Na Deodatus Balile, Seoul,Korea
“Ukijumulisha dola bilioni 6.4 za Uturuki, ukaongeza angalau dola milioni 500 zitakazotokana na Nishati Safi ya Kupikia za Ufaransa kati ya hizo dola bilioni 2.2 zilizochangwa, ukaweka dola bilioni 2.5 za Korea Kusini, ni wazi katika ziara tatu tu za Rais Samia nje ya nchi katika nchi tatu na katika miezi mitatu, zimeiingizia Tanzania dola za Marekani bilioni 9.4 sawa na Sh trilioni 25.38. Fedha hizi zitajenga miradi ya kudumu kizazi hadi kizadi ikiwamo reli ya kisasa SGR. Ziara za Rais Samia nje ya nchi ni wazi zina faida kubwa kwa taifa.”
Ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan hapa nchini Korea, ikiunganishwa na zile za Uturuki na Ufaransa zinayo nafasi ya kukuza uchumi na kuivusha Tanzania katika kisiki cha umaskini kilichodumu kwa zaidi ya miaka 60 baada ya Uhuru, iwapo Watanzania tutaamua kushiriki kwa vitendo ujenzi wa uchumi wa taifa letu na kuweka siasa nyepesi kando.
Sitanii, yapo maeneo ambayo uchumi wetu hauna muunganiko au misingi ya uzalishaji yanayokwamisha kuzalisha bidhaa na huduma tukauza ndani na nje ya nchi, lakini upungufu uliokuwapo nashuhudia ukiondolewa kupitia ziara hizi na kuipa nchi yetu nafasi ya kujinasua kiuchumi. Katika Mkoa wa Kagera nilikozaliwa, kuna usemi kuwa “Kalitunga agila obwemelo”, ambao kwa tafsiri isiyo rasmi, ni kuwa kila tajiri kuna aliyemshika mkono.
Historia ya Korea Kusini inathibitisha kila mantiki ya msemo huo, kwani leo ninavyoandika makala hii, nchi hii ambayo ilikuwa haifahamiki hata nafasi yake katika uchumi wa dunia na ambayo mwaka 1966 pato la mtu mmoja mmoja lilikuwa chini ya dola 75 kwa mwaka, wakati Tanzania ikiwa na dola 260 kwa mwaka, kwa maana kuwa wakati huo Tanzania ilikuwa tajiri kuliko Korea Kusini, leo Korea Kusini ni nchi ya 12 kwa uchumi mkubwa duniani na pato lake kwa mtu mmoja kwa mwaka ni dola 33,700. Nitalieleza zaidi baadaye hili.
Nchi zilizotoka kiuchumi, kama Korea Kusini, China na Japan, takwimu zote zinaonyesha kuwa Marekani ilizishika mkono, zikazalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu na huduma, kisha zikapata masoko ya uhakika nchini Marekani na Jumuiya ya Ulaya, na huo ndiyo ukawa kwanzo wa kufuta umaskini na kugeuka mataifa tajiri. Leo sisi Tanzania kupitia ziara ya Korea, Uturuki na Ufaransa, wakubwa hawa wamejitoa kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan, kilichobaki ni sisi kuamua kama tunayapokea haya au tunaendelea kuraruana yanatupita.
Mtakumbuka kuwa katika ziara ya mwezi Aprili, 2024 nchini Uturuki Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan ameamua kuipatia Tanzania dola bilioni 6.4 sawa na Sh trilioni 17.3 kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) katika vipande vya kaunzia Dodoma kwenda Kigoma. Huu ni uwekezaji wa kudumu. Nasema ni ziara ya ukombozi kwani reli hii ya Dodoma hadi Kigoma ikijengwa na kuunganisha nchi za Rwanda na Burundi ni uwekezaji wa kudumu.
