Na Fauzia Mussa – MAELEZO, Zanzibar
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, kazi Uchumi na uwekezaji Al Hajj Shariff Ali Shariff amesema Serikali inaendelea kuwatambua na kuwathamini viongozi wote walitangulia mbele ya haki kwa mchango wao katika kuipigania Nchi.
Akitoa nasaha mara baada ya kukamilika kwa dua ya kumuombea aliekuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar Bregedia Ramadhan Haji Faki katika Maadhimisho ya Wiki ya Kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa na Waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar huko Mkwajuni.
Amesema Kiongozi huyo ameacha historia kubwa kwani alipigana hadi kuhakikisha Zanzibar inakomboka kutokana na makucha ya wakoloni .
” Brigedia Ramadhani alipigana na kuwa mzalendo Hadi kuhakikisha Nchi hii inapata mapinduzi bila kujali majeraha aliyokuwa akiyapata katika mapigo hayo.”Alieleleza
Aliwataka Vijana kuiga ujasiri na uzalendo walikuwa nao viongozi hao ili kudumisha Mapinduzi yaliyofanywa na waasisi waliokwisha tangulia mbele ya haki.
Hata hivyo amewataka familia na wananchi Kwa ujumla kuendelea kumuombea dua kwa Mwenyezi Mungu amsamehe makosa yake na amuweke mahala pema peponi ,Amin .
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Rashid Hadid Rashid amesema April mosi Hadi 7 ni wiki maalum ya kuomboleza Kwa kuwaombea dua viongozi ambao wameacha alama ndani ya Zanzibar jambo ambalo linaleta faraja Kwa familia za viongozi hao.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Familia Ali Ramadhan Haji amesema Mzee wao alijitoa Kwa Serikali na jamii na wanachoamini kuwa uliolala ni mwili tu wa mzeee wao na sio utendaji wake.
Aidha ameishukuru Kwa dhati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi waliofika kuwaunga mkono katika hafla hiyo kwani uwepo wao umepelekea jambi hilo kufanikiwa.
Mapema Bwana Ali alitumia fursa hiyo kutoa pole kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi kwa kuondokewa na mzazi wake siku za karibuni .
Hayati Ramadhan Haji Faki ni miongoni mwa Vijana walioshiriki Mapinduzi ya Zanzibar, na kuwa Waziri Kiongozi na Mjumbe wa Baraza la Kwanza la Mapinduzi 1964 ambae alifariki dunia Machi 2020 jijini Dar-es-salaam alipokua akipatiwa matibabu baada ya kupata mshituko wa moyo na kuzikwa Mkwajuni Magombewa.