DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Mwanasoka maaarufu nchini raia wa Zambia, Cletous Chama, ameondoka nchini miezi mitatu tu iliyopita lakini taarifa zake za kurejea nchini zinavuma kwa wingi kuliko hata kile anachokifanya akiwa uwanjani huko aliko sasa.

Hali hii ni marudio ya ile hali iliyowahi kutokea kwa mchezaji mwingine wa soka, raia wa Uganda, Emmanuel Okwi.

Wakati nyota yake ikiwa juu katika soka la Tanzania, ilikuwa kila Okwi anapoondoka nchini, hakai muda mrefu nje ya nchi kabla wakubwa wawili hawajaanza kuvutana mashati na kisha mkubwa mmojawapo anafanikiwa kuinasa saini yake. Anamsajili.

Baada ya muda mfupi Okwi anarudi nchini na kusajiliwa kweli. Hii imewahi kutokea zaidi ya mara tatu kama nipo sahihi. Kwa hakika haijatokea mara moja! 

Sasa ninadhani kwa uhakika kabisa Chama naye anaelekea kule kule alikokuwa Okwi, ambaye kwa sasa yuko nchini kwao Uganda, akizichanga upya karata zake. 

Tunaomfuatilia kwa karibu mshambuliaji huyo, kwa hakika pale alipo sasa Okwi ni kama amejiegesha tu, atakuja nchini wakati wowote na atachezea timu kubwa. Kama si katika dirisha hili dogo linalofunguliwa katikati ya Desemba, basi atakuja kwenye usajili wa dirisha kubwa. Atakuja tu, hii inaonekana wazi kabisa.  

Je, ligi ya soka ya Tanzania Bara maarufu kwa sasa kama NMB Premier League, ina thamani kubwa na kila mchezaji anatamani kuwa sehemu ya washiriki wa ligi yenyewe? Inawapa uhuru hawa nyota wa soka? Hawa mastaa wanalipwa vema kuliko watoto wa nyumbani? 

Haya ni baadhi ya maswali magumu ambayo kwa namna yoyote ile hata majibu yake pia ni magumu. 

Kuna kitu kimejificha hapa katika soka la Tanzania Bara. Inawezekana mimi na wewe hatukioni kwa urahisi, lakini tayari wenzetu hawa, akina Okwi na Chama, wanakiona katika mpira wetu na maisha ya Kitanzania kiujumla. 

Kinachoumiza roho na kushangaza juu ya nyota wa soka wa Kitanzania waliokwenda nje na kurudi nyumbani ni kimoja tu; hawa wakirudi nchini wanakwenda kucheza soka katika timu za daraja la kati, hawarudi katika timu kubwa kama ilivyo kwa hawa akina Okwi. 

Chukua mfano wa Banda aliyekuwa akikipiga Afrika Kusini. Amerudi nchini na badala ya kuchezea klabu kubwa, amekwenda Mtibwa Sugar. 

Nickson Kibabage naye amerudi kutoka Morocco alikukuwa akicheza soka la kulipwa na sasa yupo na KMC. 

Elioud Ambokile naye ametoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kujiunga tena na Mbeya City. Moses Kitandu amerudi kutoka Msumbiji na sasa yupo Sumbawanga na Tanzania Prison. Kwa hakika kuna tatizo mahala fulani. 

Angalau Farid Mussa alivyorudi nchini kutoka Hispania akajiunga na Yanga. Kwa kiwango fulani, Farid hakurudi nyuma sana japo Yanga hauwezi kuifananisha na klabu aliyokuwa akichezea Hispania. 

Kuna kitu hapa kwetu Tanzania. Watazame Said Kokoo na Ramadhan Wasso ambao ni Warundi. Hawa ‘wamegoma’ kurudi kwao. Wameyapenda maisha ya Tanzania na ya Kitanzania. 

Hawa ni kama wameshakuwa wenzetu tunaopigana nao vikumbo katika shughuli za kuutafuta mkate wetu wa kila siku licha ya wao sasa kuwa katika shughuli nyingine nje ya soka lililowaleta nchini.

Wamestaafu zaidi ya miaka 10 iliyopita, lakini wameweka makazi yao Tanzania. Kwa upande mwingine tujiulize, vipi kuna Mtanzania anaweza kumalizia soka lake nchi nyingine, kisha akafanya maisha mengine huko huko aliko?

Bila shaka wapo. Lakini ni wachache. Yupo Nteze John anayeishi Marekani na mwingine ni Hussein Amani Masha aliyeweka makazi Uingereza.

Vijana wenzangu huu ni mjadala unaohitaji siku maalumu kuujadili. Inawezekana vipi ‘wakuja’ wanakwenda na kurudi Kariakoo, wenzetu wakirudi wanarudia timu za mikoani?

By Jamhuri