Zahoro Matelephone arejea Dar

Mfanyabiashara anayedaiwa kujihusisha na usafirishaji na uuzaji dawa za kulevya nchini Zahoro Khamis Zahoro (Zahoro Matelephone) amerejea nchini kimya kimya baada ya kudaiwa kukamatwa katika nchi za Falme za Kiarabu.
Matelephone ni mfanyabiashara anayemiliki maduka kadhaa ya simu za mkononi jijini Dar es Salaam.
Matelephone amerudi nchini wiki moja iliyopita ambako baada ya kuwasili alifanya mawasiliano na ndugu zake wa karibu ikiwa ni pamoja na kukutana nao na kufanya mazungumzo kuhusu mikasa iliyomsibu.
Watu walio karibu naye wameiambia JAMHURI kwamba afya yake inaonekana kudhoofu.
Mmoja wa watu hao amesema Matelephone aliingia nchini kimya kimya na hapendi watu wafahamu ujio wake kutokana na mikasa iliyomkumba miaka miwili iliyopita.
Alieleza kuwa  miezi miwili iliyopita, mmoja wa ndugu zake alienda Oman kufanya mipango ya kumsaidia Matelephone kuweza kuachiwa huru; jambo ambalo limefanikiwa.
Ameoonekana eneo la Magomeni Kagera jijini Dar es Salaam kwa baba yake mzazi na pia eneo la Manzese
Gazeti hili lilifika katika jengo lake lililopo Shule ya Uhuru, Kariakoo ambako lilikuta jengo hilo likiwa limevunjwa na kuanza kujengwa upya huku ujenzi huo ukibainisha Zahoro kuwa mmiliki wa jengo hilo la kibiashara.
Hata hivyo, JAMHURI liliendelea kufanya juhudi za kumpata na kufika katika maduka yake ya simu za mkononi yaliyopo katika mzunguko wa barabara ya Shule ya Uhuru ambako lilifanikiwa kuzungumza na mdogo wake, Humud.
Humud hakuwa tayari kueleza wapi kaka yupo, lakini akasema kuwa ndugu yake huyo amesafiri nje ya nchi. Hata hivyo, baadhi ya wafanyakazi waliozungumza na JAMHURI walidai kwamba Matelephone yupo jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Kikosi cha Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya nchini Godfrey Nzowa, anakiri kwamba ofisi yake imepata taarifa za kukamatwa kwa Matephone, lakini haijapata taarifa zozote kuhusu ujio wake nchini.
Nzowa anasema kuwa ofisi yake haikuhusishwa juu ya kukamatwa kwake kutokana na tukio hilo kufanyika nje ya nchi.
“Tutamfuatilia kwa ukaribu zaidi iwapo ataendelea na biashara yake hiyo ya dawa za kulevya tutamkamata tena bila tatizo lolote, maana wafanyabiashara hii ni vigumu kuacha, nakuhakikishia tutamkamata tena akithubutu kufanya hii biashara kwa mara nyingine,” anasisitiza Kamanda Nzowa.
Matelephone anadaiwa kukamatwa na vyombo vya dola katika nchi za Falme za Kiarabu, Novemba 2013 kwa madai ya kukutwa na dawa za kulevya. Mkewe anadaiwa kuwa miongoni mwa waliokamatwa.
Taarifa zinaeleza kuwa mwaka mmoja kabla ya kumatwa kwake, yaani mwaka 2012 alihamia Oman baada ya biashara zake hapa nchini kuyumba.
Zahoro Matelephone ni miongoni mwa watu waliowahi kuvuma hapa nchini na kuwa karibu na viongozi wa ngazi za juu za serikalini na katika vyombo vya dola. Mara kadhaa ameshirikishwa kwenye safari za Rais Jakaya Kikwete nje ya nchi akitambulishwa kama mmoja wa wafanyabiashara nguli nchini.