Barua yangu kwa Profesa Ndalichako

wanafunziAwali ya yote naipongeza Serikali kwa hatua chanya iliyoichukua ya kutoa elimu bure kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha nne.

Ni hatua ya kupongezwa na kila mpenda maendeleo wa nchi yetu. Lakini, hatua ya kutoa elimu bora kwa kila Mtanzania bado ni ndefu ambayo inahitaji mchango wa hali na mali kwa kila Mtanzania. Kutokana na ukweli huu juu, ninayo mapendekezo kwako Mheshimiwa ya namna ya kufikia azma hiyo.

Hata hivyo, kabla ya kutoa mapendekezo hayo, ninatao maelezo ya awali yafutayo:

Kwa mwanadamu kupata elimu ni Amri ya Mungu Mwenyezi kwa kiumbe wake kama vitabu vitakatifu vinavyotufundisha. Tukianza na Biblia Takatifu, inatufundisha: “Mkamate elimu wala usimwache aende zake, mshike maana yeye ni uzima wako (Mith: 4:13, Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa (Hosea: 4:4-7).”

Kwa upande wake, Koran Tukufu inatufundisha: “Tafuteni elimu hata Uchina -Mtume Mohamad (SAW).”  Mtume alitumia Uchina akisisitiza umuhimu wa elimu na kutumia Nchi   ya Uchina kwani ni umbali wa nchi. Bahati mbaya agizo hili la Mwenyezi Mungu, kwa kila kiumbe wake kupata elimu bora limekiukwa na  binadamu huyo huyo kiumbe wake na  sasa imekuwa ni biashara. Ni vyema kutii sauti ya Mungu kama alivyoagiza.

Kama nilivyosema hapo juu, kinyume cha agizo la Mungu, hivi sasa elimu ni biashara ambako ukiwa nayo unapata elimu nzuri kulingana na uwezo wako kama hauna unakosa kwa msemo wa kisasa wanasema; “Inakula kwako”.

Hii ni tofauti na enzi za Serikali ya Awamu ya Kwanza ambako wananchi bila kujali uwezo wao waligawana kilichopo kwa kuwapeleka watoto wote kwenye shule za aina moja ambako zote zilitoa viwango bora vya elimu.

Hivi sasa kuna kinachoitwa eti “shule bora” ambazo zote  ni shule binafsi na za taasisi za dini ambazo wanaosoma hapo ni watoto  wa Watazania wa wenye  uwezo kifedha, hasa wafanyakazi serikalini, mashirika ya umma na wafanyabiashara. Kwenye shule hizi zinzoitwa “shule bora” ada kwa mwaka ni kubwa mno  kama ifutavyo:

Chekechea: Sh 900,000 – Sh 1,000,000.

Darasa la kwanza hadi la saba: Sh 1,00,000- Sh 1,500,00.

Sekondari: Kidato I-IV: Sh 2,000,000 – Sh 3,000,000.

Sekondari kidato V-VI: Sh 3,500,000-Sh 5,000,000.

ChuoKikuu: Sh 6,000,000-Sh 10,000,000.

Kwa wale ambao hupeleka watoto wao nchi za nje, ada hufika hadi Sh milioni 20 au zaidi.

Hizi ada ni kubwa mno, kiasi kwamba inapofika wakati wa kulipa ada, ni maumivu kwa wazazi na walezi.  Kwa bahati mbaya, hata shule za taasisi za dini ambazo kusema kweli zinahubiri usawa hasa kuwasaidia masikini, katika hili nazo ada za shule zao ni kubwa.  Ada katika shule hizi, zipo juu pamoja na kuwa, majengo, vitabu, madawati, vitanda, magadoro (kwa shule za bweni) n.k. vinadumu muda mrefu.

Kuna taarifa, kwa baadhi ya shule hata majengo ya shule hizo wazazi wamechangia; hii ikiwa ni mbali na karo kubwa wanayolipa. Maelezo wanayotoa wamiliki wa shule binafsi ili kaharalisha ada kubwa wanayotoza ni mishahara mikubwa na marupurupu wanayowalipa walimu.

Inasikitisha sana kuwa kinapowadia kipindi cha kulipa ada, baadhi ya wazazi wanauza viwanja, wengine wanakopa na wenye nyumba za kupangisha ni tatizo kubwa kwa wapangaji. Lakini kwa upande wa wafanyakazi, baadhi yao ni  mtanziko.

Je, Kitu ambacho ni muhimu kama elimu kwa kila jamii iweje kilete usumbufu kwa jamii kiasi hicho wakati wakulipa ada? Sawa, mtu anaweza kusema kuwa hawa wanapeleka watoto wao kwa hiari. Lakini ukweli ni kwamba, endapo shule za serikali zingetoa elimu bora naamini hakuna ambaye angepeleka mtoto wake huko ili akalanguliwe.

Ukweli ni kwamba sisi kama jamii tunatakiwa tujitambue tulikotoka, tulipo na tunakokwenda na kwa mikakati gani na kuwa elimu bora inatakiwa ipatikane kwa Watanzania wote; na ipatikane katika shule zote za  serikali na binafsi kwa kiwango sawa.

Lakini ikumbukwe kuwa, enzi za Mwalimu Julius Nyerere, watoto wote waliofaulu walijiunga shule za serikali. Shule binafsi walisoma watoto walioshindwa mtihani wa serikali. Cha kushangaza, siku hizi ni tofauti. Sasa hivi, hata mtoto akishinda mtihani wa serikali, ikatakiwa kujiunga na hizi zinazoitwa “shule bora” sharti apewe mtihani na shule husika- hii ikimanisha kuwa, shule hizi haziutambui mtihani wa serikali kama kigezo cha kujiunga katika shule hizi.

