Wiki iliyopita Gazeti hili la JAMHURI lilichapisha habari kuhusu kashfa iliyojitokeza wakati wa maadhimisho ya kilele cha Siku ya Wafanyakazi, Mei Mosi, kwa mwaka huu yaliyofanyika kitaifa jijini Mbeya.

Kashfa hiyo imekikumba Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (TRAWU). Ndani ya chama hicho, baadhi ya viongozi wake wanadaiwa kuwasilisha jina la kigogo asiyestahili kuwa mfanyakazi bora ili apewe mkono na Rais Dk. John Magufuli, kukabidhiwa cheti cha mfanyakazi bora pamoja na zawadi ya hundi.

Katika habari hiyo imeelezwa kuwa baadhi ya viongozi wa TRAWU walisababisha Rais Dk. John Magufuli kumpa zawadi ya mfanyakazi bora mtu asiyestahili. Kwamba aliyestahili zawadi hiyo ni James Kunena na si Focus Sahani kama ilivyofanyika. Leo gazeti hili limeendeleza habari hiyo kwa kuonyesha namna wafanyakazi wasivyoridhishwa na baadhi ya viongozi wa TRAWU kiasi cha kuwasilisha malalamiko yao kwa Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri.

JAMHURI tunaamini kuwa suala hilo linaweza kupata ufumbuzi kwa kuwasikiliza wafanyakazi wa ngazi za chini wanaolalamika mwenzao kutokupewa heshima aliyostahili ya kuwa mfanyakazi bora kwa mwaka huu wa 2019.

Badala ya kuhangaika huku na kule wakati uhalisia ukiwa wazi mbele ya umma, viongozi wa TRAWU wajitokeze hadharani kuomba radhi kwa tukio lao la kusababisha Rais Dk. Magufuli akutanishwe na mtu ambaye si mfanyakazi bora kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC).

Sifa zilizotumika kumpa ushindi wa mfanyakazi bora mhusika ni pamoja na ubunifu wake wa kutengeneza vipuri ambavyo kama si ubunifu huo, ilibidi viagizwe kutoka nje ya nchi. Na kwamba, ubunifu wake huo umesababisha idadi ya mabehewa kwa TRC kuongezekana hadi kufikia mabehewa 80. Hili si jambo dogo, ndiyo maana JAMHURI tunapigania mhusika apate haki yake na wale waliogeuza ushindi wake kwa kusoma jina lisilostahili mbele ya rais wawajibike kwa kuwaomba radhi wafanyakazi wa TRC na umma wa Watanzania kwa ujumla, lakini pia kuahidi kwamba makosa ya aina hiyo hayatatokea tena mbele ya macho yao.

Please follow and like us:
Pin Share