Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Nkasi
Mtoto mmoja aliyefahamika kwa jina la Jenifa Mafuru (8) mkazi wa Kijiji Cha Ipanda kata ya Nkomolo amefariki Dunia baada ya kusomwa na maji alipokuwa akivuka.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kamanda wa Polisi mkoa Rukwa SACP Shadrack Masija ni kuwa mtoto huyo alifariki Aprili 28,2026 majira ya saa 9 alasiri alipokuwa akivuka mto kupelekea Shambani kwa Babu yake.
Amesema kuwa mtoto huyo akiwa ameongozana na wenzie wawili wakifika kwenye mto huo wa Natene ambapo marehemu aliwashawishi wenzie wauvuke mto huo lakini wenzie walikataa na ndipo yeye alipojitosa ndani ya mto huo na kumbe ilikua na kina kirefu ndipo aliposombwa na maji na kupelekea umauti wake.
Awali Mwenyekiti wa Kijiji hicho Cha Ipanda Izack Ladislaus Wamanyala amesema kuwa walipata taarifa za kifo Cha mtoto huyo majira ya saa 9:30 alasiri ndipo Wananchi walipojitosa ndani ya maji kwenda kumtafuta mtoto huyo.
Amefafanua kuwa wakati zoezi la wananchi la kumtafuta mtoto huyo ndani ya mto likiendelea wao kama uongozi wa Kijiji walitoa taarifa Jeshi la Zima Moto na Uokozi pamoja na Polisi ambao wakifika kwa wakati na kuungana kutafuta miwili wa mtoto huyo.
Amesema kuwa jitihada za kumtafuta mtoto huyo zilizaa matunda ingawa alikutwa akiwa amefariki Dunia na mazishi yake yamefanyika leo jumatano kijijini hapo.
Mwisho


