Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umeua raia 109 katika mashambulizi tofauti ya ndege katika kipindi cha siku 10, wakiwemo watu 14  wa familia moja na kuacha simanzi kubwa katika familia hiyo.

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Jamie McGoldrick amesema mapigano yanayoendelea nchini humo ni ya hatari na kuhuzunisha kiasi cha kuhitaji msaada kutoka jumuiya za kimataifa.

Amesema watu wengi wakiwemo wanawake na watoto wamekuwa ni wahanga wakubwa wanaopoteza maisha tangu vita hivyo vilipoanza miaka zaidi ya mitano iliyopita huku jumuiya za kimataifa zikiwa kimya.

Kuna haja ya jumuiya za kimataifa kuhakikisha vita hivi vinamalizika ili kuweza kukiokoa kizazi hiki cha wazee, wanawake na watoto kinachoendelea kuteketea bila ya msaada wowote unaohitajika,” amesema MacGoldrick.

Amesema mashambulizi yanayofanywa na ndege nchini humo yamekuwa yakilenga maeneo ya soko lenye watu wengi katika Wilaya ndogo ya Al Hayma katika Mkoa wa Taiz na kuua watu wengi kila kukicha.

Siku za karibuni tumeshuhudia shambulizi la ndege kwenye shamba lililopo Wilaya ya Attohayta katika Mkoa wa Hodeidah na kusababisha vifo vya watu 14, na mashambulizi ya ndege kwingineko yakaua raia wengine 41 na kuwajeruhi 43,” amesema McGoldrick.

Umoja wa Mataifa umesema mgogoro wa Yemen ni miongoni mwa migogoro mibaya zaidi na uliojaa ukiukaji wa kibinadamu ambapo watu wapatao milioni nane wako katika hatari kubwa ya kukumbwa na janga la njaa.

Mgogoro wa Yemen ulianza kushika kasi kuanzia Machi 2015 wakati waasi wa Kihouthi waliposonga mbele kuelekea mji mkuu wa muda wa Serikali wa Aden, na kuilazimu Saudi Arabia pamoja na mataifa washirika ya Kisunni kuanzisha mashambulizi ya ndege dhidi ya kundi hilo la Kishia.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (UNICEF), takribani watoto milioni 2.4 wa Yemen walio chini ya umri wa miaka 15 wanakabiliwa na hatari ya maradhi kama vile rubella na polio.

Kwa mujibu wa Muungano wa Kiraia Yemen, hadi sasa Wayemen wasiopungua 6,091 wameuawa Yemen kutokea Saudia, ianzishe hujuma zake dhidi ya nchi hiyo Machi 26, mwaka huu na wengine zaidi ya 13, 552 wamejeruhiwa.

3718 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!