Mei Mosi mwaka huu wafanyakazi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaungana na wafanyakazi wenzao kwingine duniani kuadhimisha siku ya wafanyakazi.

Kwa kawaida mataifa karibu yote duniani huadhimisha siku hii kwa namna tofauti, lakini yenye baadhi ya matukio yanayoshabihiana kama maandamano ya makundi ya wafanyakazi wa sekta tofauti wakiwa na mabango yenye ujumbe wanaoulenga kwa sababu mahususi kwa mujibu wa mtazamo wao.

Lakini mbali na maandamano, katika mataifa mengi duniani siku hii huwa ni siku ya mapumziko ya kitaifa. Hapa Tanzania kila mwaka wafanyakazi wamekuwa wakiadhimisha siku hii muhimu kwao na kwa taifa kwa ujumla, na kwa umuhimu wake, serikali huitambua siku hii kuwa ya mapumziko ya kitaifa ili kuwapa nafasi wafanyakazi kuiadhimisha.

Mwaka huu kama ilivyo ada, wafanyakazi wanajumuika tena kuiadhimisha siku hiyo. Hata hivyo, pengine mwaka huu mazingira ya kuadhimisha siku hiyo yamekuwa na sura ya kipekee. Kwa mfano, mbali na kuwapo kwa matarajio au kiu ya kutaka kutangazwa kwa viwango vipya vya mishahara, wafanyakazi wanaadhimisha siku hii katika mazingira yanayoshuhudia kuwapo kwa mvutano kati ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.

Kwa ujumla, kazi ya CAG ni muhimu katika tasnia ya utawala bora na pale kwenye utawala bora wenye viwango maana yake ni kwamba wafanyakazi watakuwa katika matumaini makubwa ya kunufaika kwa kadiri ya jasho lao.

Kwa hiyo tafakuri zaidi inahitajika katika maadhimisho ya mwaka huu ya Mei Mosi, kwamba, fedha zinazotumika katika shughuli mbalimbali za kitaifa ambazo hukaguliwa na CAG kwa sehemu fulani ni makato ya kodi kutoka katika kipato cha wafanyakazi nchini. Sasa, kama fedha hizo zinazokaguliwa na CAG ni sehemu ya jasho la wafanyakazi, je, wafanyakazi wanatoa ushirikiano kwa kiwango gani katika kufanikisha kazi za CAG kwa niaba ya wananchi kwa ujumla?  

Wafanyakazi nchini watambue kuwa pamoja na haki yao ya kudai masilahi bora zaidi kwa mujibu wa jasho wanalovuja lakini matumizi ya kile wanachochangia kwa mfumo wa kodi kwa ajili ya kufanikisha miradi mbalimbali ya kitaifa au matumizi mengine nyeti ya taifa hili yanapaswa kukaguliwa, na mwenye jukumu hilo ni CAG, hivyo basi, watambue na kuzipa nafasi ya kutosha kazi za watu aina ya CAG wanaotimiza majukumu yao kwa mujibu wa Katiba ya nchi. Mchango wa CAG Mei Mosi hii utambuliwe.

Please follow and like us:
Pin Share