Mnyukano Jiji, TARURA

DAR ES SALAAM

NA DENNIS LUAMBANO

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeingia kwenye mvutano mkali wa kimasilahi na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Dar es Salaam kuhusu ukusanyaji wa tozo za maegesho batili (wrong parking) ya magari.

Wakati mvutano huo ukijitokeza, kwa miezi kadhaa sasa halmashauri ya jiji hilo imekuwa ikikusanya fedha hizo kupitia kwa mtu ambaye hakupatikana kisheria, jambo linalotia shaka kuhusu usalama wa makusanyo hayo.

Hata Meya mwenyewe wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto, hakumbuki jina la kampuni inayokusanya fedha hizo. 

Kauli ya meya inaibua hisia kwamba mapato yanayotokana na aina hiyo ya tozo hayaeleweki vema yanaishia kwa nani.

Wakati TARURA wakisema wao ndio wenye jukumu la kukusanya tozo hizo kwa mujibu wa sheria na taratibu za kuanzishwa kwao, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wametangaza zabuni kutafuta kampuni itakayokusanya tozo hizo kwa niaba yake.

Kutangazwa kwa zabuni hiyo kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, kumetokana na kuvuja kwa taarifa kwamba ukusanyaji wa fedha hizo kwa sasa unafanywa bila kuzingatia taratibu za kisheria.

Ili kuhalalisha jambo hilo ndiyo maana kumetangazwa zabuni ambayo mwisho wa kuomba kwake ni Desemba, mwaka huu.

Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Geofrey Mkinga, pamoja na mambo mengine anasema kitendo cha Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kutangaza zabuni hiyo kitaleta mkanganyiko mkubwa kwa wateja, na kinapingana na sheria.

“Mambo ya maegesho ya magari kimsingi ni jukumu letu sisi kwa mujibu wa sheria na kanuni za uanzishwaji wa TARURA na taratibu zake nyingine.

 “Sisi ndio tunashughulika na masuala hayo ya parking za magari, pia kuna mkataba ambao mzabuni wetu anao na moja ya shughuli anazofanya ni kukusanya tozo za wrong parking. Mkataba wetu na yeye unaagiza hivyo.

“Sijafahamu au sijajua hiyo zabuni yao ina uwezo gani, lakini wao na sisi tunafanya kazi kwa pamoja, …hadi sasa eneo hilo la maegesho ya magari tunashughulika nalo sisi,” anasema Mkinga. 

Anasema wanaoshughulikia masuala ya maegesho ya magari yaliyopo ndani ya hifadhi ya barabara ni Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na TARURA na hadi sasa hivyo ndivyo ilivyo kwa taratibu na sheria.

“Sasa kama wao wanataka kufanya itakuwa ni confusion (mkanganyiko), na hiyo kitu italeta mkanganyiko kwa wateja. Hata hivyo, siwezi kusema zaidi kwa sababu sijaiona nyaraka ya zabuni.

“Hadi sasa kuna mkataba wa mzabuni aliyepo anatakiwa kufanya hivyo, pia wapo watu wa jiji wanakusanya na wana maeneo yao, pia wanashughulika na wrong parking.

“Kimsingi wrong parking zilizopo katika maeneo ya maegesho yaliyopo katika hifadhi za barabara yanatakiwa kusimamiwa na TARURA.

“Kuna maeneo ya jiji waliyoyatenga wao kwa mfano ndani ya stendi ya mabasi wanaweza kufanya hivyo, lakini sehemu kubwa ni ya kwetu sisi TARURA,” anasema.

Anasema kuna suala la kiutawala wanaloendelea kuongea na jiji na anatoa mfano wa eneo la Buza ambako kuna watu wanatozwa maegesho batili.

“Suala hilo nalo linaendelea kufanyiwa kazi. Kuna mwingiliano kidogo upo tunaufanyia kazi ila sasa kama kuna watu wamefikia hatua ya kutangaza zabuni kabisa hapo ndipo sifahamu, kwa sababu sina takwimu na siwezi kulisemea zaidi jambo ambalo sina takwimu zake.

“Unachotakiwa kufahamu ni kwamba kuna mkataba wa mzabuni anasimamia wrong parking, sasa hao kama wametangaza zabuni ujue kwamba kuna mgogoro hapo, kwa kweli itakuwa shida, japo sina uhakika itakuwaje hiyo shida, sina uhakika.

