Kwenye vitabu vya dini tumezuiwa kujisifu, lakini hatukatazwi kutangaza mafanikio. Ndiyo maana nakiri kuwa miongoni mwa wadau tuliosimama imara kuhakikisha tunaondoa ukiritimba wa Chama cha Wamiliki wa Kampuni za Uwindaji wa Kitalii Tanzania (TAHOA), kutoka kwenye mizengwe ili kiwe na manufaa kwa Watanzania na kwa Taifa letu kwa jumla.

Kuna wakati mwekezaji mmoja raia wa kigeni alikuwa akimiliki vitalu ambavyo – kwa kuviweka pamoja – ukubwa wake ulikuwa sawa na nchi ya Djibouti. Hilo tulilipinga kwa nguvu zote.

Mchuano huo wa haki uliwezesha, pamoja na mambo mengine, kutungwa kwa Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 pamoja na kanuni zake za mwaka 2010. Sheria hii ndiyo iliyowezesha wazawa kumiliki asilimia 85 ya vitalu vyote, ilhali wageni wakiachiwa asilimia 15.

Jambo ambalo hatukulizingatia, na pengine ndilo kosa letu, hatukuheshimu ukweli kuwa uwindaji wa kitalii ni biashara ngumu yenye mtandao mzito wenye kuhitaji mtaji wa kutosha. Kutojali hilo kumesababisha tasnia hii ionekane kama sera ya upokwaji mashamba ya Wazungu kule Zimbabwe. Weusi wameshindwa kuyaongoza. Hatuwezi kushindwa kuendesha vitalu, lakini tunapaswa kuwa na uongozi unaotabirika kwa kuheshimu sheria na kanuni.

Nimeyasema haya mapema ili kuwasaidia wasomaji kujua kuwa tunapopambana na mambo haya huwa tunafanya hivyo kwa nia njema ya kulisaidia Taifa letu na watu wetu. Mimi ni kati ya wale wanaoamini kuwa kila Mtanzania ana mchango wake katika ujenzi wa Taifa letu.

Pamoja na ukweli huo, kuifia nchi hakumaanishi kuwa pale baadhi ya mambo yanapofanywa sivyo, tunyamaze. Hapa nailenga Wizara ya Maliasili na Utalii.

Oktoba 23, mwaka jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, akiwa mjini Dodoma, alitangaza uamuzi mgumu. Nilikuwapo. Alitangaza kufuta umiliki wa vitalu vyote vya uwindaji wa kitalii vilivyotolewa Januari 16, mwaka jana na aliyekuwa mtangulizi wake, Profesa Jumanne Maghembe. Umiliki huo ulikuwa wa miaka mitano – kama ilivyo kisheria – na ungeanza Januari hii hadi Desemba 31, 2022.

Alichukua uamuzi huo kwa kile alichosema ni kupisha mfumo mpya wa ugawaji vitalu kwa njia ya mnada!

Desemba 28, mwaka jana, Waziri Kigwangalla alikutana na wadau mbalimbali wakiwamo TAHOA, Chama cha Wawindaji Bingwa Tanzania (TPHA) na Shirikisho la Vyama vya Utalii Tanzania (TCT). Lengo likawa ‘kusikiliza’ maoni yao. Hitimisho la waziri likawa kuwapa miaka miwili kuanzia Januari, mwaka huu hadi Desemba 2019 kwa kampuni 47 ambazo zilipata barua ya kuendelea na umiliki (barua za Januari 2017).

Waziri akaamua kuwa mnada kwa ajili ya vitalu 61 vya uwindaji ambavyo vimerudishwa na waliokuwa navyo utafanyika Julai, mwaka huu. Baada ya hapo mnada utafuatiwa na mwingine kwa vile alivyotangaza kuwapoka Desemba 2019. Huu ndiyo msimamo wa waziri na kwa maana hiyo tunaweza kusema ndiyo msimamo wa Serikali.

Kwanza nimpongeze Waziri Kigwangalla kwa sababu walau ameanza kuonyesha usikivu. Spidi aliyoanza nayo mwanzo ilileta shaka. Nilimwomba apate muda kidogo wa kuijua wizara. Nayaona matumaini.

