Polisi Kata Kata ya Nawenge, iliyopo Wilaya ya Ulanga Mkoani Morogoro, ametoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nawenge na kuwapa mbinu kuhusu namna ya kuepukana ukatili na kuripoti vitendo vya ukatili.

Akizungumza na wanafunzi hao, Staff Sajenti wa Polisi (SSGT) Sabas Rovetha amesema kuwa ni muhimu kwa wanafunzi kutoa taarifa pindi wanapokumbana na vitendo vya ukatili kutoka kwa watu wasio na nia njema na maendeleo yao ya kitaaluma.

Ameeleza kuwa zipo njia mbalimbali za kuripoti matukio hayo, zikiwemo klabu za Marafiki wa Polisi, FEMA, Haki Elimu, majukwaa ya Twaweza, walimu, wazazi pamoja na vituo vya polisi, ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa wakati.

Aidha, amesisitiza kuwa utoaji wa taarifa utasaidia kulinda haki za wanafunzi, kukuza taaluma zao, na kukomesha vitendo vya ukatili mashuleni amewataka wanafunzi kutokukaa kimya wanapokumbana na changamoto hizo.

Sambamba na hilo, SSGT Rovetha amewahimiza wanafunzi kuzingatia masomo yao na kusoma kwa bidii na kuepuka utoro, akibainisha kuwa utoro ni kikwazo kikubwa kwa mafanikio ya kitaaluma.