Buriani Mzee Kitwana Selemani Kondo ‘KK’

Jumatano Mei 24, 2017 ni siku ambayo itakumbukwa na Watanzania wengi na hasa Waislamu, kwa kuondokewa na mzee wetu, Alhaj Kitwana Selemani Kondo, maarufu KK au mzee wa mjini.
Siku nne kabla ya kifo chake, mwanaye wa kiume, Adnan Kitwana Kondo maarufu Saku, alinitumia ujumbe kwenye WhatsApp akiniarifu kuwa mzee KK amelazwa Hindu Mandal na hali ya afya yake inazidi kuzorota. Siku ya pili yake nilimtumia ujumbe Saku kutaka kujua hali ya mzee inaendeleaje. Majibu ya Saku yaliniashiria kuwa mzee wetu amekaribia kufika mwisho wa safari yake.


Aliniambia kuwa kwa sababu ya ukaribu wangu na mzee KK, hana budi aniarifu ukweli ulivyo. Aliniarifu kuwa hali ya mzee ni mbaya sana na kwamba kinachosubiriwa ni rehma zake Mwenyezi Mungu.
Kwa kweli, ujumbe ule ulihuzunisha sana na sikuweza kuhimili uchungu ule peke yangu. Nikamwarifu Profesa Hamza Mustafa Njozi, Makamu Mkuu wa Chuo cha Waislamu Morogoro na Faraji Abdallah Tamim, mwalimu wa chuoni hapo.
Ilipofika Jumatano Mei 24, nikapata taarifa kupitia moja ya kundi sogozi (chat groups) kuwa mzee KK amefariki dunia. Pamoja ya kuwa hali hiyo ilikuwa tayari inatawala fikra zangu lakini kifo hakizoeleki.
Taarifa hiyo ilinikuta nikiwa najiandaa kwenda uwanja wa ndege wa Kuala Lumpur kumsindikiza shemeji yangu. Wakati huo kwa saa za Malaysia ilikuwa kama saa 4 usiku. Nilipwelewa sana kwa sababu ya uhalisia kuwa sitowahi kumzika mzee wangu mzee KK. Haikuchukua dakika 10 baada ya taarifa hizo, Saku kanipigia simu ambayo hatukuweza kuzungumza hata neno moja kutokana na vilio.


Kila mmoja alikuwa analilia kwake. Haikuchukua muda akakata simu na kunitumia ujumbe mfupi uliosema “KK is dead. Allah is Great”. Mara tu baada ya kupata taarifa hiyo nilichanganyikiwa na kuona uchungu sana baada ya kuona kuwa sitoweza kumzika mzee KK ambaye aliwahi kunitamkia mbele ya mkewe, Bi Hanifa, kuwa ikitokea atafariki kabla mimi basi angependa asaliwe Masjid Mtoro, azikwe makaburi ya Tambaza na mimi niwe mmoja kati ya watu watakaoingia kaburini. 
Katika maishani mwangu, hii ni mara ya tano kuandika tanzia yaani ‘obituary’. Buriani zilizotangulia ni za aliyekuwa mwalimu wangu Chuo Kikuu DSM na rafiki yangu wa karibu, Profesa Ken Edwards, mwenye asili ya Jamaica, aliyekuwa Afisa wa Uhusiano wa NSSF, Alfred Ngotezi, rafiki yangu tokea utotoni Abubakar Mohamed Saleh Tambaza maarufu Babu Chela na Saidi Masimango aliyekuwa Mkurugenzi wa Teknohama NSSF.


Kila niandikapo tanzia huwa nafanya hivyo nikiwa na moyo mzito na huzuni sana. Kila niandikapo huwa naomba kuwa hiyo iwe ndiyo ya mwisho kwani kuandika tanzia ni jambo zito sana hasa ikiwa inamuhusu mtu wa karibu yako kama nilivyo mimi kwa mzee KK na hao waliotangulia kabla yake.
Kwa huzuni niliyokuwa nayo, niliamua kutoandika tanzia hii kwa sababu nisingeweza kufikia mwisho kwa kilio. Lakini mara tu baada ya habari za msiba kuenea nikaanza kupata salamu kutoka kwa watu mbalimbali akiwamo Prof. Hamza Njozi, mdogo wangu Abdul Dau na Saku.
Ujumbe kutoka kwa Saku ndiyo uliozidisha majonzi yangu lakini pia ulinipa nguvu ya kuandika kwani kama alivyosema Saku na nakuu ‘Dr. please write an eulogy for KK. You knew him well, no one can talk of him better than you’.
Baada ya kutafakari nikaona kama sikuandika nitakuwa sikumtendea haki mzee Kondo. Kwa kuwa nimekosa fursa ya kumtimizia wosia wake kuwa niwe miongoni mwa watu watakaoingia kaburini kumzika, nimeona nisikose vyote.  Kwa kuzingatia kanuni ya fiqh kuwa kama jambo haliwezi kufanyika lote basi lisiachwe lote. Waswahili nao wana msemo wao ‘lisobudi hutendwa’. Hivyo basi nimeamua kuandika tanzia hii kwa huzuni na unyonge kubwa.