Kwanza, kabla sijaingia kwenye hoja yenyewe, nimweleze Waziri Kigwangalla kuwa naunga mkono uamuzi wa Serikali wa kuongeza mapato. Tulipopambana kupata sheria na kanuni mpya hilo ndilo lililokuwa lengo letu la pili kwa umuhimu baada ya lengo la kwanza ambalo ni uhifadhi. Kuhifadhi tu bila kutumia vilivyohifadhiwa kuinufaisha jamii ni kazi bure. Kwa hiyo, kama ni suala la kuongeza mapato, hapo hakuna shaka. Swali linakuja, hayo mapato yaongezeke kwa njia ipi? Waziri au wizara wameona njia nzuri ni kupiga mnada vitalu vya uwindaji wa kitalii. Hapa lazima kuwe na angalizo. Sharti tusimame kwanza kwenye dhima ya kwanza ambayo ni uhifadhi kabla ya kuelemea kwenye mapato.

Mimi si mwanasheria, lakini mtazamo wa kawaida unanisukuma nione kuna dosari kwenye uamuzi huu mpya unaokusudiwa kuanza mwaka 2019. Dosari inayoonekana sasa ni ya namna uamuzi wa waziri unavyoweza kuwasumbua wamiliki wa vitalu. Hizo nyingine sitaki kuwa mtabiri ingawa kwenye minada tujiandae kuona vitalu vikiwa vya Wamarekani, Wachina na Waarabu. Kwa ufupi, sioni Mtanzania wa kujipima ubavu. Kwa maneno mengine kifo cha wawekezaji Watanzania kwenye tasnia hii kimewadia. Basi waandaliwe kifo cha kiungwana kisichokuwa cha maumivu.

Ukiacha kuongeza mapato kama sababu kuu ya Waziri Kigwangalla kuwapoka vitalu hawa wawekezaji 41, sababu yake nyingine ni kuwa ugawaji uliofanywa na mtangulizi wake ulikuwa kinyume cha sheria. Anasema hapakuwapo Kamati ya Ushauri wa Ugawaji Vitalu ambayo kisheria inaundwa na waziri. Sijui hilo lina uzito namna gani! Lakini kwa maneno yake ni kuwa ugawaji vitalu uligubikwa na vitendo vya rushwa na upendeleo. Kwa hii sheria ya mwaka 2009 sijui, lakini huko nyuma kauli hii ilikuwa sahihi asilimia 100.

Kama kuna makosa yamefanywa kwenye ugawaji huu wa mwaka 2018-2022 waliokosea ni wizara yenyewe. Ofisi hiyo hiyo. Kiti hicho hicho. Serikali hii hii. Kama kweli yapo makosa waliostahili adhabu si hao waliopewa vitalu, bali walioshiriki kuyatenda.

Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 kifungu 38(12) inampa waziri mamlaka ya kumfutia mwekezaji umiliki wa kitalu. Kwa kimombo, inasema:

a) The person to whom the hunting block was allocated has failed to satisfy any or a combination of matters required by the Minister;

b) Has given false or incorrect information on the application for a hunting block;

c) Has been convicted of an offence under the Act;

d) Has failed to pay the necessary fees or any other debt due to him in relation to his hunting block; and

e) Has sublet a hunting block allocated to him without the consent of the Minister.

Sheria hiyo hiyo, kifungu 38 (13) inasema hakuna kumnyang’anya mtu kitalu isipokuwa hadi awe amepewa fursa ya kusikilizwa. Hawa wenye vitalu hawakusikilizwa. Wameambiwa kupitia redio, televisheni na magazeti. Juzi Dodoma hawakusikilizwa, bali waliitwa kupewa ‘msimamo’.

Kama nilivyosema awali, sipingi utaratibu wa mnada, lakini ni vizuri utaratibu huo ukazingatia sheria, haki; na zaidi ya yote busara. Sheria inaweza kumpa waziri nguvu ya kufanya alivyofanya, lakini busara inaelekeza suala kama hili lingepaswa kufanywa kwa kuwapa notisi wawekezaji hawa. Notisi hiyo isingekuwa vinginevyo, isipokuwa kuwaeleza kwa barua kwamba baada ya Desemba 31, 2022 hakuna kitalu kitakachotolewa kwa utaratibu wa sasa, isipokuwa kwa mnada. Muda huo ungekuwa sahihi ili kwanza Serikali na wadau waketi na kutoa mapendekezo ya sheria mpya. Tunaweza kuwa na sheria mwaka 2019 kama alivyosema waziri, lakini hizi ni aina ya sheria ambazo kila mwezi zitakuwa zikihitaji ‘amendments’.

Pili, muda huo ungewafaa hawa waliopewa vitalu hivi kisheria, kurejesha mitaji na nguvu kubwa waliyotumia kuwekeza. Pengine si vibaya kwa viongozi wetu wakawa wanapata fursa ya kuzuru maeneo ya kambi walizowekeza watu hawa ili kujionea hali halisi.

