Pamoja na migongano ya wataalamu wa lugha juu ya fasili ya neno familia, kiujumla familia ni kundi la watu wanaokaa pamoja kama babamama na watoto

Kikundi hiki mara nyingi ni sehemu ya kundi kubwa zaidi la ukoo unaounganisha watu wenye asili katika uzazi wa pamoja. 

Familia zinatofautiana duniani kutokana na utamaduni na hali ya jamii. Katika nchi nyingi za Afrika familia ndogo ya baba, mama na watoto (Nuclear Family), ni sehemu tu ya familia kubwa zaidi (Extended Family) pamoja na ndugu wa baba na mama, akina babu na bibi na kadhalika.

Katika hali ya kawaida, familia inahusika zaidi katika malezi ya mtoto, na kwa hakika ina mchango mkubwa sana katika mchakato wa kumfanya mtoto kuwa mwanajamii bora na kinyume chake. 

Kwa kuwa mtoto anajifunza na kuyaiga yale yaliyomzunguka katika familia yake na jamii kwa ujumla, mpango wa ulezi unaofuatwa na familia huwa ndio mwongozo wa namna mtoto atakavyokuwa na kujengeka kitabia. Chambilecho: “Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.”

Mtihani mkubwa unaozikumba familia nyingi hivi sasa ni kukosa mwongozo wa malezi, hivyo watoto hulelewa kwa kufuata mazingira yanayoizunguka familia husika. 

Zipo familia ambazo watoto ndio wanaoamua nini wafanye na wazazi katika kinachoonekana kuwaridhisha watoto wao huwaachia wafanye yanayowapendeza. 

La hatari zaidi linalodhihirika kwa familia nyingi ni kutothamini mafunzo na maadili ya dini. Ushahidi wa wazi ni watoto wetu wengi kuathiriwa na utamaduni wa Kimagharibi katika kuvaa kwao, mitindo ya nywele na kuyafanya mengi yaliyo kinyume cha mafunzo na maadili ya dini.

Idili ya makala yetu leo ni kumzindua Muislamu kuwa baada ya kujitathmini yeye mwenyewe ni kwa kiwango gani yeye ni Muislamu, aitupie jicho familia yake na kuitathmini ni kwa kiwango gani imekuwa ni familia ya Kiislamu yenye kutekeleza kwa kauli na vitendo yale yanayoamrishwa na Uislamu na kuyaacha, kwa maana ya kuyaacha, yale yanayokatazwa na Uislamu. 

Kwa nini afanye hivyo? Kwa sababu yeye ni mchungaji atajayeulizwa na Mola wake Siku ya Kiyama juu ya wale aliopewa dhamana ya kuwachunga.

Tunasoma katika Hadithi iliyopokewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (Allaah Amridhie) kwamba Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amesema: “Nyinyi nyote ni wachunga na kila mmoja wenu ataulizwa kuhusu alichokichunga. Kiongozi ni mchunga, na mume ni mchunga juu ya mkewe na mke ni mchunga juu ya nyumba ya mumewe na watoto wake. Kwa hivyo nyote ni wachunga na kila mmoja wenu ataulizwa kuhusu alichokichunga.” (Hadithi hii inapatikana katika Vitabu vya Hadithi za Mtume, Sahih Al-Bukhary na Sahih Muslim).

Katika kusisitiza juu ya utekelezaji wa jukumu hili adhimu tunasoma katika Qur’aan aya mbili; moja ikisisitiza umuhimu wa mtu kuinusuru familia yake na adhabu ya moto aliouandaa Mwenyeezi Mungu kwa watu waovu, na nyingine ikionyesha umuhimu wa kuiongoza familia kutekeleza maamrisho ya Mwenyeezi Mungu ili ipate radhi zake na Siku ya Kiyama inusurike na Moto na izawadiwe Pepo.

Tunasoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 66 (Surat At-Tahriim) Aya ya 6 kuwa: “Enyi mlio amini! Ziokoeni nafsi zenu na ahali (familia) zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi Mwenyezi Mungu kwa anayowaamrisha na wanatenda wanayoamrishwa.”

