Katika mazingira ya siasa tunayoshuhudia sasa, upo uwezekano kuwa hatuelekei kuzuri. Hata bila kutafuta wapiga ramli kutabiri yakakayojiri baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba tafakari ndogo inaashiria uwezekano wa kuvunjika kwa amani.

Matamshi ya wahasimu wakubwa wa kisiasa, ikiwa ni pamoja na viongozi wa vyama vikuu vya siasa pamoja na washabiki wao, yanatoa taswira kuwa tunaelekea kwenye mpambano ambao kila upande unaamini utaleta ushindi kwao.

Kuamini kupatikana kwa ushindi ni jambo moja. Jambo la pili na ambalo ni la msingi zaidi, ambalo linazua hofu kwa baadhi yetu, ni lipi litatokea iwapo upande mmoja ambao umetabiri ushindi kwao ukishindwa, na utachukua hatua gani pale ambapo Tume ya Uchaguzi itatangaza matokeo yaliyo tofauti na matarajio.

Wanasiasa wanawaambia mashabiki wao kuwa ushindi ni lazima. Kutamka lazima kama neno linaloamsha mori ya washabiki kuweka juhudi kubwa kwenye kutafuta ushindi ni mbinu inayotumika kwenye ushindani wowote.

Hakuna anayeingia kwenye ushindani wa aina yoyote akitamka hadharani kuwa anatarajia kushindwa bila msimamo huo kudhoofisha azma ya ushindi. Jemadari bora ni yule anayeingia vitani akiwaambia wapiganaji wake kuwa anategemea kushinda hata kama anafahamu anadanganya. Msimamo wa aina hii unajengea nguvu kubwa wapiganaji wake na kuongeza uwezekano wa kushinda. Naamini wapo wanasiasa wa pande zote zinazopingana wanafahamu fika kuwa ushindi ni ndoto lakini hatuwategemei kutangaza kushindwa. Tatizo ni wafuasi wanachukulia vipi matamshi hayo na kama watakuwa tayari kukubali matokeo ambayo ni tofauti na yale waliyotabiriwa na viongozi wao. Dini zote kubwa zinahubiri amani, ingawa wakati mwingine hutokea mazingira yanayosababisha viongozi wa dini kubadilisha msimamo wa amani na kuhimiza mapambano. 

Lakini mpaka sasa sijasikia kiongozi wa dini yoyote Tanzania kuhamasisha uvunjifu wa amani kama nyenzo ya kutetea msimamo wa kisiasa. Hata hivyo haihitaji kuwa muumini wa dini kuona madhara yanayoweza kujitokeza pale amani inapotoweka.

Anayetafakari vyema hahitaji kuambiwa mara kwa mara umuhimu wa kulinda amani. Lakini hiyo itakuwa sawa na kusema inatosha kuambiwa mara moja na viongozi wetu wa dini tuepuke maovu na tukabaki waumini wazuri maisha yetu yote bila kukumbushwa kila siku.

Mafundisho ya dini yapo kwa sababu hulka ya binadamu ni kusahau na anahitaji kukumbushwa kila wakati kuishi kwa uadilifu na kudumisha yaliyo mema kwa sababu vishawishi vya kufuata yaliyo maovu vipo machoni mwetu kila wakati. Na kwenye siasa za leo hali ni hivyo hivyo. Yapo mengi yanayosemwa ambayo yanaendelea kuwa chachu au vishawishi vinavyotufanya tusahau kuwa upo umuhimu mkubwa wa kulinda amani. Tujikumbushe mauaji ya kimbari yaliyotokea Rwanda, na matukio yanayoendelea kwenye baadhi ya nchi jirani kama Somalia, na maeneo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Mambo yakiharibika tunaweza kukaa miaka nenda rudi tukibishania chanzo cha kuvunjika kwa amani na nani alaumiwe lakini haitazuwia watu kuathirika. Na makundi yanayoathirika zaidi huwa ni wanawake, watoto, na wazee.

Malumbano ya kisiasa yanaweza kuibua mapigano kati ya makundi ya pande mbili au zaidi zinazounga mkono msimamo wa kisiasa.  Lakini siyo kweli kuwa kila njiti ya kibiriti inayowashwa lazima iibue moto wenye madhara, au hata kuibua moto. 

