Zambia inaihujumu Tanzania Tazara?

Mbao, saruji vyapungua Tazara

Miaka ya nyuma, mbao za kila aina kutoka Iringa, na saruji kutoka mkoani Mbeya ilikuwa vikisafirishwa kwa wingi na kushushwa Tazara. Kwa sasa ukiingia katika yadi unashangaa. Mbao utadhani zimeletwa na lori moja.

Gazeti la JAMHURI lilipofuatilia na kuuliza sababu za kupungua kwa mzigo wa mbao, maelezo yaliyotolewa yalikuwa kichekesho.

Kwa utaratibu wa siku zote, Tazara ilikuwa na wajibu wa kupeleka mabehewa sehemu mbalimbali zinazozalisha mbao katika vituo maalumu walivyokubaliana kama SPM Mgolole. Mbao za kutosha zilikuwa zinapakiwa kwenye mabehewa na kisha kusafirishwa kuja Dar es Salaam.

Kinachotokea sasa ni kwamba eti uongozi wa Mamlaka, kwa makusudi, umeamua kuacha kuwapelekea mabehewa wasafirishaji wa mbao, hivyo wanakata mbao na kurundikwa hadi ninaozea chini, hatimaye wanaachana na subira na kuamua kutumia malori kusafirisha mbao.

Kiwanda cha Saruji cha Mbeya nacho kimeacha kusafirisha saruji kuja Dar es Salaam, baada ya uongozi wa juu wa Mamlaka, kwa makusudi, kuamua kupandisha bei ya kusafirisha saruji kwa kiwango ambacho mteja hawezi kupata faida akitumia reli ya Mamlaka hiyo.

“Unawaambia kila mfuko Sh 8,000 wakikataa unasusa. Tazara kama mfanyabiashara ilipaswa kuzungumza nao kama wao wanaweza kulipa kiasi gani, kisha tukaingia kwenye majadiliano na kufikia maafikiano.

“Lakini kinachotokea sasa hivi ni kuwa uongozi unasema ‘kama hataki basi’. Wanaiona Tazara kama ‘mtakuja’ na kweli, ameacha hakuna tunachopata,” ameongeza Mleke.

Kilombero na molasisi

Kiwanda cha Sukari cha Kilombelo nacho kinachohitaji ni kupelekewa mabehewa tu, na kinalipa gharama za usafirishaji hata kabla ya kusafirisha mzigo, lakini uongozi wa Tazara umeacha kupeleka mabehewa Kilombero.

Hivyo wenye kiwanda cha Kilombero wanaotafuta kwa udi na uvumba jinsi ya kusafirisha molasisi kuja Dar es Salaam, kwa sasa wanalazimika kutumia malori.

Sasa unaweza kujiuliza ni kwa faida ya nani haya yote yanafanyika? Ila zipo hisia za hujuma na kwamba zimepangwa kimkakati na taifa mshirika wa Zambia.