Zoezi la utayari katika afya EAC lipewe uzito

Mwezi ujao, kwa muda wa siku nne, kuanzia tarehe 11 hadi 14, Tanzania itashiriki zoezi la kupima utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani.

Hali hiyo inatokana na nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki kuwa katika hatari ya kuathirika na magonjwa ya mlipuko kama Homa ya Bonde la Ufa, Mafua Makali ya Ndege na Ebola.

Zoezi hilo litazingatia dhana ya afya moja ambayo hujumuisha sekta ya afya ya binadamu, wanyamapori, mifugo na mazingira katika kujiandaa, kufuatilia  na kukabili magonjwa yanayoathiri binadamu.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, zoezi  hilo linalenga kufanyia majaribio ya utekelezaji wa mipango ya dharura ya taifa na kanda, miongozo ya utendaji na kuwapa washiriki fursa ya kujifunza namna sekta zingine zinavyotekeleza majukumu katika kuzuia na kupunguza madhara pamoja na kujiandaa kukabiliana na maafa ya magonjwa ya mlipuko.

Maelezo zaidi ya wizara hiyo ni kwamba zoezi litaandaliwa kwa kuhusisha mlipuko wa virusi vinavyoshabihiana na Homa ya Bonde la Ufa katika eneo la mpakani, na washiriki watahitajika kuonyesha utayari wa kukabiliana na ugonjwa huo kwa kuzingatia mfumo wa afya moja. Eneo husika la shughuli hiyo ni mpaka wa Namanga, kati ya Tanzania na Kenya.

Ni zoezi ambalo msingi wake ni matokeo ya kikao cha 11 cha kawaida cha mawaziri wa sekta ya afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichofanyika Machi, 2015, kikao kilichoelekeza Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuandaa zoezi la nadharia la kukabiliana na magonjwa ya mlipuko katika mpaka wa Tanzania na Kenya, eneo la Namanga.

Ni matarajio yetu kuwa zoezi hili litakuwa lenye manufaa kwa mataifa husika kama inavyotarajiwa, na kwa maana hiyo, tunawatakia kila la heri wote watakaoshiriki zoezi husika.