Mapinduzi Z’bar yaenziwe

Januari 12 mwaka huu kama ilivyo kila mwaka, Visiwa vya Zanzibar vimeadhimisha Mapinduzi matukufu ya visiwa hivyo yaliyofikisha umri wa miaka 52.

Mapinduzi hayo yanakumbukwa katika kuonesha nguvu ya umma inafanya kazi kuliko kitu chochote kile, pale umma unapochoshwa na ukandamizwaji.

Umma unaweza kuvumilia unyanyaswaji kwa muda, lakini si kwa wakati wote. Sababu udhalili wa umma siyo udhaifu wa umma, umma ukiamua una nguvu za kutisha.

Mapinduzi ni kitu kigumu sababu yanakusudia kuwaondolea mamlaka walio madarakani.

Bila shaka walio madarakani kwa kunogewa na utamu wa madaraka, kamwe hawafikirii kuyaachia, kwa hiyo ni lazima wanakuwa wamejipanga kwa zana za kila aina katika kujihami na lolote linaloweza kuwaondolea utamu wanaouona ni haki yao peke yao. Kwa maneno mengine ni utamu usio wa haki.

Kwa hiyo, katika Mapinduzi ya Zanzibar kilicholengwa ni kuwaondolea utamu wa madaraka waliokuwa wanatawala kinyume cha haki za binadamu – Waarabu chini ya sultani – wakiwatawala watu wa asili ndani ya ardhi yao na kuwageuza watu wa daraja la chini kabisa na wakiwa wamewaondolea kabisa hadhi ya utu na kuwafanya wabaki ni watu wa kutumikishwa tu kama vyombo visivyo na uhai. Kamwe haijawahi kutokea na haitatokea vyombo kama gari, trekta, pikipiki na kadhalika vidai haki za kujitawala wala kuwatawala wengine. Vitabaki vikitawaliwa milele.

Kwa hiyo, siku ya siku ilipofika ya wananchi wa asili kule Zanzibar kusema sasa basi inatosha, ndipo yakafanyika mapinduzi bila kujali kwamba wageni kutoka bara jingine waliokuwa madarakani – Waarabu, wana zana nyingi za kujihami pamoja na vikosi vya kuwalinda. Wananchi waliojulikana kama wakulima na wakwezi, bila zana za kutosha na za kisasa wakaamua kukabiliana na nguvu za sultani na kumuondoa madarakani.

Huo ndiyo ninaoutazama kama ugumu wa mapinduzi hasa hayo ya Zanzibar, nikiwa nimelinganisha nguvu za zana zilizotumiwa na watawala wa Kiarabu na nguvu ya umma. Kweli Mapinduzi ya Zanzibar yanapaswa kuenziwa.

Heshima ya wakulima na wakwezi wa Zanzibar ikapanda juu na kujulikana duniani kote. Zanzibar, Visiwa vilivyojulikana duniani kote, navyo vikaanza kutambulika kuwa ni visiwa vinavyokaliwa na wenyewe, visiwa vyenye wenyeji wa asili, tofauti na ilivyojulikana mwanzo kama visiwa vinavyokaliwa na Waarabu wakati weusi wakiwa ni manamba tu, kwa maana ya watu wa kutumikishwa.

Kwa hiyo, kwa mtu yeyote mwenye uelewa ulio sawa hana budi kuyaenzi Mapinduzi hayo. Nasema mtu mwenye uelewa ulio sawa hata awe ni wa nje ya visiwa vya Zanzibar, ni lazima ayaenzi Mapinduzi hayo kwa vile yaliweza kurudisha heshima ya utu hata kama heshima hiyo siyo ya mahali alipo yeye. Mtu mwenye umakini anayeujali ubinadamu ni lazima authamini utu bila kujali yuko upande gani wa dunia.

Kwa mantiki hiyo, litakuwa ni jambo la ajabu kumuona mtu aliye mzaliwa wa Visiwa vya Zanzibar anajifanya kutoyathamini Mapinduzi hayo matukufu yaliyourudisha utu wa Mzanzibari. Sababu tujiulize, mtu wa mbali na Zanzibar anapoguswa na utu wa Mzanzibari na hivyo kuyaenzi Mapinduzi ya 1964, iweje kwa mtu aliye Mzanzibari ayapuuzie Mapinduzi hayo?

Mwanazuoni mmoja, ambaye pia ni mwanadiplomasia, anaonesha kukerwa sana na kitu kinachoendelea visiwani Zanzibar ambapo baadhi ya watu wanaonekana kukinzana na Mapinduzi hayo. Anaonesha kuwashangaa watu – wawe wa Visiwani au Tanzania Bara – wasiopenda kuyasikia Mapinduzi akisema kwamba kama ni weusi basi hao ni watumwa wanaoushangilia utumwa wao na kama ni wa asili ya Uarabu basi hao wanapaswa kupuuzwa kwa vile wanaulilia unyama waliokuwa wanawafanyia wenzao weusi.

Kwa wafuatiliaji wa mambo wataona jinsi watumishi wa ndani kutoka Afrika wanaokwenda kwenye nchi za Kiarabu kutafuta ajira wanavyodhalilishwa na wanaowapatia ajira.

Wanafanyiwa mambo ya aibu kupitiliza kana kwamba watumishi hao siyo binadamu. Ni heri ya mbwa wanaofugwa, maana mfuga mbwa humpenda mbwa wake. Ni tofauti na Waarabu wanaowaajiri watumishi wa ndani kutoka Afrika.

Kwa hiyo, kuuchukulia unyama wanaofanyiwa watu weusi ndani ya bara la Waarabu kwa wakati huu na vilevile kuukumbuka unyama waliofanyiwa weusi ndani ya ardhi yao na watu walewale enzi hizo, mtu akakosa kuyathamini Mapinduzi yaliyouondoa unyama huo kule Zanzibar ni lazima zijitokeze fikra za kwamba hapo panakosekana utu.

Kunakosekana uwezo wa mtu kujitambua, sababu mtu yeyote anayejitambua, hata kama siyo wa jamii inayofanyiwa unyama, anapaswa aelewe kwamba unyama anaofanyiwa mwingine akifanyiwa yeye atajisikiaje!

Yeyote asiyefikiria hivyo hapaswi kujiweka fungu moja na watu wengine. Maana mtu ni mtu bila kujali rangi yake wala kabila lake. Hapo ndipo ulipo umuhimu wa kuyaenzi Mapinduzi ya Zanzibar, yaliyouondoa unyama dhidi ya utu.