Nimemfahamu mzee tokea nikiwa mdogo kwa sababu ya kuzaliwa na kulelewa Mwembetogwa, jijini Dar es Salaam. Wakati wa utoto wangu sikuwa na ukaribu sana na mzee Kondo kwa sababu ya tofauti ya umri. Ukaribu wangu kwake ulianza mwaka 1995 wakati alipoteuliwa na Rais Ali Hassan Mwinyi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (THA) ambapo mimi nilikuwa Mkurugenzi wa Masoko kwa miaka tisa.
Nakumbuka siku moja mara tu baada ya kumaliza kikao cha Bodi, niliamua kumsindikiza mpaka kwenye maegesho ya gari. Baada ya kufika kwenye gari yake, nikaona nichukue fursa hiyo nijitambulishe zaidi kwake kwani mpaka wakati huo alikuwa ananifahamu kama Mkurugenzi wa Masoko. Nikajitambulisha kuwa mimi nimezaliwa na nina asili ya Dar es Salaam. Mara tu baada ya kumwambia hivyo haraka kabisa akaniuliza baba yangu nani. Ili kumtosheleza kiu chake sikutaka kumtambulisha baba yangu. Badala yake, na kwa makusudi kabisa nikamwambia mimi ni mtoto wa ‘John’ Iddi.
Mara tu nilivyojitambulisha akasema “wewe mwanangu, ‘John’ Iddi alikuwa mkwe wangu.” Nilifanya makusudi kumtaja ‘John’ Iddi ambaye ni baba yangu mkubwa. Jina lake halisi ni Thabit Iddi Dau. Jina la ‘John’ aliitwa na mama yake baada ya kumzaa akiwa ana umri mkubwa sana. Baada ya kujifungua akasema mtoto huyu nimempata ‘Jioni’ kwa maana ya kuwa amemzaa hali ya kuwa yeye ana umri mkubwa sana na alikwisha kata tamaa ya kupata mtoto.