Sitanii, inawezekana kuna watu wasiolifahamu hili. Reli ya Kati inayotumika sasa ujenzi wake ulikamilika mwaka 1914, yaani miaka 110 iliyopita lakini hadi leo mataluma na iliyojengwa miaka hiyo 110 iliyopita bado hadi leo yanatumika. Kwa sasa wakati mataluma ya mwaka 1914 yaani miaka 110 iliyopita yanayotumika hadi sasa yalikuwa ya chuma ambayo yana hatari ya kupata kutu, mataluma ya SGR ni ya zege, ambayo ni ya kudumu.
Tukikamilisha ujenzi Dar es Salaam – Morogoro – Kigoma – Tabroa – Dodoma au Tabora – Mwanza, reli hii itakuwapo vizazi na vizazi. Hii ina maana hata kama reli hii inakuwa imejengwa kwa mkopo, itatumiwa na wajukuu na vitukuu, hivyo ikitumika kusafirisha mizigo na abiria itakuwa na faida ya kudumu pia kwa taifa letu, hivyo Rais Samia anaikomboa nchi kwa miundombinu, kwani wapo watu waliodhani mradi huu ungesimama.
Katika ziara ya mwezi Mei, 2024 nchini Ufaransa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Kinara wa Nishati Safi ya Kupikia Afrika, aliziunganisha nchi na mashirika makubwa ya ufadhili kuchangia dola bilioni 2.2, ambazo mchango unaendelea kuelekea lengo la kukusanya dola bilioni 4 kila mwaka hadi mwaka 2030, fedha ambazo zitatumika kuziwezesha nchi za Afrika kuanza kutumia Nishati Safi na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.
Wema huanzia nyumbani, kwani katika fungu hilo nchi za Marekani, Uingereza na Ufaransa, zilitangaza miradi mahsusi kwa ajili ya Tanzania pekee na kwa Rais Samia kuwa Rais mwanamke pekee Barani Afrika, mataifa makubwa yanaipa Tanzania kipaumbele katika kushiriki nafasi ya kuikomboa kiuchumi nao wawe sehemu ya historia. Kuna kila dalili kuwa Mpango Mkakati wa Nishati Safi uliozinduliwa, kufikia mwaka 2034 Watanzania wengi watakuwa wanatumia gesi, umeme na nishati nyingine tofauti na kuni na mkaa. Hiyo ndiyo njia ya nchi kuendelea sawa na zilipo nchi zilizoendelea.
Kama hiyo haitoshi, mwezi Juni 2024 Rais Samia amefanya ziara hapa nchini Korea, ambapo Serikali ya Korea Kusini kwanza inasaini mkataba wa mkopo wa riba nafuu wa dola bilioni 2.5 sawa na Sh trilioni 6.8, ambazo baada ya kupatikana Tanzania itazifanyia miradi mbalimbali ikiwamo kuijenga upya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) iwe ya kisasa, yenye uwezo wa kuchukua wagonjwa wengi na iwe na wataalam na vifaa tiba vyenye uwezo wa hali ya juu.
Korea inataka kuiwezesha Tanzania si tu kupima ardhi ya taifa letu lote kusomeka kidigitali, bali pia kushirikiana na Tanzania katika kuchimba madini na kuyaendeleza. “Hatutaki kufanya makosa tuliyoyafanya kwenye dhahabu na almasi. Tunataka Wakorea tushirikiane nao kuwa na kampuni za kuchimba madini yetu, lakini katika mnyororo wa thamani kazi nyingi zifanyike Tanzania, watu wetu wapate ajira na huku yaletwe madini kama bidhaa zinazouzwa sokoni,” ameniambia Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Togolani Edriss Mavura.
Ukijumulisha dola bilioni 6.4 za Uturuki, ukaongeza angalau dola milioni 500 zitakazotokana na Nishati Safi ya Kupikia za Ufaransa kati ya hizo dola bilioni 2.2 zilizochangwa, ukaweka dola bilioni 2.5 za Korea Kusini, ni wazi katika ziara tatu tu za Rais Samia nje ya nchi katika nchi tatu na katika miezi mitatu, zimeiingizia Tanzania dola za Marekani bilioni 9.4 sawa na Sh trilioni 25.38. Fedha hizi zitajenga miradi ya kudumu kizazi hadi kizadi ikiwamo reli ya kisasa SGR. Ziara za Rais Samia nje ya nchi ni wazi zina faida kubwa kwa taifa.