Tatizo lililopo ni kuwa raia wanaweza kuwa wameishi kwa muda mrefu na kero ambazo zilikuwa zinafukuta miongoni mwao na zilikuwa zinasubiri kuwashwa kwa njiti moja tu ili kulipua hasira zao na kuwafanya waachane na amani. Wanaopanda kwenye majukwaa ya siasa wanatembea na vibiriti vilivyojaa hata kama wenyewe hawaoni hivyo.

Kuna mengi ambayo yanapaswa kufanyika ili kuleta amani ya kweli ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira yanayomfanya kila raia aamini kuwa anaishi kwenye nchi yenye uongozi ambao, kwa dhati, unajali masilahi yake. Raia aliyeamka na njaa hana motisha yoyote ya kulinda amani ya nchi, wacha ya jirani zake. Raia ambaye amechoka kutoa rushwa ili apate huduma za kijamii ambazo amezilipia kodi hawezi kulinda amani.

Yapo matatizo mengi ambayo yapo sasa na yatakuwepo siku, miezi, na miaka baada ya kupiga kura. Ndiyo maana ni muhimu kukumbushana kuwa yapo maisha baada ya uchaguzi. Lakini kutokana na uwezo mkubwa wa kupazwa kwa sauti za vyama vya siasa, zipo sauti ambazo hazisikilizwi sana sasa hivi zinazohubiri kuwa yapo maisha yatakayoendelea baada ya uchaguzi.

Maana rahisi ya kusema yapo maisha baada ya uchaguzi ni kusema kuwa watakaoshinda watashinda, watakaoshindwa watashindwa, na jirani yako yule yule ambaye ulikuwa unashikana naye mashati ukitetea chama chako atabaki kuwa jirani yako. Rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano ataapishwa na wote tutarudi kutafakari tuweke juhudi gani za msingi za kuendeleza maisha yetu na maisha ya familia zetu. Ahadi za siasa tunazopewa sasa zitakuwa majaliwa ya Mwenyezi Mungu au, kwa wale wasioamini kuwepo kwa Muumba, itakuwa ni suala la bahati nasibu.

Tume ya Uchaguzi inayo wajibu wa kusimamia vyema mchakato wa uchaguzi kuhakikisha kuwa malalamiko yatakayojitokeza hayawi sababu ya msingi kwa upande wowote kulalamika kuwa umepokonywa ushindi. Lakini mazingira yaliyopo sasa hivi yanadhoofisha uwezo wa Tume kufanya kazi hiyo kwa ufanisi. Siku hizi kila tukiamka tunapewa matokeo ya kura za maoni yanayotabiri ushindi kwa mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na siku chache zinazofuata tunapata matokeo mengine ya kura za maoni yanayotabiri ushindi kwa mgombea wa vyama vinavyoudwa na UKAWA.  Haiwezekani kuwa matokeo haya yanayokinzana yakawa yote ni sahihi. Bila kunyoosheana vidole inatosha kusema kuwa kuna upande ambao umekubali matokeo yenye mchakato ambao haukuzingatia misingi sahihi ya kuendesha kura za maoni. Lakini ingawa imani siyo ukweli, haitakuwa kosa kuamini kuwa baadhi ya matokeo haya yamepikwa. Muhimu kusisitiza hili: imani siyo lazima kuwa ndiyo ukweli.

Lakini ni imani, ya ukweli au ya kupikwa, ambayo wapiga kura wengi wataibeba kwenda nayo kwenye vituo vya kupiga kura tarehe 25 Oktoba. Muujiza ambao hautatokea kati ya sasa na siku ya kupiga kura ni kubadilisha imani ya mpiga kura kuwa tafiti za chama chake ni za kupika na zimewekwa viungo vya kila aina. Kwa hiyo tukubali kuwa mazingira imara ya kutokubaliana tayari yapo.

Na maisha baada ya uchaguzi yapo pia. Hatujui kwa uhakika kama yatakuwa ya amani.

By Jamhuri