Moja ya habari zilizochapishwa na gazeti hili ni kuhusu kupotea katika mazingira ya kutatanisha kwa mtuhumiwa wa uhalifu, Josephat Jerome Hans, akiwa mikononi mwa Jeshi la Polisi mkoani Dodoma.

Habari hiyo imeeleza kuwa kijana huyo anatuhumiwa kwa wizi wa Laptop katika moja ya nyumba za kulala wageni Dodoma.

Tayari mama mzazi wa mtuhumiwa huyo, Lusina Joseph Kiria, ameandika malalamiko yake kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi mwezi Machi, mwaka huu, akielezea tukio hilo, akitaka mwanaye ambaye anadhani amekwisha kufariki dunia apatikane.

Kijana huyo, habari inaeleza alikamatwa Machi 4, mwaka huu, saa tano usiku eneo la Majengo na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi.

Mama wa mtuhumiwa huyo anadai kuwa kabla ya mtoto wake kutoweka akiwa mikononi mwa polisi, dada wa mtuhumiwa huyo aliyetajwa kwa jina la Adelina Hans aliwaomba polisi wampe dhamana ndugu yake huyo lakini polisi hao waligoma.

Katika barua yake anadai kuwa polisi walimweleza hawawezi kumpa dhamana kwa kuwa kosa lake ni kubwa na kama ni dhamana ataipata mahakamani.

Ananukuliwa akisema:  “Tulipompelekea chai hiyo tarehe 5, mwezi Machi alitumia muda mrefu akitembea kwa kujishikiza ukutani hadi kuja kuchukua chai, kwa sababu alikuwa hawezi kutembea vizuri, polisi walimpiga sana na hakupatiwa matibabu yoyote.”

Kwa kuzingatia tukio hili, JAMHURI tunasisitiza haki itendeke. Nafasi yetu katika hili si kutetea uhalifu au mhalifu bali kuhakikisha haki inatendeka kwa mujibu wa sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila kujali haki hiyo inapaswa kumnufaisha nani au upande gani kati ya ule unaotuhumiwa au kutuhumu.

Kosa la wizi wa aina hiyo bila shaka linastahili dhamana, kwa hiyo Jeshi la Polisi lilistahili kumpa dhamana mhusika. Dhamana ni haki ambayo imepata kuzungumzwa hata na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wa sasa, Kangi Lugola, aliyetaka Jeshi la Polisi kuheshimu haki ya dhamana kwa watuhumiwa wanaostahili kupewa haki hiyo.

Lakini ukiondoa hilo la mtuhumiwa huyo kunyimwa dhamana, kuna suala la kutoweka kwake. Ingawa madai hayo kwamba mtuhumiwa huyo ametoroka yanaendelea kuchunguzwa, ni matumaini yetu sisi JAMHURI kwamba uchunguzi huo hautachukua muda mrefu ili ikibidi mhusika ama afikishwe mahakamani au aachiwe huru. Tunatambua kuwa haki iliyocheleweshwa ni sawa na haki iliyopokwa.

Please follow and like us:
Pin Share