Sitanii, nimejifunza na kushuhudia hatua kwa hatua nchi hizi zilivyowekeza na kuzalisha uchumi mkubwa, na bila kuuma maneno nasema njia pekee ya nchi yetu kukua kiuchumi ni uwekezaji katika viwanda na miundombinu, suala linaloona mwanga kupitia ziara za Rais Samia. Nimesema hapo juu, China na Korea ilizishika mkono Marekani, ni wazi Marekani kwa kushirikiana na Uturuki, Korea na China zimeonyesha hamu ya kuisaidia Tanzania kujinasua, hivyo uamuzi ni wetu kusuka au kunyoa.
Kwa Tanzania soko la bidhaa si tatizo, kwani ni nchi yenye bahati ya kuwa katika eneo la kijiographia ambalo kwa bahati mbaya sisi tuliozaliwa Tanzania hatujawahi kufahamu vyema faida ya eneo tulilochaguliwa na Mungu. Nchi yetu imezungukwa na nchi nane; Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Zambia, Malawi na Msumbiji.
Ziara ya Uturuki niliandika katika safu hii, kuwa inafungua mlango wa aina yake kwani Serikali ya nchi hiyo ilitoa dola bilioni 6.5 karibu Sh trilioni 17.3 ambazo zinatumika kujenga reli ya kati. Reli hii inakuwa haina kazi yoyote iwapo haina mzigo wa kusafirisha, lakini sasa Uturuki imekuja na ajenda ya kushirikiana na Afrika kupitia Tanzania. Kabla sijagusa eneo hili lenye manufaa makubwa kwa nchi yetu, nieleze kwa ufupi hadi sasa Korea imeisadia nini Tanzania.
Hadi sasa Korea imeisadia nini Tanzania?
Tanzania na Korea zilitiliana saini mkataba wa mikopo ya masharti nafuu Septemba 9, 2022 wa jumla ya dola za Marekani bilioni 1 sawa na Sh trilioni 2.3 kwa ajili ya kuekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hapo nchini.
Mkataba huo ulisainiwa jijini Dar es Salaam kati ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, sasa ni Gavana wa Benki Kuu, Emmanuel Tutuba na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa Korea nchini Tanzania, Kim Sun Pyo. Mkataba huo ni mkubwa kuliko yote iliyokuwa imetolewa awali na Serikali ya Korea kwa Tanzania. Kabla ya mkopo huo, Serikali ya Korea kati ya mwaka 2014 – 2020 waliikopesha Tanzania jumla ya dola milioni 733 karibu Sh trilioni 2.
Watanzania inawezekana hawafahamu fedha hizi zilitumika kufanya nini, ila kupitia ziara hii ya Rais Samia hapa nchini Korea nami nimepata fursa ya kufahamu kuwa fedha hizi ndizo zilizotumika kujenga daraja la Kikwete-Malagarasi huko Kigoma lililokuwa limeshindikana tangu enzi. Wengi wetu hawajui, lakini kumbe Wakorea kwa fedha hizo ndiyo waliojenga Hospitali ya Mloganzila, Dar es Salaam.
Daraja la Tanzanite ambalo lina sura ya aina yake pale jijini Dar es Salaam nalo limejengwa kwa sehemu ya fedha hizo. Kituo cha Data cha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Njia ya Kusafirisha Umeme kutoka Shinyanga kwenda Kigoma (ikumbukwe Kigoma haikuwa imeunganishwa kwenye gridi ya taifa, hivyo ni Wakorea walioliwezesha hili) na miundombinu ya Umwagiliaji Zanzibar vyote vimejengwa kutokana na fedha hizo.