“Mnachotakiwa kujua kutoka kwangu ni kwamba TARURA anasimamia hilo suala la maegesho batili na kuna mzabuni ambaye yupo anasimamia sheria hizo, ila hilo jingine siwezi kulisema kwa sababu sijaliona na halijaja mezani kwangu,” anasema Mkinga.

Ofisa Habari wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Tabu Shaibu, ameulizwa na JAMHURI ili kupata ufafanuzi wa mgongano huo, lakini akasema yupo safarini na hawezi kulizungumzia.

“Niko Dodoma kuna activities (kazi) ninafanya huku, kwa hiyo siwezi kulizungumzia suala hilo,” amesema Tabu.

Meya Kumbilamoto ameliambia JAMHURI kuwa tozo wanazokusanya wao ni za maegesho batili ya magari wakati TARURA wanakusanya za maegesho ya magari.

“Kuna tozo za maegesho, pia kuna tozo za wrong parking, hivyo ni vitu viwili tofauti; zile za maegesho ni TARURA, ila zile za mtu aliye-park vibaya gari lake ndizo za jiji, kwa hiyo ni vitu viwili tofauti.

“Kuna kampuni zamani ilikuwa inafanya kazi hiyo na walipewa zabuni hiyo kwa muda, ina maana sasa hivi kwa utaratibu wa serikali tunaanza kutangaza, anapatikana mtu ambaye anakaa kwa mwaka mmoja, ndio utaratibu wa sasa hivi,” anasema Kumbilamoto.

Hakumbuki jina la kampuni inayokusanya fedha hizo, lakini anakiri kuwa ilipewa ukusanyaji wa  tozo hizo kwa kipindi kifupi, kwani kulikuwa na ucheleweshwaji wa makabidhiano ya ofisi kutoka lililokuwa jiji la zamani baada ya kuvunjwa Februari 24, mwaka huu na kuja jiji jipya lililotokana na kupandishwa hadhi kwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.

“Mwaka wa fedha tu wa kiserikali unapogeuka basi, sasa kipindi hicho cha huyo mzabuni aliyepewa kwa sababu mambo ya kukabidhiana kutoka jiji la zamani yalikuwa hayajakamilika,” anasema Kumbilamoto na kuongeza:

“Ndiyo maana tukamtafuta kwa muda, kwa hiyo keshamaliza ndiyo maana tukaamua kutangaza.

“Alipewa mkataba wa muda labda kwa miezi mitatu kisha anapatikana mtu kwa mwaka mmoja, basi. Jina kidogo la mzabuni aliyepewa kazi hiyo kwa muda limenitoka,” anasema.

Wakati mgongano huo wa kimasilahi ukiibuka, wiki iliyopita JAMHURI liliripoti jinsi vigogo watano wa jiji hilo walivyosimamishwa kazi kupisha uchunguzi maalumu wa tuhuma za ufisadi wa mamilioni ya shilingi.

Uchunguzi huo unafanywa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kubaini upotevu wa fedha za mapato yanayokusanywa kupitia mashine za POS.

Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jumanne Shauri, amethibitisha kuwapo kwa ukaguzi huo.

“Ni kweli kuna ukaguzi ila wanaochunguza si TAMISEMI, ni CAG na hadi sasa hivi hakuna kiasi cha fedha kilichotajwa kupotea,” anasema Shauri.

Anasema tuhuma zilizopo si za wizi, bali ni kutaka kujua kwanini makusanyo yamegota asilimia 26. Shauri hakutaka taarifa hizo za ukaguzi zichapishwe kwenye vyombo vya habari.

“Kwa kuwa kuna ukaguzi ndiyo maana hao watumishi wa jiji ikabidi wasimamishwe ili uchunguzi ufanyike, kwa sababu isingewezekana wao wabaki ofisini wakati uchunguzi unaendelea.

“Ukaguzi ukishamalizika watarudi ofisini kuendelea na majukumu yao. Tumwache CAG afanye kazi yake na hata akimaliza ukaguzi huo ataandika ripoti yake ambayo itapatikana kuanzia mwakani, hebu tusubiri kwanza,” anasema.

Taarifa za kusimamishwa kwa watumishi hao zimekuwa zikifichwa zisivifikie vyombo vya habari.

Pia kuna taarifa zisizo na shaka kuwa baadhi ya watumishi wa Ofisi ya CAG wamekuwa wakikutana na kila aina ya vishawishi ili kufukia baadhi ya taarifa. 

Hata hivyo JAMHURI limethibitishiwa kuwa uongozi wa juu wa Ofisi ya CAG umesimama kidete kuhakikisha kazi hiyo inafanywa kwa kiwango kilichotukuka.