hata Simba Day au Siku ya Wananchi, achilia mbali katika mchezo wa Ngao wa Jamii.

Wala sitashangaa kuona makocha wa Simba, Yanga na Azam wakifukuzwa baada ya mechi tano tu, huku wachezaji wengi wakitolewa kwa mkopo au kutupiwa virago wakati wa dirisha dogo la usajili, yote kutokana na presha ya mashabiki kwa viongozi wao.

Mbali ya hayo, naamini Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi watakuja na ratiba bora zaidi itakayotoa mazingira sawa kwa timu zote za Ligi Kuu.

Pamoja na Yanga, Simba na Azam kufanya usajili wa mamilioni, bado zitahitaji mbeleko ya TFF na Bodi ya Ligi katika panga – pangua ya ratiba ya Ligi Kuu ili kutengeneza mazingira ya kushinda mechi zao kwa kisingizio cha kucheza mashindano ya kimataifa.

Katika upangaji wa matokeo ya timu, kigezo cha timu moja kupewa viporo vingi au kuwa na ratiba inayotoa nafasi kubwa ya kupumzika kwa timu hizi kubwa kuliko wapinzani wao ni ishara ya kuibeba timu na kupanga matokeo.

Pia nawakumbusha viongozi wa Yanga, Simba na Azam kwamba tumeona usajili wao ukiwa bora zaidi, sasa tunataka kuona timu hizo zikipata matokeo uwanjani, si kwa mbinu zao za nje ya uwanja.

Ni kawaida kusikia viongozi wa klabu hizo wakishutumiana kuhusu suala la rushwa na kashfa ya kuhonga wachezaji wa timu ndogo au waamuzi ili kununua ushindi katika mechi zao.

Mpira unaochezwa nje ya uwanja katika ligi yetu umechangia kwa sehemu kubwa klabu zetu kushindwa kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.

Wachezaji wa klabu zetu wameshindwa kutengenezwa kwa ushindani, kwa sababu viongozi wamekuwa wakitumia fedha nyingi kurahisisha matokeo ya uwanjani.

Mwisho, usajili huu wa wachezaji wengi wa kimataifa ni mzuri kwa klabu zetu – hakuna ubishi, lakini ni hatari kwa timu yetu ya Taifa Stars.

Nasema hivyo kwa sababu endapo klabu hizi kubwa zitaamua kuwatumia wachezaji wanane wa kigeni katika mechi za ligi kama kanuni inavyosema na kule kimataifa ikiwatumia wote 11, tusitarajie kuwa na Taifa Stars bora.

Unaweza kusema mbona klabu nyingine zina wachezaji wengi wazawa – sawa, lakini wanakosa uzoefu wa kucheza mechi za kimataifa ukilinganisha na wale waliopo Simba, Yanga na Azam, kwa hiyo itakuwa changamoto kwa Kocha Kim Poulsen katika kutimiza ndoto ya Tanzania kucheza AFCON.

Hata ukiangalia Stars kwa sasa kuna namba zimeanza kuwa na changamoto ya kukosa wachezaji bora, hii yote kwa sababu katika klabu zetu wamejaa wachezaji wa kigeni.

Ni kanuni nzuri kuruhusu timu kusajili wachezaji 12 wa kigeni, lakini inaumiza timu ya taifa kwa muda mrefu na nadhani inapaswa kutazamwa na idadi ya wachezaji wa kigeni wanaopaswa kuanza ili kuwalinda wachezaji wetu.