Pamoja ya kuwa jina lake halisi lilikuwa Thabit lakini tokea utotoni alijulikana kwa jina la ‘Jioni’ ingawa kwa urahisi wa matamshi badala ya kusema ‘Jioni’ likavuma jina la ‘John’. Marehemu Thabiti alijulikana sana kwa jina hilo la utani hadi kufa kwake.
Nimesema niliamua kujitambulisha kupitia baba yangu mkubwa kwa makusudi kwa sababu marehemu mzee ‘John’ Iddi alikuwa na mkwewe akiitwa Kijakazi wa Mgoto ambaye alikuwa anafanya kazi Halmashauri ya Jiji (City Council). Bibi Kijakazi alikuwa na binti yake akiitwa Kurwa na ndiyo aliyekuwa mke wa kwanza wa marehemu mzee ‘John’ Iddi.
Katika uhai wao walijaaliwa kupata watoto wawili. Iddi ‘John’ na Mwatatu Thabit. Iddi alifariki mwaka 2001. Mwatatu yu hai ameolewa na Mohamed Mfaume maarufu ‘Difu’ ambaye alikuwa golikipa wa Yanga, Cosmo na Timu ya Taifa.
Tokea siku ile ambayo nilijitambulisha kwa mzee Kondo, tukajenga ukaribu sana na alikuwa ananipenda sana. Ilikuwa haipiti wiki bila kwenda nyumbani kwake Hill Road Oyster Bay na baadaye mtaa wa Mtitu Upanga kwenda kumwamkia na “kupata habari za mjini.”
Ni kutokana na mazoea hayo ndipo mzee KK akapata jina lingine la utani la “mzee wa mjini”. Na ni kweli, wakati wa uhai wake, kila utakapoenda kwa mzee KK hukosi kupata “habari za mjini” ingawa wakati mwingine zinakuwa ni habari au fikra zake yeye lakini ili kuzipa uzito atakwambia kuna habari mjini kuwa … (hapo anaeleza hiyo habari ilivyo).
Moja katika hizo habari za mjini zilininufaisha sana na kuninusuru na janga kubwa sana ambalo lingenikuta. Leo hapa si mahala pake kuzungumzia habari hiyo. In Shaa Allah kuna siku nitaitafutia nafasi kuizungumza. Naendelea kumshukuru sana kwa hilo na mengi ambayo amenifanyia mimi na watu wengine wengi.
Mzee KK atakumbukwa, kuliliwa na wengi kwani alikuwa mwepesi sana kusaidia watu wenye shida. Marehemu alikuwa mcheshi na mwenye kupenda maskhara sana. Alichanganyika na watu wa kila rika. Alikuwa mtu wa msaada sana kwa watu wa aina zote, wake kwa waume.
Nyumbani kwake kulikuwa hawapungui wageni wa kila aina kuanzia wanasiasa, wanamichezo, viongozi wa dini nk. Alikuwa ni mtu wa watu sana kiasi ya kwamba haipiti mwezi bila kupita mitaa ya Kariakoo (na hasa klabu ya Pan African) kwenda kupiga soga na watu wa mjini wenziwe.
Kwa upande wa siasa, mzee Kondo ametoa mchango mkubwa sana kwa muda wote wa uhai wake nje na ndani ya Bunge, TANU na CCM. Mzee KK alikuwa mzalendo ambaye aliitakia mema nchi yetu. Kwa wale wazee wa Dar es Salaam waliobaki watakumbuka sana mchango alioutoa tokea wakati wa ukoloni na hasa baada ya Uhuru. Yapo mengi ya kihistoria aliyoyafanya kwa kuinusuru nchi yetu na kufika hapa ilipofika leo.


Moja kati ya sifa zake nyingi ni ujasiri. Mzee KK hakuwa mwoga na alikuwa na ujasiri wa kusimamia jambo ambalo anaamini ni sahihi na lina manufaa kwa nchi yetu. Mifano iko mingi. Kwa leo itoshe tu kuwa alisimamia suala la upatikanaji wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro kwa kujenga hoja kwa Rais wa wakati huo, Mhe. Benjamin William Mkapa. mpaka Mhe. Rais akashawishika kuwa ni jambo jema kuanzishwa kwa chuo hicho kwenye majengo ya kilichokuwa Chuo cha Mafunzo cha TANESCO.
Kama kuna mtu mmoja ambaye ametoa mchango wa kipekee uliosababisha  upatikanaji wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro (MUM) mtu huyo ni mzee Kitwana Kondo. Kwa kuenzi jitihada zake hizo, na kwa kuzingatia mzee Kondo ni Mwenyekiti mwanzilishi wa Taasisi ya Maendeleo ya Waislamu (MDF), taasisi ambayo ndiyo Mmiliki wa MUM, nashauri uongozi wa Chuo utafute jengo lenye hadhi pale chuoni lipewe jina lake. Kwa siku za usoni, chuo kitakapoanza kutoa shahada za Uzamivu (PhD), nashauri mzee Kitwana Kondo atunukiwe PhD (Honoris Causa) posthumously.
Sambamba na ujasiri, mzee KK alikuwa anaipenda sana dini yake na alikuwa mtetezi mkubwa wa Waislamu. Ilikuwa kila ukienda nyumbani kwake ukimtajia aya kwenye Quran, basi haraka huchukua kitabu chake kidogo (note book) na kuiandika ili akaifanyie kazi kwa vitendo au hata kwa kuzungumza kwa wengine. Miongoni mwa aya ambazo mzee KK alikuwa akizipenda sana ni Aya ya 10 na ya 11 kwenye Sura ya 61 (As-Saff), pia Aya ya 31 kwenye Sura ya 76 (Al-Insan au kwa jina lingine Dahr). Kwa kumuenzi mzee KK sitotoa tafsiri ya aya hizo kwa makusudi ili msomaji upate ushawishi wa kwenda kuzisoma mwenyewe ili nawe upate fadhila za kuisoma Quran.


