NGO ni kifupi cha neno Non-Governmental Organization. Kwa Kiswahili neno hili humaanisha shirika lisilo la kiserikali. Kawaida Serikali huwa ina mashirika yake, kwa mfano Shirika  la Bima, Shirika la  Nyumba, Shirika  la Umeme, mashirika ya vyakula n.k.  

Tunapozungumzia NGO maana yake ni kuwa ni mashirika ambayo kwa namna yoyote ile Serikali haihusiki na umiliki wake. Ni mashirika ambayo humilikiwa na watu binafsi.  Serikali huweza kushirikiana nayo tu, lakini si kuyamiliki.

Taratibu za uanzishaji, usajili na uendeshaji huratibiwa bayana na Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na. 24, 2002.

 

1. YAPI YAWE MALENGO YA KUANZISHA NGO

Malengo makuu ya kuanzisha NGO yawe ni kusaidia makundi au kundi maalum katika jamii. NGO siyo shirika la biashara.  Siyo kampuni ambayo muanzishaji  wake hutarajia kutengeneza faida. NGO ni shirika la hisani. Ni shirika la kujitolea kusaidia makundi jamii. Usitarajie kuanzisha NGO kwa ajili ya kutengeneza faida ya fedha. 

 

2. MGAWANYO WA USAJILI WA NGO

Usajili wa NGO umegawanyika katika makundi makuu manne. Kwa mujibu wa sheria, mgawanyo huu umelenga maeneo ya kijiografia. Hata hivyo, ada za usajili na mambo mengine muhimu katika usajili hutegemea mgawanyo huu.

Kwanza,  kuna mgawanyo wa usajili wa ngazi ya wilaya. Usajili wa aina hii huiwezesha NGO kufanya shughuli zake ndani ya mipaka ya wilaya.  Husajiliwa hapo hapo wilayani na hufanya kazi zake ndani ya mipaka hiyo.

Pili, usajili ngazi ya mkoa. Huu huhusisha usajili ngazi ya mkoa na mipaka ya kazi itakuwa ni ndani ya mkoa husika. 

Tatu, usajili ngazi ya Taifa ambao hufanyika makao makuu na mipaka ya kazi ni Taifa zima. 

Nne, ni usajili ngazi ya kimataifa ambao huiwezesha NGO kufanya kazi zake katika taifa zaidi ya moja.

 

3. WAPI UKASAJILI NGO

Kwa ngazi ya wilaya nenda makao makuu ya wilaya yako, na ulizia afisa maendeleo ya jamii.  Hawa ndiyo wanaohusika na usajili. Hali kadhalika, ngazi ya mkoa utaenda makao makuu ya mkoa wako ndipo usajili utakapofanyika.

Aidha, kwa ngazi ya Taifa usajili hufanyika makao makuu ya wizara kwa msajili wa NGO. Kwa sasa wizara husika ni Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto. Wasajili wa ngazi zote hupata mamlaka ya kusajili kutoka kifungu cha 22(1) cha Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.

 

4. VITU GANI VINATAKIWA KATIKA USAJILI

(a) Katiba ya NGO. Hizi hutakiwa nakala tatu zilizojaladiwa (binding).

(b) Maelezo binafsi ya viongozi watatu wa NGO. Mwenyekiti, Katibu na Mhazini.  Maelezo binafsi ni wasifu (CV) pamoja na picha mbili za kila mmoja.

(c) Muhtasari wa kikao cha kuanzishwa kwa NGO ukienda sambamba na majina na sahihi za waanzilishi.

(d) Fomu ya maombi ya usajili iliyojazwa (NGO Form No. 1). Hii hupatikana kwa msajili. Itatakiwa kubandikwa ushuru wa stempu wa Sh 1,500.

(e) Barua ya utambulisho kutoka kwa afisa maendeleo ya jamii wa wilaya, mkoa husika.

(f) Taarifa nyingine yoyote ambayo msajili anaweza kuomba kutoka kwako.

 

5.  ADA ZA USAJILI NI KIASI GANI

Ngazi ya wilaya Sh 80,000, ngazi ya mkoa Sh 100,000, ngazi ya Taifa Sh 115,000  na kimataifa dola za Marekani 350.

 

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA  YAKUB BLOG.

2610 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!