*Atangaza ‘Baraza Kivuli la Mawaziri’ nje ya Bunge

Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo na mwanasiasa maarufu nchini, Zitto Kabwe, amesema wananchi wanahitaji kupata hoja mbadala.

Akizungumza na wahariri na wanachama wa Jukwaa la Wahariri (TEF) jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kutangaza wasemaji wa kisekta wa chama hicho, Zitto amesema ni muhimu kwa changamoto zinazowakabili wananchi kupatiwa ufumbuzi mara moja.

“Sote tunafahamu uchaguzi uliopita (2020) ulivyokuwa. Hatuna sauti ya kutosha ndani ya Bunge, hivyo hakuna hoja mbadala.

“Kwa hiyo ACT Wazalendo tumejipanga kuziba hilo ombwe lililopo. Kuanzia sasa wasemaji wetu wa kisekta, ambao mtawaona hapa pamoja na wasifu wao, watakuwa wakitoa hoja mbadala kwa serikali,” amesema Zitto.

Akijibu swali iwapo hoja zitakazotolewa na ACT Wazalendo zitafanyiwa kazi na serikali au la, Zitto amesema:

“Zipo hoja nyingi zilizowahi kutolewa na upinzani ambazo zimefanyiwa kazi na serikali. Nyingi tu hata kama si nyingi sana. Hata kama hazifanyiwi kazi mara moja, utakuta zinaingizwa baadaye kwenye mipango yao.”

Kuhusu wasemaji hao wa kisekta ambao ni sawa na Baraza Kivuli la Mawaziri, Zitto amesema limepangwa kwa kuzingatia jinsia.

“Lakini pia ni jukumu letu kuwalea na kuwakuza vijana ili waje kuwa wanasiasa wazuri hapo baadaye kama sisi tulivyolelewa, na hapa utaona kuwa tumewaweka vijana wengi kuwa manaibu wasemaji wa kisekta,” amesema mbunge huyo wa zamani wa Kigoma.

Amesema miongoni mwa maofisa 24 wa kisekta, 12 ni wanawake na 12 ni wanaume, ambapo Msemaji Ofisi ya Waziri Mkuu ni Dorothy Semu.

Kimuundo Dorothy ndiye atakayekuwa mtendaji mkuu wa shughuli zote zitakazofanywa na Baraza Kivuli nje ya Bunge.

Miongoni mwa majukumu yake ni kuisimamia serikali kutekeleza wajibu wake.

Maofisa wengine wanaounda Baraza Kivuli la Mawaziri wa ACT Wazalendo ni Abdul Nondo (Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu na Msemaji Mkuu wa Baraza Kivuli), Emmanuel Mvula (Fedha na Uchumi), Fatma Fereji (Mambo ya Nje), Masoud Salim (Ulinzi) na Mbarala Maharagande (Mambo ya Ndani).

Wengine ni Riziki Mngwali (Elimu), Dk. Nasra Omar (Afya), Mwanaisha Mndeme (Uwekezaji, Mashirika ya Umma na Hifadhi ya Jamii), Pavu Abdallah (Utumishi wa Umma, Utawala Bora na Muungano) na Kulthum Mchuchuli (Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Maendeleo Vijijini).

Zitto amewataja maofisa wengine  kuwa ni Isihaka Mchinjita (Nishati), Edgar Mkosamali (Madini), Halima Nabalang’anya (Viwanda na Maendeleo ya Biashara), Esther Thomas (Maji na Mazingira), Wakili Victor Kweka (Katiba na Sheria), Mtutura Mtutura (Kilimo, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi), Bonifasia Mapunda (Ardhi na Maendeleo ya Makazi), Mhandisi Mohammed Mtambo (Miundombinu ya Ujenzi, Barabara na Reli) na  Ally Saleh (Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Uchukuzi).

Katika baraza hilo pia wapo Juliana Makan’gwali (Maliasili na Utalii), Wakazi Wasira (Utamaduni, Sanaa, Ubunifu na Michezo), Mwalimu Macheyeki (Vijana, Kazi na Ajira) na Janeth Rithe (Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto).

Manaibu wasemaji ni Petro Ndolezi (Maji), Juma Kombo (Fedha), Julius Masabo (Biashara), Dahlia Majid (Nje), Said Bakema (Ulinzi), Bahati Chirwa (Elimu), Fidel Hemed (Ujenzi) na Japhet Masawe atakayekuwa msemaji katika masuala ya Mawasiliano.

Wengine ni Antony Ishika (Utalii), Vitale Maembe (Sanaa), Khadija Anwar (Ndani), John Kivuyo (Utumishi), Ruqqaya Nassir (Madini), Christina Makundi (Sheria) na Selemani Misango (Kilimo).

Akizungumza kwa niaba ya wahariri, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, ameahidi kufanya kazi ni ACT Wazalendo katika kuchagiza maendeleo ya taifa.

“Nisisitize tu kwamba wahariri wapo tayari kushirikiana nanyi pamoja na taasisi zote. Tunachotaka ni hoja za maana, si matusi,” amesema.

By Jamhuri