Hujuma?

*Mwezi mmoja tu baada ya Rais kutembelea Kariakoo, soko lawaka moto

*Ni nembo ya biashara Tanzania, Mashariki na Kusini mwa Afrika 

*Alama ya kihistoria tangu ukoloni wa Mjerumani, Mwingereza hadi Uhuru

*Ofisa Ilala asema: ‘Nyaraka muhimu zipo salama, nyingine zipo Jiji’

*CAG amewahi kuonya kupuuzwa Sheria ya Zimamoto na Uokoaji

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Ni simanzi na vilio kwa wafanyabiashara wenye maduka ndani ya Soko la Kimataifa la Kariakoo baada ya moto mkubwa kuzuka na kuunguza sehemu kubwa ya jengo hilo usiku wa Jumamosi, Julai 10, mwaka huu.

Kwa upande mwingine hofu imetanda, wananchi wakidhani kuwa huenda kuna hujuma zimefanyika kuficha ‘uchafu’ unaodaiwa kufanywa sokoni hapo.

Juni Mosi mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan alifanya ziara ya kushtukiza sokoni Kariakoo ambapo mbali na kupokea kero za wananchi, aliusimamisha uongozi wa soko hilo kupisha uchunguzi wa tuhuma kadhaa zinazoukabili. 

Mmoja wa wafanyabiashara ameliambia JAMHURI kuwa kuna kila dalili kwamba moto uliozuka sokoni hapo ulilenga kuteketeza ushahidi wa tuhuma hizo. 

“Mimi nipo Kariakoo kwa zaidi ya miaka 25 sasa. Hakujawahi kutokea janga kama hili. Moto? Sokoni? Inawezekanaje? Ni hujuma tu,” anasema mfanyabiashara huyo kwa hasira Jumapili asubuhi wakati mwandishi wetu alipotembelea sokoni hapo. 

Huku akiomba kutotajwa jina lake, anakiri kwamba eneo la biashara yake halijaathirika kwa kuwa moto haukufika. 

“Sijalala. Nilipata taarifa saa tatu usiku na nikaondoka nyumbani kwangu (Goba) kuja hapa. Askari hawakuniruhusu kwenda kutoa bidhaa zangu wakihofia kwamba huenda vibaka wangepata nafasi ya kufanya uhalifu, lakini ninashukuru Mungu kila kitu kipo salama ingawa kuna wenzangu wameathirika vibaya sana,” anasema. 

Pamoja na kuelezwa kwamba moto ulianzia juu na si kwenye ofisi za soko zilizopo chini, bado anasisitiza: “Kaka, ni mipango tu hiyo kwamba moto uanzie huko lakini malengo ni huku.”

Kauli kama hiyo inaungwa mkono na wananchi wengine waliokuwa wakizungumza katika vikundi, wakisema hata namna Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kilivyokuwa kikifanya kazi, inatia shaka.

Hata hivyo, ofisa mmoja wa Manispaa ya Jiji (Ilala) aliyekuwapo eneo la tukio, ameliambia JAMHURI kuwa hizo ni hofu tu na tuhuma ambazo hazina uthibitisho. 

“Ofisi za soko hazijaungua, na hata kama zingeungua, nyaraka nyingi tena muhimu sana zipo ofisini kwetu Ilala (ofisi za jiji). Sasa kwa nini watu wanadhani kuwa ni hujuma? Hii ni ajali tu,” anasema mwanamama huyo. 

JAMHURI halikuweza kuzungumza na maofisa wa juu wa Jiji mpaka Jumapili mchana wakati tunakwenda mitamboni, wengi wakiomba kupewa muda kabla ya kuzungumza kwa kina nini kimetokea. 

Hata hivyo, tayari Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameunda timu ya uchunguzi na kuipa siku saba kukamilisha uchunguzi na kutoa majibu. 

“Pamoja na timu hiyo, pia tutazungumza na benki kuangalia namna ambavyo wafanyabiashara waliokopa ambao wameathiriwa na janga hili wanaweza kuongezewa muda kujipanga kulipa,” anasema Majaliwa, kauli iliyochukuliwa na wengi kama faraja kubwa wakati huu wa majonzi.