Mkopo mpya wa dola bilioni 1, huo sasa ulitumika kuanzisha mradi wa Ardhi ya Kidigitali hapo nchini, ambapo wakati William Lukuvi akiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutumia fedha hizi ndipo alianzisha mpango na hati za ardhi za kidigitali. Hati za kumiliki ardhi nchini kwa sasa zinapatikana kwa urahisi kuliko wakati wowote katika historia ya nchi hii. Chini ya mpango huu, ardhi yote ya Tanzania inapimwa kwa satelaiti, ambapo kila kipande cha ardhi kitafahamika umiliki wake na kumaliza kabisa migogoro ya ardhi nchini. Hati za kidigitali tayari zimeanza kutolewa.
Mtakumbuka kuwa kipindi cha nyuma watu wengi ilikuwa wanajiandikisha kupata vitambulisho vya NIDA inakuwa vigumu kupata hata namba tu za vitambulisho na ilifika mahala ikaonekana kama NIDA wameshindwa kutoa vitambulisho, ila kwa sasa tatizo hili limekwisha na kila mwananchi anatumiwa meseji akitakiwa kwenda kuchunua kitambulisho chake. Kwa sasa Serikali inawatafuta wananchi wakachukue vitambulisho vyao, badala ya watu kushinda ofisi za NIDA wakiambiwa mitambo haifanyi kazi. Serikali ya Korea ndiyo imewezesha ufanisi tunaouona NIDA sasa kupitia mkopo huo ilioutoa.
Sitanii, mkopo huo ambao ni matunda ya safari za nje za Rais Samia umetumika kujenga mradi wa maji safi na maji taka Iringa, ujenzi wa chuo cha reli ya kisasa (SGR) katika eneo la Malabi lenye ukubwa wa ekari 183.1, kwenye Manispaa ya Tabora. Chuo hiki kinatarajiwa kuhudumia nchi za Tanzania, Zambia, Rwanda, Burundi na baadhi kutoka Uganda. Ujenzi tayari unaendelea. Pia zimetumika kujegna hospitali Binguni, jijini Zanzibar. Hospitali hii mpya yenye uwezo wa vitanda 600 itakuwa na ubora sawa na hospitali ya Mlonganzila. Hao ni Wakorea!
Korea ni nchi ya aina gani?
Korea Kusini ni nchi iliyoanzishwa rasmi Agosti 15, 1948, ikifuatiwa na kuanzishwa kwa Korea ya Kaskazini Septemba 9, 1948. Nchi hizi zilianzishwa kutokana na misuguano ya kisiasa, ambapo Marekani ilikuwa mshirika wa Korea Kusini na Urusi ilikuwa mshirika wa Korea Kaskazini. Kaskazini walichagua mkondo wa Ujamaa na kutaifisha ardhi kutoka kwa wamiliki, Kusini waliegemea mkondo wa Ubepari, japo nao waliigawa upya ardhi yao kutoka mikononi mwa wachache.
Misuguano ya Kaskazini na Kusini ikikuzwa na mataifa makubwa; Urusi na Marekani, mwaka 1950 ilizaa vita kati ya Korea Kusini na Kaskazini. Vita hii inayokisiwa kuua watu zaidi ya zaidi ya milioni 2.5 , iliisha Julai 27, 1953. Serikali ya Korea Kusini chini ya Rais Syngman Rhee (wakati huo), ilirejea jijini Seoul, ambako ilipafanya makao makuu ya Serikali ya nchi hii. Nchi hizi mbili Korea Kusini na Korea Kaskazini, zilitambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa na kuwa wanachama, mwaka 1991. Tanzania ilianzisha uhusiano na Korea Kusini, mwaka 1992.
Mwaka 1960 yalitokea Mapinduzi ya wanafunzi yaliyomkimbiza uhamishoni Rais Rhee. Machafuko yaliendelea hadi mwaka 1963 Rais Park Chung Hee alipoingia madarakani. Park aliiongoza Korea Kusini hadi mwaka 1979. Katika uongozi wake, alifanya mapinduzi makubwa ya kiuchumi. Alizichagua familia 15, akazipatia mtaji kufanya biashara na uwekezaji katika viwanda na teknolojia.