Kibaya zaidi kupitia mitihani hii, hukusanya mamilioni ya fedha ambayo sina hakika kama matumizi yake yanawekwa wazi kwa wazazi wa watoto wanaosoma kwenye shule hizo.

Ni jambo la kushangaza kuwa watoto wanaosoma shule zinazoitwa bora, babu au baba zao walisoma elimu bora ya bure ambayo iliwekwa na sera nzuri za Azimio la Arusha enzi za Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere.

Leo, badala ya kuendeleza mikakati iliyowafikisha hapo, wamewaacha solemba wale waliowadhamini na kuwagharimia kupata elimu bora bure. Unakuta mwalimu au profesa anafundisha shule ambayo mtoto wake hasomi.

Viongozi serikalini- ngazi mbalimbali ikiwamo Wizara ya Elimu na mashirika ya umma watoto wao hawasomi katika shule za serikali ambazo ndizo wanazozitungia sera na kuziendesha, badala yake wanasoma katika shule ambazo hawazitungii sera wala kuziendesha. Hii ni sawa na baba ambaye anawanunulia watoto kauzu kama mboga, lakini yeye mwenyewe anajichana kwa chips na nyama choma. Cha ajabu, baba huyu anaporudi nyumbani anawauliza mke na watoto kama wameshiba.

Enzi hizi imefika hatua kwamba, ilimradi mtu mwanaye anasoma shule bora, haoni uchungu endapo watoto wa wengine wanapata elimu duni. Tatizo ya hali hii ni kutengeneza tabaka la wachache ambao wana elimu nzuri, lakini hawawezi kujisimamia wao wenyewe kwani wanalelewa kama kuku wa kizungu.

Inawezekanaje mwanafunzi wa kidato cha sita ashindwe kwenda na kurudi shule yeye mwenyewe hadi asimamiwe na wazazi ilhali zamani tuliweza kwa maelezo kuwa atapata vishawishi na hasa watoto wa kike?

Upande mwingine kuna kundi kubwa ambalo japo linaweza kujisimamia lenyewe kwa sababu limelelewa kama kuku wa kienyeji, hawana elimu nzuri ya kuwezesha kusimama peke yao katika dunia hii ya utandawazi.

Katika mazingira haya  kama hali hii ya utoaji elimu haitashughulikiwa kuwezesha watoto wote kupata elimu sawa, yafuatayo  yatatokea kwa sababu makundi yote mawili hayawezi kujisimamia yenyewe na ilhali kundi la kwanza litapenda kuendeleza hali ya juu ya maisha waliyoyapata kutoka kwa wazazi wao na shuleni walikosoma.

Hili la pili litataka kwa msemo wa kisasa “kutoka”, wengi wao watashirikiana katika kutengeneza kitu kinachojulikana kwa lugha ya kileo “kundi la watu wa michongo”. Lakini pia, kundi dogo linaweza kujitenga na kwa vyovyote vile kutokana na historia yao ya kutokusimama peke yao, wataajiriwa na kampuni kubwa na kuwa madalali kwenye rasilimali zetu huku kundi kubwa likiweka chuki kubwa dhidi ya wachache kwa kuwajuhumu au yote mawili  yatotokea.

Lakini linaloweza kutokea ni kukosekana kwa mlandano wa utendaji baina ya makundi haya mawili. Yakitokea haya, kuna uwezekano mkubwa wa nchi kuingia kwenye matatizo au hata mchafuko.

Elimu sharti imwezeshe mhusika kupambana na mazingira yanayomzunguka; si kwa manufaa yake tu, bali kwa jamii nzima. Tofauti na hivyo, elimu haina maana. Haya ndiyo anayoyasema Bw. J. Maurus katika kitabu chake kiitwacho: How to use your complexes. Huyu bwana aliandika kwa lugha ya Kiingereza: To achieve something in life, one must come out of  oneself, fight constantly in the inborn need to selfishness and self protection that may go the extent of protecting and loving oneself and become more less hostile to the outer world. Man is mature on the degree he is related to others, family and society and not in the isolation of the lone” Watanzania sharti tubadilike. Hali hii ambako kila Mtanzania anajiangalia yeye mwenyewe na familia yake tu badala ya kuwaangalia na wengine, katika suala hili la elimu Wizara ya Elimu itumbue jipu, kazi ambayo haina gharama yoyote.

Naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutoa elimu bure hadi kidato cha nne. Lakini ili uamuzi huu ulete manufaa yaliyokusudiwa, serikali sharti iende mbali zaidi kwa kufanya uamuzi mgumun kama nitakavyopendekeza kwenye mfululizo huu wa makala hii.

Lengo la barua yangu inalenga kurudisha ubora wa elimu katika hali ya Serikali ya Awamu ya Kwanza ambako watoto wote bila kujali ni mtoto wa mzazi ambaye ni mwenye uwezo au la, walisoma shule moja.

Na katika hili ni vyema serikali ikashauriwa vilivyo hatari  iliyo mbele yetu ya elimu inayotolewa sasa kama haitachukuliwa mikakati ya dhati na makusudi ili  kuibadilisha na kuirudisha katika hali ya elimu ya Serikali ya Awamu ya Kwanza.

Hili linawezekana  tu kama kutakuwa na utashi wa dhati kwa kisiasa kutoka kwa viongozi wetu wa  serikali, hasa Wizara ya Elimu.

 

>>ITAENDELEA….

 

Mwandishi wa makala hii, Leonard Ndimubansi, ni msomaji mahiri wa JAMHURI. Anapatikana kupitia simu: 0713363351/0766687356; e-mail: [email protected]