Kuzuka kwa moto

Taarifa za kuzuka kwa moto katika jengo hilo la kihistoria zilianza kusambaa kuanzia majira ya saa tatu usiku wa Jumamosi.

Mashuhuda wanasema moto huo ulianzia eneo la paa la juu la soko na baadaye kusambaa katika maeneo mengine.

“Kulikuwapo na juhudi za kuuzima, lakini mazingira ya eneo hayakuwa rafiki kwa magari na maofisa wa Zimamoto, ndiyo maana kazi ikaonekana kuwa ngumu,” anasema Jamal Rickady, mkazi wa Mtaa wa Mafia, Kariakoo.

Rickady aliyekulia Kariakoo, anasema hajawahi kushuhudia janga kubwa la moto kama hilo na kuongeza:

“Moshi mzito ulitanda mitaani kwetu. Ilitisha. Lakini nadhani Jeshi la Zimamoto bado ni dhaifu pia. Ni vema kikosi hiki kikaimarishwa kimafunzo na vifaa.

“Sasa kama soko linateketea hapa Kariakoo huku Kikosi cha Zimamoto kikiwa hapo Mwembetogwa (Fire), wanachelewaje kufika? Je, mikoani itakuwaje?”

Anasema janga hilo limewafilisi mitaji wafanyabiashara kadhaa anaofahamiana nao ambao hadi Jumapili asubuhi hawakuwa katika nafasi ya kuzungumza na mtu.

Hadi sasa sababu ya moto huo inatajwa kuwa ni hitilafu ya umeme.

Hamida Hassan Awadh, mkazi wa makutano ya Sikukuu na Kariakoo, anakwenda mbali akitaka Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene kuwajibika.

Anawataja mzee Ali Hassan Mwinyi, Brigedia Jenerali Abdallah Natepe, Dk. Emmanuel Nchimbi na Shamsi Vuai Nahodha kuwa miongoni mwa waliowahi kuwajibika kutokana na yaliyotokea wizarani kwao.

“Kwa hiyo Simbachawene hana sababu ya kubaki. Haiwezekani waziri ukubali kubeba dhamana hiyo halafu mambo ya kuhatarisha maisha ya watu yanatokea wewe upo tu,” anasema.

Hamida anasema udhaifu wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, majengo hatarishi ya serikali, udhaifu katika mapambano dhidi ya uhalifu ulioanza kujitokeza kuwa ni hoja zinazopaswa kutolewa maelezo na Simbachawene.

Katika eneo la tukio, vikosi vyote vya Zimamoto vilivyopo Dar es Salaam vilishirikiana katika kupambana na moto huo.

Walau magari zaidi ya sita ya Zimamoto kutoka Ilala, Temeke, Kinondoni, Uwanja wa Ndege na bandarini yalionekana kuuzingira na kuukabili moto huo.

Serikali yaweka kambi

Kwa mujibu wa maagizo aliyoyatoa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, viongozi wa kiserikali Mkoa wa Dar es Salaam, wakiongoza na Mkuu wa Mkoa, Amos Makalla, wanapaswa kuwapo eneo hilo wakati wote.

Majaliwa ameagiza vyombo vingine kama Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), Ofisi ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP), TANESCO na Jeshi la Polisi vyote kupiga kambi kwa muda eneo hilo.

“Kwa sasa wafanyabiashara wasiingie ndani kwa muda hadi hali itakapokuwa shwari na uchunguzi kukamilika,” anasema Majaliwa.

Alama ya kihistoria

Kuungua kwa Soko la Kariakoo kumewatoa machozi wananchi kadhaa, wakidai kuwa ni alama ambayo haipaswi kupotea.

“Hapa pana historia ndefu. Eneo hili limeanza kutumika tangu enzi za Mjerumani. Askari waliopigana Vita Kuu ya Kwanza walikuwa wakikutana hapa.

“Askari hawa walitoka kila kona ya ‘koloni’ la Mjerumani (Tanganyika) na hata nje ya koloni hilo. Yaani ni mkusanyiko wa kimataifa kama ilivyo leo.

“Awali palijulikana kwa Kiingereza kama ‘carrier corps’. Silaha zilikusanywa hapa. Baadaye matamshi yakabadilika na ndipo likaja jina Kariakoo,” anasema mzee Abdallah Tambaza, mwenyeji wa eneo hilo.

