Ziara ya ghafla ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Joseph Kabila, katika mji wa Goma ulioko mashariki mwa nchi hiyo, imezua taharuki na mjadala mkali wa kisiasa nchini humo, huku serikali ikiitaja kuwa ni “usaliti wa kitaifa,” wakati wafuasi wake wakisema inalenga kurejesha amani.
Kwa mujibu wa taarifa za uhakika, Kabila alitia timu usiku wa manane kwa njia ya barabara na kupokelewa na Corneille Nangaa, kiongozi wa kundi la waasi la AFC/M23 linaloshikilia maeneo ya Goma na Bukavu, miji mikuu ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini. Mkutano wa faragha ulifanyika kati ya wawili hao, huku maudhui yake yakibaki kuwa siri.
Ziara hiyo inafanyika kipindi ambacho Seneti ya DRC imeondoa kinga ya kisheria dhidi ya Kabila, hatua inayomfungulia mlango wa kushtakiwa kwa kosa la uhaini kufuatia tuhuma za kuwaunga mkono waasi wa M23.

Wafuasi wa Kabila: “Lengo ni amani”
Ramazani Shadari, Katibu Mkuu wa chama cha PPRD kinachoongozwa na Kabila, amethibitisha ziara hiyo na kueleza kuwa inalenga kutafuta suluhisho la mzozo wa mashariki.
“Kuwasili kwake Goma kunamaanisha kwamba Joseph Kabila anatafuta amani kwa Kongo, sababu yeye alikuwa rais na anafahamu vyema changamoto za taifa. Kwetu sisi tunachotaka ni amani irejee nchini Kongo,” alisema Shadari katika mahojiano na DW.
Aidha, Shadari alisisitiza kuwa ziara hiyo siyo ya kichochezi kama inavyodaiwa, bali ni ya maridhiano na utulivu wa kitaifa, akiongeza kuwa chama cha PPRD hakitatishika na hatua ya serikali ya kuzuia shughuli zake.
“Chama ni katika moyo wa mtu na kichwani mwake. Sisi ni wanachama wa PPRD na tutaendelea kuwa wanachama. Wanachokifanya ni mzaha na mchezo mtupu,” alisema Shadari.
Serikali: “Huu ni usaliti”
Serikali ya Rais Félix Tshisekedi imeikosoa vikali ziara hiyo, ikiitaja kama njama ya kuhujumu mamlaka halali. Msemaji wa serikali, Patrick Muyaya, alisema kuwa Kabila hana tena nafasi ya kisiasa nchini humo.
“Tumeona maoni ya Wakongo baada ya hotuba ya Kabila. Maoni ya Wakongo waliowengi kwenye mitandao ya kijamii ni ishara tosha kuhusu wanachofikiria: kwa hakika, Rais Kabila amepitwa na wakati, ambaye hana jambo jipya la kupendekeza kwa ajili ya mustakbali wa taifa,” alisema Muyaya.
“Kwa upande wetu, sisi tunajikita katika kutatua matatizo ambayo yeye Kabila hakuweza kuyatatua wakati alipokuwa madarakani,” aliongeza.
Madai ya njama ya mapinduzi
Hotuba ya Kabila ya tarehe 23 Mei 2025 imeelezwa kuwa kichocheo kikubwa cha mvutano wa sasa. Katika hotuba hiyo, Kabila alimtuhumu Rais Tshisekedi kwa kuendesha taifa kwa udikteta na kulifanya kuwa kichekesho mbele ya jamii ya kimataifa.
“Uongozi wa sasa umelitumbukiza taifa katika mgogoro wa kimuundo na kuifanya Kongo kuwa kichekesho mbele ya dunia,” alisema Kabila.
Kwa upande wake, Corneille Nangaa kupitia ukurasa wake wa X alithibitisha ushirikiano na Kabila akisema:
“Kwa pamoja na Joseph Kabila, tunadhamiria kukomesha kile tunachokiita kuwa ni udikteta na migawanyiko nchini Kongo.”
Je, Kabila anarejea kwa maridhiano au mapambano?
Taarifa za ndani kutoka Goma zinaeleza kuwa Kabila alikuwa na mashauriano ya muda mrefu na watu wake wa karibu, lakini hadi sasa agenda rasmi ya ziara hiyo haijawekwa wazi. Hata hivyo, kwa kuzingatia hali ya kijeshi mashariki mwa DRC na uhusiano wa karibu kati ya Kabila na Rwanda, wachambuzi wanasema kuna dalili kuwa anaweza kuhusika katika harakati za kijeshi au kisiasa dhidi ya serikali iliyoko madarakani.
Tishio la kurejea kwa vita
Kuongezeka kwa mawasiliano kati ya Kabila na viongozi wa waasi wa M23 kunatishia kuvuruga hali ya usalama mashariki mwa DRC na kuanzisha tena mzunguko wa vita vya muda mrefu. Hali hiyo imezua hofu miongoni mwa wananchi na jumuiya ya kimataifa juu ya hatima ya amani ya nchi hiyo yenye historia ndefu ya machafuko.
Wakati dunia ikisubiri hatua ya serikali ya Kinshasa na msimamo wa jeshi, Kabila anaonekana kujiimarisha kisiasa katika eneo lenye mvutano mkubwa, huku serikali ikijaribu kuzuia kile kinachoonekana kama jaribio la kusambaratisha mamlaka halali.