Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Dk.Hamza Kondo amesimamishwa kazi ya uhadhiri katika mazingira ambayo ameyataja kujaa utata na ukiukwaji wa taratibu za utumishi.

Akizungumza na JAMHURI, Dk. Kondo ambaye amekuwa mhadhiri katika kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii, Idara ya Uandishi wa Habari kwa miaka kadhaa, katika kipindi amefanya kazi kama mkuu wa idara hiyo.

Mhadhiri huyo anasema, kusitishwa kwa kandarasi yake ya kufundisha elimu ya juu, kumegubikwa na kile anachokiita mvutano uliopo baina yake na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Elifas Bisanda.

“Amekuwa na ‘bifu’ ya miaka mingi tangu mwaka 2014 nilipomshtaki kwenye kamati ya nidhamu na badaye kumsamehe kumbe aliweka kisasi…tangu kipindi hicho amekuwa akinidhalilisha kupitia mitandao ya kijamii,” anasema Dk. Kondo.

Anasema sababu iliyotumika kusitisha kandarasi yake ya kufundisha ni kitendo cha yeye kukaidi kurudisha mkopo wa Shilingi milioni 43 aliouchukua Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kwa ajili ya masomo yake ya shahada ya uzamivu katiya mwaka 2010 hadi 2014.

 

Akizungumza na JAMHURI, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria, Prof Elifas Bisanda anasema, binafsi hana ugomvi wowote na Dk. Kondo. Anasema yeye ndiye aliyemwajiri hivyo hawezi kuwa na ugomvi wowote naye.

“Ninashindwa kutoa ufafanuzi wa jambo hili, maana kwanza kuna shauri liko Mahakamani…yeye ametufungulia kesi mbili, na Jamhuri imemfungulia kesi moja ambayo siwezi kuielezea kwa undani sana.

“Shauri hili liko Mahakamani, hata ukiandika litakugeukia, kuna kesi tatu, mbili katufungulia yeye na moja amefunguliwa na Jamhuri, kwa hiyo kama gazeti lako litaandika jambo lolote kuhusu taasisi yetu tutakushtaki na utatulipa fidia,” anasema Prof Bisanda

Hata hivyo, katika moja ya vielelezo ambayo JAMHURI limeviona, Mwezi Februari, mwaka huu, Prof Bisanda alimwandikia barua Dk. Kondo akimtuhumu na mambo kadhaa, huku akisema asilazimishwe kutoa masuala ya kimaadili yanayomhusu mhadhiri huyo.

“Nimeamua kuchagua kujikita kwenye jambo moja la wewe kukataa kulipa mkopo wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, tafadhari usinilazimishe kuzungumzia masuala mengine yanayohusu mwenendo wako kimaadili. Idara ya usalama wa taifa inafahamu kuhusu mapungufu yako…Hata Dk. Magufuli alilipa ada ya shahada yake ya uzamivu, kwa taarifa yako nilikuwa mtahini wake wa nje,” inasomeka sehemu ya barua hiyo.

Wachambuzi wa masuala ya sheria hata hivyo wanahoji, utaratibu huo mpya aliouanzisha Katibu Mkuu wa Utumishi Dk. Lauren Ndumbaro wa kuachisha kazi watumishi kwa maagizo ya siri bila ya kuzingatia sheria za utumishi wa umma.

Katika kiapo chake cha utumishi wa umma, kifungu cha 8 kinasema, “Nitatekeleza wajibu wangu kwa kufuata sera, sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya utumishi wa uuma.”

3707 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!