Tunaona hapa jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa anajiokoa yeye mwenyewe na kuiokoa familia yake na adhabu ya Moto wa Mwenyeezi Mungu. 

Tunasoma pia katika Qur’aan Tukufu Sura ya 20 (Surat Twaa-Haa) Aya ya 132 kuwa: “Na waamrishe watu wako kuswali, na uendelee mwenyewe kwa hayo. Sisi hatukuombi wewe riziki, bali sisi ndio tunakuruzuku. Na mwisho mwema ni kwa mcha-Mungu.”

Hapa tunaona msisitizo kwa familia kutekeleza Ibada ya Swala ambayo ni Ibada kubwa sana ambayo hakuna udhuru wa kutoitekeleza isipokuwa kwa kupitiwa na usingizi au kusahau, kwa maana ya kusahau, na si kujisahaulisha au kupuuza utekelezaji wake ndani ya wakati. 

Ni ibada yenye nyakati maalumu ambayo hata mgonjwa hana udhuru wa kuiacha muda wa kuwa ana akili timamu; anatakiwa aitekeleze kwa hali yoyote awezavyo; kwa kusimama, kukaa, kulala kwa ubavu wa kulia; kwa kuleta nguzo za Swala kwa vitendo au hata kuvileta kwa kuashiria au kuvileta mawazoni, ili mradi hakuna sababu yoyote ya kutotekeleza Ibada ya Swala kwa Muislamu mwenye akili timamu na msafi (hili la usafi hapa ni maalumu kwa wanawake na wanalijua vizuri maana yake).

Swali la kujiuliza: Wanaotangaza kuwa wao ni Waislamu wanatekeleza Ibada ya Swala? Lililo dhahiri ni kuwa asilimia chache sana ya wanaotangaza kuwa wao ni Waislamu wanatekeleza Ibada ya Swala. Huamini? Jiulize, katika familia yako wangapi wanatekeleza Ibada ya Swala? Unapotoka alfajiri kwenda msikitini ni wangapi unawaacha wakiasi kuswali?

Kwa nini familia nyingi za Waislamu zinashindwa kuwa “familia za Kiislamu”?

Jibu la dhahiri ni kuwa familia nyingi za Waislamu hazithamini mafunzo na maadili ya Uislamu na hazina elimu ya kutosha ya kuiongoza familia husika kuwa familia ya Kiislamu. 

Dosari hii inasababisha, kwa kusema kweli, familia nyingi za Waislamu kutumia mfumo chotara wa malezi unaokusanya yanayokubalika na Uislamu na yasiyokubalika. 

Baya zaidi ni baadhi ya wazazi kuharibu saikolojia ya mtoto anapolinganisha maandalizi ya kwenda shuleni akilinganisha na maandalizi ya kwenda madrasa (shule maalumu kwa kutoa mafunzo na maadili ya Dini ya Uislamu).

Utaona mzazi anamwandaa vema mtoto pale anapokwenda shuleni huku akiwa hamfanyii maandalizi yoyote yenye hadhi pale anapokwenda madrasa. 

Yaani, wakati nguo zake za shule zitaandaliwa vema na kunyooshwa, wakati wa kwenda madrasa mzazi atamwambia: “Angalia nguo yoyote hapo kwenye kapu”. 

Ni vema kutambua kuwa wazazi kutothamini mafunzo na maadili ya dini ni sababu ya msingi ya watoto pia kutoyatilia maanani mafunzo na maadili ya dini na kutofikia lengo la kuelimika kidini na hatimaye kuwa Waislamu wasio na elimu ya kutosha ya misingi ya dini yao na katika maisha yao na watakapofikia kujenga familia zao watazijenga familia zenye kufuata mfumo chotara unaokusanya yanayokubalika na yale yasiyokubalika katika Uislamu.

Athari hasi za wazi za familia za aina hiyo ni kushindwa kwa wakuu wa familia hizo  kutekeleza amri ya Mwenyeezi Mungu inayowataka kuziamrisha familia zao, na si kuziomba na kuzibembeleza, kutekeleza Ibada ya Swala.

