China Yapuuza Vikwazo vya UN

Rais wa Marekani Donald Trump ameilaumu nchi ya China kwa kukiuka vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini kwa kuzipa matuta meli za nchi hiyo.

Rais Trump aliandika katika ukurasa wake wa twitter kuwa China imeshuhudiwa ikiruhusu mafuta kusafirishwa kwenda Korea Kaskazini na kusema amekatishwa tamaa na kitendo cha nchi hiyo kukiuka maazimio ya UN.

Rais huyo ambaye mara kadhaa amekuwa akisifu juhudi za China katika kuweka mbinyo dhidi ya Korea Kaskazini hakugusia hatua za kutumia nguvu za kijeshi kutatua mzozo huo unaoendelea kushika kasi.

China ambayo ni mshirika muhimu wa kibiashara na Korea Kaskazini wiki iliyopita ilisifiwa na Rais Trump kwa msaada wake katika juhudi zinazoongozwa na Marekani dhidi ya Korea Kaskazini.

Gazeti moja la Korea Kusini likiwanukuu maofisa kadhaa wa nchi hiyo wakisema kuwa setelaiti za Marekani zilishuhudia meli za China zikihamishia mafuta katika meli za Korea Kaskazini katika eneo la bahari upande wa China.

Habari hiyo pia iliandikwa na vyombo vya habari vya Marekani pamoja na Shirika la Habari la Fox ambalo liliripoti kuwepo kwa tukio hilo lililotekelezwa na Serikali ya China huku ikifahamu kuwa inakiuka maazimio ya UN.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema kuwa nchi hiyo inataarifa kuwa baadhi ya meli zimekuwa zikihusika na shughuli zilizopigwa marufuku na UN dhidi ya Korea Kaskazini ikiwa ni pamoja na usafirishaji wa shehena ya mafuta.

Ofisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amesema wanaushahidi kuwa baadhi ya meli zinazohusika na usafirishaji wa mafuta zinamilikiwa na kampuni za nchi kadhaa ikiwemo China.

Marekani imesema inalaani kitendo hicho na kuwa ina tumaini kuwa nchi yeyote mwanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiwemo China itatoa ushirikiano wa karibu kuzuia usafirishaji wa aina hiyo.

China yakanusha taarifa hizo

Wizara ya Mambo ya Nje ya China kupitia kwa msemaji wake imesema inatekeleza ipasavyo vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini na kuongeza kuwa haina taarifa za hivi karibuni meli zake kuhusishwa na tukio hilo.

Usafirishaji wa bidhaa kwa njia ya meli unaoihusisha Korea Kaskazini ni suala lililozuiwa kupitia vikwazo vilivyotangazwa na Umoja wa Mataifa Septemba 11 pamoja  na vikwazo vilivyotangazwa  hivi karibuni.

Mwezi uliopita Idara ya Fedha ya Marekani ilitangaza vikwazo dhidi ya kampuni sita za Korea Kaskazini pamoja na meli 20, na Oktoba 19 mwaka huu ilichapisha picha ilizodai ni meli za Korea Kaskazini zikihamisha  mafuta ili kukwepa vikwazo dhidi yake.