Familia hizi zinazofahamika kama Chaebol zimewekeza katika kila kitu unachofikiria, kuanzia kilimo, ufugaji, viwanda, teknolojia, sayansi, elimu na kila unachokiwaza ambazo katika uchumi wa Korea Kusini wa USD trilioni 1.67 (Sh trilion 4,519), familia za Chaebol zinamiliki asilimia 80 sawa na dola trilioni 1.339 (Sh trilioni 3,615). Wakorea Kusini milioni 52 waliobaki wanamiliki asilimia 20 ya uchumi wa taifa lao uliosalia. Eneo hili nitaliandikia makala inayojitegemea.
Korea Kusini ni nchi ya 5 kwa mauzo ya nje duniani, ni ya 8 kwa kununua kutoka nje (import), 5 kwa nguvu ya bahari, 2 kwa ujenzi wa meli, 6 kwa sekta ya anga, uzalishaji wa magari ni nchi 3 ikitanguliwa na Wolkswagen (Ujerumani), Toyota (Japan) na Hyundai yao ni ya tatu. Nchi hii ipo katika uzalishaji wa betri za magari ya umeme (EV). Miaka ya 1960 pato la mtu mmoja mmoja lilikuwa chini ya dola 75 kwa mwaka, lakini leo mwaka 2024 ni dola 33,700 kwa mwaka.
Kutokana na huduma bora, umri wa mtu kuishi hapa Korea Kusini ni miaka 86. Nchi hii ina upungufu wa watoto. Wastani wa umri wa watu wake ni miaka 44, ambapo sisi hapo kwetu ni 18 (wastani wa umri). Korea Kusini ina watu milioni 51, wanaokaa kwenye eneo la mraba kilomita 100,000 sawa na ukubwa wa mikoa ya Tabora na Geita. Theluthi mbili ya ardhi ya nchi hii ni milima, hivyo watu wanaishi katika theluthi moja iliyosalia.
Nchi hii haina madini wala mafuta, ila imewekeza katika rasilimali watu na inategemea jiografia yake. Miaka ya 1950 Benki ya Dunia ilikataa kuikopesha kwa kusema haina uchumi imara, lakini leo nchi hii ndiye mfadhili mkubwa wa Benki ya Dunia. Kwa ufupi, hiyo ndiyo nchi iliyoamua kushirikiana na Tanzania. Kampuni za Hyundai, LG, Samsung na nyingine 12 ndizo zinashikilia uchumi wa taifa hili. Nitaandika makala inayojitegemea. Je, Watanzania tutarajie kupata kutokana na ushirikiano huu?
Kwa nini Tanzania na tutapata nini?
Kuna habari njema. Kuanzia mwakani Kampuni ya Hyundai inaanza kuzalisha magari kwa njia ya kuunganisha (assembling ikiwa hapo Tanzania). Mwaka 2019 Korea Kusini ilipata changamoto ya kupata rasilimali za kuendesha viwanda vyake kutokana na ukweli kwamba ilikuwa inaagiza asilimia 80 ya rasilimali za viwanda vyake kutoka China.
Baada ya janga la Covid 19, China ilifunga uchumi wake kwa miaka minne bila kufanya kazi. Hii iliwafanya uchumi wao pia kudorora kwani hawakuwa wakifanya biashara ya malighafi kwa ajili ya viwanda vyao na nchi nyingi ikiwamo nchi za Afrika. Hadi sasa Korea Kusini inafanya biashara na nchi za Afrika kwa kiwango cha chini ya asilimia 1 ya biashara zote inazofanya kwa mwaka.
Sitanii, Korea Kusini imebaini sasa kuwa Afrika ina rasilimali kama madini na chuma ambazo imekuwa ikinunua kutoka China, ambapo China inanunua kwa wingi rasilimali hizo kutoka Afrika. Korea Kusini imezichekecha nchi 55 za Afrika ikachagua kushirikiana na nchi tatu tu, ambazo ni Tanzania, Kenya na Morocco.
