Benki yazidisha uonevu kwa wafanyakazi

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Baada ya gazeti hili la uchunguzi kuchapisha taarifa za benki moja nchini zinazoeleza kuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo ana dharau, ananyanyasa na kufukuza wafanyakazi hovyo bila kuheshimu sheria za kazi wiki mbili zilizopita, mambo makubwa yameibuka.

Katika habari iliyopita tulichapisha taarifa za mwakilishi wa benki hiyo Zanzibar kufukuzwa kazi kwa “kosa la kupata kazi Benki ya CRDB” baada ya benki hiyo kukataa kumwongezea mshahara. 

Pia tuliorodhesha baadhi ya kesi ambazo tayari wafanyakazi waliofukuzwa kwa uonevu wamefungua kwenye Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), ambapo baadhi wanadai fidia ya hadi Sh milioni 550 kila mtu.

JAMHURI sasa limepata taarifa kuwa kwa kiburi kile kile na kwa ushauri wa wapambe wake, wamewafukuza watu tisa kati ya 25, miongoni mwa wafanyakazi wa Tawi la Kariakoo kwa kosa lililofanywa na wakurugenzi waliomzunguka. Hali kama hiyo imetokea Tawi la Mbeya, Mwanza na moja ya wilaya za Shinyanga.

“Sisi ametufukuzwa kazi kwa uonevu wa hali ya juu. Anasema katika kipindi cha corona tumetoa mikopo kwa wafanyabiashara na mikopo hiyo imeshindikana kulipwa. Hiki ni kichekesho cha mwaka na ndicho kimetufanya twende mahakamani. Mikopo aliyotufukuzia  hatukuiidhinisha sisi.

“Benki ina utaratibu kuwa mkopo wowote unaoanzia Sh milioni 200 unaidhinishwa na wakurugenzi makao makuu. Sisi hapa Kariakoo unafahamu biashara ziliyumba sana wakati wa corona na maduka mengi yakafungwa. Hata wengi waliokuwa wanakwenda China wanaleta mizigo, mipaka ya nchi hiyo ilifungwa.

“Wengi kati ya hawa walikuwa na mikopo ya Sh milioni 200 na zaidi. Wakurugenzi makao makuu ndio walioidhinisha hii mikopo, sasa inakuwaje tufukuzwe sisi kwa kosa lililofanywa na wakurugenzi wa makao makuu? 

“Lakini pia Benki Kuu imekwisha kuelekeza kuwa mikopo iliyokuwa na shida katika kipindi cha corona, waingie makubaliano ya kulipa kwa masharti nafuu. Sasa tunajiuliza, kama BoT imebaini tatizo lilitokana na corona, sisi tunaangukia wapi tuliofukuzwa kwa kosa lisilo la kwetu?” amehoji mmoja wa wafanyakazi wa benki hiyo mwenye kesi CMA.

Mfanyakazi mwinigne wa benki hii iliyojipanga kunyanyasa wafanyakazi aliyeko Mbeya, naye wamemfukuza kazi na kutia dosari mafao yake. 

Walimtuhumu kutoa mikopo kwa njia ya rushwa, ila baadaye wakabaini si yeye aliyehusika na wakakiri kosa mahakamani. Mahakama ikaamuru arejeshwe kazini, lakini hadi leo hawajamrejesha kazini.

“Baadaye walisema wananilipa mafao tuhitimishe mkataba wa kazi. Ajabu, walichukua fedha za mafao yangu wakaziingiza kwenye akaunti, kisha wakazichukua zote kuwa wamekata mkopo, ilhali hayo hayakuwahi kuwa sehemu ya makubaliano yetu. Wana jeuri kubwa sana watu hawa. Wanatamba wanasema niende popote nitakapo, hawana hofu,” amesema mfanyakazi huyo.

Mfanyakazi mwingine wa benki hiyo katika Wilaya ya Kahama na watatu wa Mwanza, wameliambia JAMHURI kuwa wamefukuzwa kazi katika mazingira ya kutatanisha. 

“Tatizo si sheria wala nini, ni uwezo wa mtendaji mkuu. Ukishauriwa na wasaidizi wako, hutekelezi kama roboti. Unapoona wasaidizi wanakimbilia kubeba mikoba yako, wakakuuliza utakula nini mchana badala ya kuacha kazi hiyo kwa mhudumu wa ofisi, basi ujue kuna tatizo kubwa.

“Hapo ndipo alipoifikisha benki yetu. Baadhi ya wakurugenzi wanafanya kazi za umesenja. Wanajichekesha chekesha ofisini kama mazuzu. Ila hawa si wajinga, maana kujichekesha kwao kunawanufaisha wao na ndugu zao… tunaomba serikali iingilie kati utendaji wa benki hii ifuate misingi ya sheria. Basi. Sisi hatuhitaji kupendelewa au kujichekesha mbele ya mtendaji mkuu ndipo tusipoteze kazi.

“Tumeajiriwa kwa uwezo wetu, si kwa uwezo wa kujichekesha na kujikomba. Tupimwe kwa utendaji wetu na si kwa majungu kutoka kwa wasaidizi wetu aliowapandikiza. Hapa Mwanza ana watu wake. Hata ukienda chooni, wanataka kuchungulia kama unazungumza na simu au la, alimradi wapate neno la kumpelekea. Hawa chawa wake tumewachoka. Watu wakisikia hizi aibu watajuta kutupa fursa ya kuongoza benki kubwa kama hii,” kinasema chanzo chetu.

JAMHURI limepata taarifa kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tayari inalifuatilia kwa karibu suala hili, hasa lile la Mzanzibari aliyefukuzwa kazi kwa kuomba kazi CRDB. 

“Angekuwa ni mwizi, wasingembembeleza kumwongezea mshahara. Ni ujinga tu uliowasukuma kumfukuza. Wamepata aibu kubwa. Walifikiri mambo haya yangeishia chini kwa chini, ila tunawashukuru Gazeti la JAMHURI kwa kuliweka wazi hili. Anika na mengine, benki iwe safi,” amesema ofisa mmoja wa benki hiyo kutoka Mwanza.

Mbunge mmoja baada ya kusoma habari iliyopita alilipigia simu JAMHURI na kusema: “Tatizo si kwa wafanyakazi tu, bali hata kwa wateja. Hii benki iliahidi bilioni [kiasi kinahifadhiwa] kwa ajili ya kukopesha wakulima wadogo. Ulizia kama kuna mkulima aliyezipata. Inasemekana kwa vile hazina riba kubwa, zote zimeishia kwenye mikono ya wafanyabiashara wakubwa. Mtendaji Mkuu yupo anauza sura kwa wakubwa. Uliza wawambie ziko wapi hizo hela?”