Mzee Tambaza anasema baada ya Ujerumani kushindwa vita na Mwingereza kuingia, eneo hilo liliendelea kutumika kama sehemu ya biashara.

“Posta ya kwanza ya Dar es Salaam ilijengwa Kariakoo, kwa kuwa hapo lilipo soko palikuwa na mkusanyiko mkubwa wa wafanyabiashara, Serikali ya Uingereza ikaona ni bora pajengwe posta.

“Ile inayoitwa Posta ya Zamani iliyopo karibu na bahari, ilifuata baada ya hii ya Kariakoo. Kwa hiyo Dar es Salaam kukawa na ofisi mbili tu za posta,” anasema.

Mzee Tambaza anasema hadi miaka ya 1960, bidhaa zote zilikuwa zikipatikana hapo, na kwamba: “Hata samaki waliuzwa hapa. Walikuwa wakitoka Ununio, Kunduchi na maeneo mengine.”

 Kwa mantiki hiyo, Kariakoo imekuwa ikiwavutia wageni kutoka ndani na nje ya Afrika kutokana na historia yake na mzee Tambaza anasema:

“Miaka ya 1960 chini ya Meya wa Dar es Salaam, Ally Saleh Sambuso, ndipo mipango ya ujenzi wa soko la kisasa ilipoanza.

“Kazi ya kuchora mchoro wa jengo la Kariakoo alipewa Mhandisi aliyesomea Israel, Beda Amori. Akabuni jengo moja zuri sana kwa wakati ule hadi leo hii.

“Paa la kuvutia kama maua hivi! Soko linaanzia shimoni hadi ghorofa ya pili! Lilikuwa jengo zuri sana hata leo bado ni zuri. Likaongeza mvuto. Kumbuka wakati huo mwaka 1971 soko linaanza kutumika, nyumba za Kariako zilikuwa za miti na udongo, sasa jengo hilo halikuwa la kawaida eti!” anasema.

Mzee Amori ndiye pia aliyebuni jengo la Ushirika lililopo Mnazi Mmoja; miongoni mwa majengo marefu na ya kuvutia kuanzia miaka ya 1970.

Kitovu cha biashara

Kauli ya mzee Tambaza inashabihiana na ukweli ulivyo hata sasa ambapo wafanyabiashara kutoka mikoa yote Tanzania hufanya ununuzi Kariakoo.

Lakini pia wageni kutoka mataifa ya Malawi, Zambia DRC, Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya hufika hapo kununua bidhaa mbalimbali.

Onyo la CAG

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2018, imeonyesha kuwapo uzembe katika utekelezaji wa Sheria ya Zimamoto (Fire and Rescue Act No. 14 of 2007).

CAG anasema Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji hakitekelezi ipasavyo maagizo yaliyomo kwenye kifungu cha 15(3)(b) yanayokitaka kufanya ukaguzi wa vifaa vya zimamoto katika majengo ya serikali yaliyopo eneo lao la kazi.

“Sheria hii inawataka kutoa cheti baada ya ukaguzi huku wakifanya ukaguzi wa kawaida na wa kushitukiza kuangalia uwezekano wa kuzuka moto kwenye majengo ya serikali.

“Ukaguzi uliofanywa kwenye majengo hayo unaonyesha kwamba mengi yapo katika hatari ya kukumbwa na janga la moto,” anasema CAG.

CAG anawatupia lawama wamiliki wa majengo husika kwa kushindwa kutoa taarifa kuhusu udhaifu wa miundombinu ya kuzuia majanga ya moto, hivyo kuyafanya majengo mengi kutokuwa salama kwa matumizi.

Moto shule ya wasichana

Kutoka Morogoro, moto uliozuka katika shule moja ya wasichana umesababisha wanafunzi watano kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoani humo.

Taarifa zinadai kuwa moto huo ulizuka usiku wa Jumamosi iliyopita katika Shule ya Wasichana ya Kiislamu ya AT-TAAUN.

Wanafunzi hao wamelazwa kwa muda kutokana na mshituko baada ya ghorofa mbili za bweni lao kuwaka moto.