Wenyeji, Yanga SC wamelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Al Hilal Omdurman ya Sudan katika mchezo wa kwanza wa Hatua ya 32 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika leo Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Yanga walitangulia kwa bao la mshambuliaji wake tegemeo, Fiston Kalala Mayele dakika ya 50, kabla ya El Hilal kusawazisha kupitia kwa Mohamed Yousif dakika ya 67.

Timu hizo zitarudiana Oktoba 16, yaani Jumapili ya wiki ijayo Uwanja wa Al-Hilal Stadium Jijini Omdurman nchini Sudan na mshindi wa jumla atakwenda Hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Timu itakayotolewa itakwenda kumenyana na timu ya Kombe la Shirikisho kuwania kucheza Hatua ya makundi ya michuano hiyo midogo ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).