Hadi sasa Tanzania ni nchi ya pili kwa kupata misaada kutoka Korea Kusini kwa Bara la Afrika. Tanzania imepata dola bilioni 1.3, ilihali nchi inayoongoza ni Misri ambayo imepata dola bilioni 1.6 kutoka Korea Kusini. Kupitia ziara hii Tanzania inakwenda kupata msaada wa kujenga Chuo cha Teknolojia ya Kidigitali. Chuo hiki mbali na lengo la kuzalisha simu na teknolojia nyingine, kitatumika kuendeleza wabunifu. Hospitali ya Taifa Muhimbili inajengwa upya kuwa maghorofa ya kwenda juu na tayari Korea imetoa dola milioni 230.
Sitanii, katika ziara hii, Tanzania itasaini mkataba wa mkopo wa dola bilioni 2.5 kutoka Korea Kusini. Nimesoma na kusikia maneno kupitia mitandao baadhi ya watu wakihoji mkopo huu. Taarifa nilizopata, mkopo huu utalipwa kwa miaka 40. Lakini tangu siku ya saini Tanzania itakaa miaka 25 bila kulipa, na itaanza kulipa katika mwaka wa 26, ambapo italipa kwa miaka 15 mfululizo kutimiza hiyo miaka 40. Kizuri kuliko yote, riba ya mkopo huu ni asilimia 0.01. Kwa lugha nyingine ni sawa kama vile mkopo huu hauna riba. Kumbuka Reli ya Kati ina miaka 110 sasa, mkopo huu ukitumika katika miradi ya maendeleo, faida yake ni ya kudumu.
Eneo jingine ambalo Tanzania itanufaika, yanasainiwa makubaliano (MoU) ya Ushirikiano kwenye madini ya kimkakati. Tanzania tunataka kushirikiana na Korea, kupima ardhi yote. Hadi sasa tunafahamu asilimia 16 ya aina ya madini tuliyonayo Tanzania. Tutashirikiana kupima. Wao wanataka madini mengi ikiwamo Lithium, Nikel, Graphite na mengine kwa ajili ya kutengeneza betri za umeme wa magari. Ni katika hili Balozi Togolani amesema Tanzania haitafanya tena makosa yaliyofanyika katika dhahabu na almasi.
Eneo la tatu yanasainiwa makubaliano katika eneo la uchumi wa bluu. Kuna samaki wengi, wakiwamo jodari ambao tani moja inatajwa kuuzwa kwa dola milioni 50. Samaki hawa wanatembea, tusipowavuna wanakwenda India, Mauritius na wanarejea kwetu wanapita. Korea Kusini wenye ujuzi mkubwa katika masuala ya uvuvi, sasa wanataka kushirikiana na Tanzania kuvuna mazao ya bahari. Hii itatimiza ndoto ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi ya kuona Uchumi wa Buluu unakua.
Katika mkutano huu wa wakuu wa nchi za Afrika na Korea, Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Korea, itatoa tamko la kuanza ushirikiano wa kiuchumi na Tanzania. Tamko hili sasa litaanzisha mazungumzo ya ushirikiano na maeneo ya ushirikiano. Kama Korea na China ilivyopata Marekani ikawashika mkono wakatoka kiuchumi, ni wazi Korea, Marekani na China zimeamua kuishika mkono Tanzania kupitia safari za Rais Samia.
Najua kuna msemo wa Kiswahili kuwa “Nabii hathaminiwi kwao.” Wakorea wametambua mchango wa Rais Samia katika kulifufua Shirika la Ndege la Air Tanzania na kumtunukia shahada ya udaktari wa falsafa wa heshima (PhD), ila hapo kwetu baadhi wana macho lakini hawaoni. Haina ubishi kuwa Watanzania tukiamua kuzichukua nafasi hizi, tunaufuta umaskini. Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania.
0784404827