Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha CCM wakiimba na kucheza wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika jijini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Na Deodatus Balile, Ruangwa

Ndugu msomaji wangu, heri ya mwaka mpya 2022. Naamini umefika salama katika mwaka huu baada ya changamoto kubwa tulizopitia mwaka 2021. 

Wengi walitamani kufika mwaka huu wa 2022, lakini Mungu hakuwapa nafasi hiyo. Mimi ni muumini wa Kanisa Katoliki. Naamini katika Mungu. Kila jambo naamini linatokea kwa mapenzi ya Mungu. 

Wewe na mimi kuuona mwaka 2022 si kwa umahiri wetu wa kukwepa kifo, bali ni kwa mapenzi ya Mungu.

Sitanii, bila kujali dini zetu, Bwana, Mungu, Allah ndiye mchungaji wetu, hatutapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabichi hutulaza. Kando ya maji ya utulivu hutuongoza. Nimetohoa maneno haya kutoka katika maandika matakatifu ya Biblia Zaburi 23:1. Nasema kila awaye kwa imani yake, mwabudu, msujudie, mwamini Mungu na kumtolea zaka, sadaka, malimbuko na matoleo. Sadaka kwa Mungu ni upatanisho kati ya mwanadamu na Muumba wake. Heri ya mwaka mpya.

Wiki iliyopita nimefanya mahojiano na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa kijiji kwake Ndagala, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi. Mahojiano hayo yamezaa habari kuu tuliyoichapisha leo katika gazeti hili. Ukisoma mahojiano hayo, unaona fukuto ndani ya CCM. Fukuto la kugombea uongozi.

Baada ya mahojiano hayo, nimekaa hotelini nikajipa muda wa kufikiri. Nikapitia kumbukumbu zangu za uongozi wa nchi hii. 

Namshukuru Mungu walau kwa umri wangu huu wa nusu karne, nimepata fursa ya kuuona uongozi wa Awamu ya Kwanza hadi ya Sita sasa, na angalau nimezaliwa enzi za chama cha ukombozi cha TANU na huko Zanzibar, ASP.

Nimezisoma darasani katika “kipindi cha Siasa” na nimeziishi, ahadi 10 za Mwana – TANU. Kwa ruhusa yako msomaji, naomba nizitaje hapa kama zilivyo kwenye Katiba ya TANU. 1. Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja. 2. Nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote. 3. Nitajitolea nafsi yangu kuondoa umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma. 4. Rushwa ni adui wa haki, sitapokea, wala kutoa rushwa.

Ahadi ya 5. Cheo ni dhamana, sitatumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu. 6. Nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu na kutumia elimu yangu kwa faida ya wote. 7. Nitashirikiana na wenzangu wote kujenga nchi yetu. 8. Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko. 9. Nitakuwa mwanachama mwaminifu wa TANU na raia mwema wa Tanganyika na Afrika. 10. Nitakuwa mtiifu na mwaminifu kwa Rais wa Serikali ya Tanganyika.

Sitanii, kuna kiongozi mmoja mkubwa serikalini nimepata kumwambia jambo. Ahadi namba nane kwa baadhi ya wana-CCM na viongozi wa vya vya upinzani imepoteza mwelekeo. Majungu, fitina, uongo, kusemeana kumegeuka ufahari. Kiongozi huyo nilimwambia haya yafuatayo: “Katika uongozi wa nchi yetu kuna jambo moja la kusikitisha. Kila awamu wanazua la kuzua, almradi kumgombanisha Rais na wasaidizi wake.

“Kipindi cha uongozi wa Mzee Mwinyi, liliibuka sakata la Mzee Malecela. Mwaka 1994 Mzee Mwinyi alilazimika kuvunja serikali baada ya kumtungia zengwe Mzee John Samwel Malecela. Nikamwambia mwaka 2004 nchi ilikuwa na zengwe kubwa. Rais Benjamin Mkapa aliaminishwa kuwa Jakaya Kikwete atauza nchi.

“Kwa kuwa baadhi wameishatangulia mbele ya haki nataja, Rais Mkapa akajenga chuki dhidi ya Kikwete. Akaamua chaguo lake la mrithi wa urais awe Dk. Abdallah Kigoda. Katika Mkutano wa Kamati Kuu ya CCM uliofanyika Zanzibar mwaka 2005, Kikwete aliwatolea uvivu viongozi waliokuwa wanamfitini. Aliwaambia urais anautoa Mungu, na kama hukupangiwa hupati.

“Mwaka 2008, tulishuhudia kilichotokea. Jakaya Kikwete aliaminishwa na mitume 12, wakiongoziwa na marehemu Samuel Sitta kupambana na Edward Lowassa. Mtakumbuka taarifa ya Richmond bungeni Februari 2008 kuhusu Lowassa, akihoji ilikuwaje Dk. Harrison Mwakyembe akasafiri hadi Marekani, lakini hakashindwa kumpa haki ya asili ya kumsikiliza akaishia kumtuhumu vibaya kwenye ripoti ya Richmond.

“Leo tunajua wale mitume 12 walivyoyeyuka. Mwakyembe ameendelea kufahamika kwa watu uhalisia wake, pamoja na digirii zake nne, akasambaratishwa na Kinanasi wa darasa la saba. Kuna mtu ameniambia Dk. Mwakyembe akigombea hata uenyekiti wa mtaa kwao ataupata kwa tabu sana baada ya watu kumfahamu hulka yake.

“Hili zengwe liliendelea 2015, baadaye Dk. John Magufuli akawa anashughulika na kila aliyeambiwa na hawa wafitini kuwa ana nia ya kugombea urais. Alianza na Bernard Membe. Januari Makamba akaonja machungu yake. Mwigulu Nchemba hakuachwa kando. Nape Nnauye naye akaonja joto ya jiwe. Hapo sitawataja akina Mzee Yusufu Makamba, John Guninita, Emmanuel Nchimbi, Abdulrahman Kinana na wengine walioonja joto ya jiwe kwa kuchongewa na wanaharakati huru!!!”

Sitanii, upepo mchafu sasa naona unamwelekea Kassim Majaliwa Majaliwa. Anavurumishiwa kila kombora. Nafuatilia kwenye mitandao ya kijamii. Kigogo 2014 ameanza anamponda akimwita KATELEFONI. 

Karibuni amesema amefuatilia hadi kijijini kwake Ndagala hapa Ruangwa, amebaini kuwa hana nia ya kugombea urais. Kwa bahati mbaya, wanaosambaza “vumbi hili la Congo” wengine wamepata kuwa wahanga wa fitina za aina hii. Hawakujifunza kitu kwa yaliyowafika.

Ni kwa mantiki hiyo msomaji nimeona nikupe zawadi ya mwaka mpya kukumbusha tuliyopitia. Hawa watengeneza fitina ndio wanaifanyia mchezo mchafu CCM. Ni hawa hawa wanaochongea wapinzani na kuwafungulia kesi zisizo na vichwa wala miguu. 

Ila kama alivyosema Rashid katika kitabu cha Kuli, haya YANA MWISHO. Hakuna marefu yasiyokuwa na ncha. 

Huu mchezo wa fitina unaoendelea ndani ya CCM, ukamwagikia hadi kweye vyama vya upinzani, usipodhibitiwa ni mauti yao CCM. Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania.

By Jamhuri