Katika mafundisho ya Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) anamtaka mzazi kumuamrisha mtoto kutekeleza Ibada ya Swala pale anapofika umri wa miaka saba na ampige (kipigo cha kumuadabisha ili atii bila shuruti, si cha kuua nyoka) kwa kuacha Swala afikapo umri wa miaka kumi.

Tunasoma katika Hadithi iliyopokewa kutoka kwa ‘Amri bin Shuayb (Allaah Amridhie) naye akiipokea kutoka kwa babaake, naye akiipokea kutoka kwa babu yake (‘Amri) kwamba Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amesema: “Waamrisheni watoto wenu kuswali wakifikisha miaka saba na waadhibuni (wapigeni) kwa kuiacha hiyo swala wakifikisha miaka kumi na watenganisheni katika vitanda (katika kulala).” (Hadithi hii inapatikana katika Vitabu vya Hadithi za Mtume, Sunanu Abi Dauud na Musnad Ahmad).

Unaweza kujiuliza kwa nini mtoto huyu aanze kuamrishwa kuswali afikapo umri wa miaka saba? Kwa nini aadhibiwe kwa kupigwa afikapo miaka kumi? 

Kuna nini katika namba saba na kumi? Bila ya kuvutwa na Mwanazuoni wa Kiswizi katika Bailojia na Saikolojia, Jean Piaget (1896 – 1980) juu ya hatua nne za makuzi ya akili, tunaona dhahiri kuwa Uislamu umetangulia kuonyesha hatua ya ukuzi wa akili ya mtoto kufikia kufikiri mawazo ya kufikirika (abstract thinking) na hapo Ibada ya msingi ya kuzoeshwa nayo ili imuingie na iwe vigumu kwake kuiacha hapo baadaye ni Ibada ya Swala.

Kwa nini Swala? Swala ni ibada yenye athari chanya ya kumzuia mwenye kuitekeleza kwa dhati kufanya maovu na machafu. 

Yaani, kipimo cha Muislamu kujipima kama Ibada ya Swala anayoitekeleza ina athari chanya kwake ni kujiangalia ni kwa namna gani amekuwa mbali na maovu na machafu. Vinginevyo, Ibada ya Swala kwake ni sawa na mazoezi ya viungo.

Tunasoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 29 (Surat Al-Ankaboot) Aya ya 45 kuwa: “Soma uliyo funuliwa katika Kitabu, na ushike Swala. Hakika Swala inazuilia mambo machafu na maovu. Na kwa yakini kumdhukuru Mwenyeezi Mungu ndilo jambo kubwa kabisa. Na Mwenyeezi Mungu anayajua mnayoyatenda.”

Nihitimishe makala hii kwa kuinasihi kila familia ya Muislamu kuhakikisha inathamini mafunzo na maadili ya dini na kwa msisitizo wa kipekee, ianze kujipima kwa kipengele kimoja tu cha kutekeleza Ibada ya Swala. 

Tukizingatia kuwa asilimia kubwa ya wanaotangaza kuwa wao ni Waislamu hawatekelezi Ibada ya Swala na kwamba familia nyingi zinazotambulika kuwa za Kiislamu hazitambuliki hivyo kwa kigezo cha kuishi Kiislamu au kutekeleza Ibada ya Swala ambayo ndiyo alama nyepesi kabisa ya kumtambua Muislamu anayefanya juhudi ya kuishi Kiislamu. 

Kwani ni Swala, iliyotekelezwa ipasavyo, ndiyo ambayo itamzuia kufanya maovu na machafu ikiwamo kutumia ulevi, kuzini, kucheza kamari, wizi na ufisadi, kutoa na kupokea rushwa, kuishi vibaya na majirani na kuamiliana vibaya na viumbe wengine wakiwamo binadamu, wanyama, ndege na mazingira yote kwa ujumla.

Haya tukutane Jumanne ijayo In-Shaa-Allaah.

Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata). Simu: 0713603050/0754603050

459 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!