Mzee Kondo alijivunia sana Uswahili na Uzaramo wake. Watoto wake wengi aliwapa majina ya Kizaramo kama vile Mtogole, Azimala, Msakuzi nk. Pamoja na nyadhifa mbalimbali alizokuwa nazo serikalini, kamwe mzee Kondo hakusahau marafiki zake ambao wengi wao walikuwa ni watu wa kipato cha chini sana. Baadhi yao ni marehemu mzee Kibiriti, marehemu mzee Sindano, marehemu Omar AbdulRahman maarufu ‘Ugundo’, Captain Maliki nk.
Ukaribu wake na watu wa kawaida umefanya mpaka baadhi ya watu wafikirie kuwa mzee Kondo hakusoma shule. Nakumbuka mwaka 1996 wakati mzee Kondo akiwa Mwenyekiti wa Bandari nilikwenda Shirika la Bima ya Taifa (NIC) kufuatilia madai ya gari yangu Musso TZH 3336 ambayo ilipata ajali. Nilifika NIC na kuonana na afisa mhusika wa madai. Katika mazungumzo yetu akabaini kuwa mimi ni Mkurugenzi wa Masoko wa THA. Alinipa pole sana kwa sababu kwa maneno yake mwenyewe, THA tumepata Mwenyekiti ambaye hajui kusoma.
Alishangaa mzee Kondo anawezaje kusoma makabrasha na kuongoza vikao vya Bodi ikiwa hata kuzungumza Kiingereza hawezi. Nikamjibu kuwa mzee Kondo ni msomi kwani mwaka 1963 alihitimu shahada kwenye ‘Strategic Studies’ kwenye Chuo Kikuu cha Howard Washington DC, Marekani.
Aidha, mzee KK amepata mafunzo kwenye nchi kadhaa zikiwamo Ujerumani na Yugoslavia. Yule afisa hakuamini na tukawa na malumbano makali sana. Msingi wa hoja yake ni kuwa mzee KK anaandikwa vibaya sana kwenye gazeti (pamoja ya kuwa kwa sasa gazeti hilo limekufa lakini jina nalihifadhi) na picha inayojitokeza ni kuwa mzee huyu hakusoma kabisa. 


Nimesema hapo awali kuwa mzee Kondo alikuwa anajichanganya sana na watu wa aina na rika zote. Nina hakika si wengi wanaofahamu kuwa wakati wa uhai wake mzee Kondo aliwahi kuwa Katibu ya Klabu ya Yanga, Dar es Salaam miaka ya 1950. Pia mwaka 1962 alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga. Wakati huo Mwenyekiti alikuwa mzee Mohamed Sultan Mabosti, Katibu Mkuu ni mzee Jabir Katundu (alichukua nafasi kutoka kwa mzee Juma Vijiga) na Makamu wake mzee Juma Shamte.
Wote hao wameshatangulia isipokuwa mzee Jabir Katundu. Tunamwomba Mwenyezi Mungu atutunzie mzee Jabir ili tuendelee kuvuna busara zake si tu katika masuala ya mpira bali maisha kwa ujumla.
Kati ya mambo mengi sana ambayo nimejifunza kutoka kwa mzee KK ni kuwa unapoitwa na mkubwa wako wa kazi – iwe ofisini au nyumbani – jiandae kwa kujua saa ya kuitwa na si saa ya kuondoka. Katika hili alinisimulia kisa kimoja wakati akiwa Meya wa Dar es Salaam.
Kuna Jumapili moja Mwalimu Nyerere aliwaita viongozi wa Mkoa (akiwamo mzee KK) nyumbani kwake Msasani saa 4 asubuhi. Ujumbe huo uliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa wakati huo. Walipofika Msasani wakakuta Mwalimu ameenda kanisani. Baada ya misa Mwalimu akaenda ofisini Ikulu.
Ujumbe ulisubiri Msasani kwa muda mrefu. Ilipofika saa 7 mchana Mkuu wa Mkoa akatoa rai kuwa waondoke na kama kutakuwa na taarifa yoyote watafahamishana. Mzee KK alirudi nyumbani kwake Hill Road Oysterbay. Haikuchukua muda kapigiwa simu kuwa Mwalimu anamwita Msasani. Alipofika Msasani Mwalimu akataka kujua sababu zilizomfanya mzee Kondo asiende nyumbani kwake saa 4 asubuhi kama alivyoagiza. Mzee Kondo akajitetea kuwa alikwenda saa 4 kama alivyoagiza na walisubiri hadi saa 7 ndipo kiongozi wa msafara wao Mkuu wa Mkoa akawaruhusu waondoke.
Mwalimu akamwambia mzee Kondo kuwa yeye aliwapa muda wa kufika Msasani saa 4 asubuhi lakini hakuwaambia muda wa kuondoka. Baada ya maneno hayo Mwalimu akamwambia kuwa ameshatengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa na kwamba yeye mzee Kondo ana bahati kwani yeye ni Diwani wa kuchaguliwa kwa hiyo hana namna ya kumfukuza kazi.


