DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amempongeza mmiliki wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Rostam Aziz, baada ya kulipa mafao ya waliokuwa wafanyakazi wake.

Pongezi za Nape kwenda kwa mfanyabiashara Rostam zimetolewa mwishoni mwa wiki iliyopita kupitia taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha wizara hiyo, Prisca Ulomi. 

“Naupongeza uongozi na mmiliki wa Kampuni ya New Habari (2006) Limited kwa

kupeleka fedha za mafao katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa waliokuwa wafanyakazi wa kampuni hiyo baada ya kusimamisha uzalishaji Desemba, 2020,” amesema Nape.

Taarifa hiyo imesema pongezi hizo amezitoa baada ya mwakilishi wa New Habari (2006) Limited, African Lyakurwa, kukabidhi hundi zenye thamani ya Sh bilioni 2.9 kwa viongozi wa wafanyakazi wa kampuni hiyo wakiongozwa na Michael Budigila.

Pia imesema jana fedha hizo zilitarajiwa kuwekwa katika akaunti za mifuko ya hifadhi ya jamii.

Pamoja na pongezi hizo, pia Nape ametoa wito kwa wamiliki wote wa vyombo vya habari kuhakikisha wanazingatia sheria za kazi kwa kuwalipa mishahara waandishi wa habari kwa mujibu wa mikataba yao ya kazi na kupeleka michango yao katika mifuko ya hifadhi ya jamii.

“Nitumie fursa hii kumpongeza mmiliki wa Kampuni ya New Habari (2006) Limited kwa kutekeleza takwa la kisheria kwa kuwalipa waliokuwa wafanyakazi wake ambao wengi ni waandishi wa habari malimbikizo ya mishahara na kulipa malimbikizo ya michango katika mifuko ya hifadhi ya jamii,” amesema Nape.

Aidha, ameitaka mifuko hiyo kuhakikisha inafanyia kazi haraka suala la mafao ya wafanyakazi hao kila mmoja apate haki yake kwa mujibu wa sheria na kwamba serikali itaendelea kusimamia masilahi ya wanahabari.

By Jamhuri