Biashara ya uwindaji wa kitalii si kama biashara ambayo unaweza kusimama barabarani ukampata mteja. Ni biashara inayohitaji fedha na muda wa kutosha. Kwa mtifuano uliopo sasa, ni wazi kuwa hakuna wageni wawindaji watakaopatikana kupitia mikutano ya kuuza safari inayoanza mwezi huu Marekani na Ulaya.

Tatu, ufike wakati, kama nchi, tuwe na mambo yanayotabirika. Tangu mwaka 2005 Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa na mawaziri kenda na makatibu wakuu nadhani saba au wanane. Tukiacha mambo yafanywe kadiri ya utashi wa wanaoingia kuongoza wizara, tutakuwa tunafanya makosa makubwa. Hilo lingekuwa na utetezi kama Serikali zingekuwa zinabadilika kadiri ya vyama tofauti vya siasa, lakini kwa Serikali ya chama hicho hicho, Serikali yenye sera ile ile ya kuwavutia wawekezaji na wananchi kufaidika na rasilimali za nchi yao, si busara kuwapo mparaganyiko huu. Hii inatoa picha mbaya kuwa kwa Tanzania kuwa utashi wa waziri anayeshika madaraka ndiyo mwongozo; na si sheria au kanuni.

Nne, tuachane na dhana kuwa kila mwekezaji ni mwizi. Kweli wizi kwenye tasnia hii ulikuwapo, lakini umedhibitiwa kwa kiwango kikubwa mno kwa sheria na kanuni mpya. Tufungue macho na masikio kujua kwa majirani zetu shughuli hizi za uwindaji wa kitalii zinafanywaje na kwa gharama gani ili tushike njia sahihi.

Tano, kama tunaona uwindaji wa kitalii hauna tija, ni heri ukafungwa kama ilivyowahi kutokea wakati fulani. Lakini ni muhimu tukajua uwindaji ni sehemu ya uhifadhi, ndiyo maana zamani zile kulikuwa na maduka ya nyamapori. Msimu wa uwindaji ulipofika kuna aina ya wanyamapori waliuawa, wananchi wakapata kitoweo. Hayo yalifanywa kwa sababu kuacha aina fulani ya wanyama ikazidi katika eneo moja kuna athari kiikolojia. Mfano, simba wakizidi eneo fulani maana yake wanyamapori wengine watapungua kwa kuliwa. Uwindaji ukifanywa kwa tija si kosa. Ni uhifadhi. Ni manufaa kwa jamii.

Sita, kama nilivyosema, hawa watu wamewekeza fedha nyingi. Wamekuwa wakishiriki kutengeneza miundombinu kwenye mapori na wametumia fedha, nguvu na wakati mwingine wamepoteza uhai wakipambana na majangili. Tutajidanganya kuamini kuwa TAWA na TANAPA pekee wanashinda vita ya ujangili bila wadau wengine. Tunapoelekea kwenye minada hatuna budi kuhakikisha kuwa vita dhidi ya ujangili ni jambo la kufa au kupona.

Mwisho, kwa kuwa waziri alianza kwa kutangaza kuwa Januari hii ndiyo mwisho, baadaye akatoa mwaka mmoja, lakini mwishowe akahitimisha kwa kuwapa wawekezaji hawa miaka miwili, naamini busara hiyo hiyo anaweza kuitumia kuwaongeza muda ili kusiwepo malalamiko kuwa wameonewa.

Hii miaka miwili aliyowapa haipo kisheria. Kama hivyo ndivyo, basi awape muda wa kutosha ili waliokopa benki waweze kurejesha mikopo na wale waliowekeza miuondombinu wajiandae kuiondoa.

Kama ni suala la kuongeza mapato, waziri awabane kwa kuwataka, kwa mfano waliokuwa wakilipa dola 60,000 kwa kitalu cha daraja la kwanza, sasa walipe dola 120,000 hadi ifikapo mwaka 2022 watakapoondoka kisheria. Uamuzi wa aina hiyo utashabihiana na mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano ya kuongeza mapato.  

Nimeyasema haya kama ushauri kwa waziri na wasaidizi wake, na pia kwa kutambua kuwa wengi kwenye tasnia hii ni Watanzania ambao sheria ya mwaka 2009 iliwapa moyo hata wakakubali kushiriki kuujenga uchumi wao na wa Taifa lao kupitia tasnia hii.

By Jamhuri