Mzee Kondo ameondoka na mambo mengi kifuani mwake. Alikuwa hazina kubwa sana kwa Taifa. Mimi binafsi nimejaribu mara kadhaa kumuomba aandike historia yake lakini alikataa kabisa. Pamoja ya kuwa mzee Kondo alinisikiliza na kukubali ushauri wangu kwenye mambo mengi, lakini hili la kuandika historia yake alikataa kabisa.
Mara zote ninapokuwa namkumbusha kuhusu suala hili jibu lilikuwa, ‘nataka nife huku nimenyooka.’ Kwa bahati mbaya sana udhaifu huu wa kutoandika historia zao wanao viongozi wetu wengi. Wamebeba hazina kubwa na wakiondoka wanaondoka nazo bila kutuachia urithi huo adimu.
Yapo mengi sana ya kuandika kuhusu mzee KK na nafasi hapa haitoshi. Kwa kumalizia, kwa wale wasiofahamu, mzee KK alikuwa mpenda sana mashairi. Miongoni mwa mashairi yake aliyokuwa akiyapenda ni shairi la Muyaka bin Ghassany wa Mombasa.
Alipoanza kuumwa kiasi miaka 3 iliyopita, ilikuwa kila nikienda kumjulia hali huwa namsomea shairi la Muyaka. Pamoja na kutokuwa na fahamu lakini nikianza tu kumsomea shairi la Muyaka hufungua macho na kunitazama kisha akatokwa na machozi na baadaye kufunga macho.
Kwa kumuenzi mzee, nimeamua kulinukuu shairi ambalo marehemu Mzee KK alikuwa analisoma ghibu.


Akutendeae Mema, Kushukuru ni lazima
Jaza ya mema ni mema, Maovu kutoyatia
Mbona umeghafilika? Kwa jambo lisilo shaka?
Shetani umemshika, Na kumuacha Nabia?
Unajifanya Mtesi, Kwa Mola wako Mkwasi
Unavitupa viasi, Sina la kukwambia
Silaha zote ni Zake, Wala na riziki Zake
Unakunywa maji Yake, Mbona umekosa haya?
Vita vyako fahamu, Havimdhuru Karimu
Ila wewe Bahaimu, Jijue Utaumia
Itunze yako fikara, Uwafikiri mabora
Wenye ngome na minara, Na panga za kuchinjia
Yatafakari mauti, Yeyote hayamuachi
Wala hayana wakati, Ghafla hukujilia
Yu wapi Firauni, Yu wapi Karuni
Na Shadadi maluuni, Wote wameangamia
Zao zilipokwisha, Ziraili kawafisha
Wameyawacha makasha, Na mambo haya na haya
Waimefika akhera, Madhalili mafukara
Uwapi wao bora, Wote umewakimbia
Kaburi zimewakaza, Hapana la kupumbaza
Kote kumefunga kiza, Adhabu kuwashukia
Adhabu hiyo ni kuu, Tena motoni kuwa juu
Majuto ni mjukuu, Tahadhari na dunia
Wapita na Siratini, Kuwangukia motoni
Kuteketea maini, Maisha kuteketea
Na yote ninayoyasema, Yatakufika lazima
Safari mbele na nyuma, Wengine hutangulia

Naam, ni kweli kabisa safari ni mbele na nyuma wengine hutangulia. Mzee KK ametangulia. Kwa kuondokewa na mzee Kitwana Selemani Kondo, Dar es Salaam will never be the same.  Maskini Dar es Salaam, imeondokewa na watu na kubaki na mfano tu wa watu!
Mwenyezi Mungu amlipe mema na azipe uzito amali zake ziwe na mizani ya juu kuliko mapungufu yoyote ya kibinadamu ambayo alikuwa nayo. In-Sha’Allah Mwenyezi Mungu Amruzuku Pepo na In-Sha’Allah Atukutanishe Peponi Firdaus, Ameen.