FIKRA YA HEKIMA

Viongozi hawa hawatufai

Wakati wa uongozi wa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa, viongozi wengi wa serikali walijenga nidhamu na uwajibikaji kwa wananchi japo si kwa kiwango kikubwa. Wengi waliheshimu utumishi wa umma.

Taswira hiyo ilijengeka kutokana na semina elekezi kwa viongozi mbalimbali wakiwamo mawaziri, makatibu wakuu wa wizara, wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi watendaji wa halmshauri za wilaya, miji, manispaa na majiji.

Miongoni mwa mambo makuu yaliyohimizwa na Rais Mkapa kwa viongozi hao ni uhusiano mzuri na vyombo vya habari. Alitishia kuwachukulia hatua za kinidhamu watakaobainika kukaidi kutii maelekezo hayo. Watanzania wengi tulipongeza uamuzi huo.

Kuanzia wakati huo mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wamikoa na wilaya wakafunguka. Wakajenga uhusiano na waandishi wa habari. Wakaonesha ushirikiano wa kutoa habari kuhusu mikakati ya serikali katika kushughulikia kero na maendeleo ya Watanzania. Wengi tukafurahi kusikia na kuona kinachoendelea serikalini.

Kwa bahati nzuri, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete, naye mara baada ya kupata ridhaa ya Watanzania ya kuongoza nchi aliendeleza utaratibu huo wa mtangulizi wake. Tukasifu na kuona huo ni mwelekekeo mzuri wa mustakabali wa serikali yetu.

Lakini tofauti na enzi za uongozi wa Mkapa, nidhamu kwa viongozi wa sasa wa serikali imeshuka kwa kiwango cha kutisha. Wengi wamejenga kiburi na dharau kwa wananchi wanaohitaji huduma katika ofisi zao. Hawataki shughuli za ofisi zao zijulikane.

Tatizo kubwa linalodhihirika wazi kwa viongozi wengi wa serikali ni kutopokea simu. Kwa kifupi ni kwamba namba za simu zilizochapishwa kwenye vitabu, majarida na tovuti za ofisi za umma zimebaki kuwa mapambo tu.

Siku hizi ni bahati nasibu kupiga simu ya waziri, katibu mkuu, wabunge na mkuu wa mkoa ikapokewa. Kasumba hiyo inadhihirika pia kwa wakuu wa majeshi ya ulinzi na usalama, madaktari bingwa na maofisa uhusiano wa idara mbalimbali za serikali.

Siwezi kukataa ukweli kwamba wapo viongozi wachache wanaopokea simu za wananchi, lakini hata hao mara nyingi hawasikilizi na kujibu shida za waliopiga simu. Mara nyingi wanapopokea simu husema “niko kikaoni/ mkutanoni nitakupigia baadaye”, mara “niko barabarani nikifika sehemu nzuri nitakupigia”, mara “mpigie kaimu wangu, katibu wangu akusaidie shida yako”, mara “niko nje ya nchi nitafute baada ya wiki moja nitakuwa nimerudi ofisini”.

Viongozi wakuu wa kada hizo wameendeleza ukiritimba huo wa kutopokea simu za wananchi kwa kitambo sasa. Wengi wamejigeuza miungu-watu katika ofisi za umma. Binafsi sitaki kuamini kwamba Rais Kikwete hajaijua kero hii inayozizunguka ofisi za umma.

Siwezi kuamini pia kwamba viongozi wa sumpuli hiyo hawajui kuwa wamepewa dhamana ya kuzitumikia nafasi hizo kwa kuwahudumia wananchi kwa kusikiliza na kushughulikia mahitaji yao. Ninachoweza kuamini ni kwamba ama hawana mtu wa kufuatilia mwenendo wa utendaji wao wa kazi, au wamelewa madaraka.

Baadhi ya wizara zinazolalamikiwa zaidi kwamba viongozi wake hawapokei simu za wananchi, na ambazo hata mimi nimepata kuonja makali ya kero hiyo ni za Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ujenzi, Nishati na Madini, Fedha na Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu).

Inapofikia hatua mawaziri wa wizara hizo kupuuza simu za wananchi ambao kimsingi ndio waajiri wao, maana yake ni kwamba matarajio ya kufikia maendeleo ya kweli chini ya wizara hizo ni ndoto za mchana kweupe.

Kama waziri, katibu mkuu, wakuu wa majeshi ya ulinzi na usalama, wakuu wa mikoa na wilaya wamejenga ukuta kati yao na wananchi, mawasiliano baina ya pande hizo mbili yatakosekana na matokeo yake ni kudidimiza maendeleo ya kiuchumi na kijamii Tanzania.

Pengine rais wetu Jakaya Kikwete hapendi kusikia na kuona taswira hiyo ikitawala katika ofisi za umma chini ya uongozi wake. Basi awadhihirishie Watanzania dhamira hiyo kwa kuweka usimamizi utakaohakikisha utendaji uliotukuka na unaotamalaki katika ofisi za umma.

Ifike mahali kiongozi wa nchi aoneshe fadhila kwa wananchi waliomkabidhi madaraka. Akemee na kudhibiti kwa vitendo tatizo la kuporomoka kwa maadili miongoni mwa watu waliowateua kuwatumikia wananchi. Ninaamini na nitaendelea kuamini kuwa kasumba ya kutopokea simu za wananchi inayoendelezwa na baadhi ya viongozi wa umma serikalini ni kinyume cha maadili ya utumishi wa umma. Viongozi wa aina hiyo hawatufai hata kidogo. Rais asiwafumbie macho.

Nidhamu na uwajibikaji wa viongozi wa umma serikalini kwa wananchi iliwezekana enzi za uongozi wa Rais Mkapa, sitaki kuamini kuwa itaendelea kushindikana enzi hizi za uongozi wa Rais Kikwete.