Iran kumchapa Trump

*Rais, majenerali wawili, Ayatollah wampa onyo kali
*Wajipanga kwa vita kuiteketeza Marekani kila kona
*Maninja waanza mazoezi jangwani, wadai wao si Korea
*Uingereza, Ufaransa, China, Urusi, Ujerumani
wamgomea

TEHERAN, IRAN

Wasiwasi umetanda duniani baada ya Jeshi la Iran
kumpa onyo kali Rais Donald Trump kuwa akianzisha
vita na taifa hilo Marekani itapotea katika uso wa dunia.
Kamanda wa Vikosi Maalumu, Meja Jenerali Qassem
Soleimani, amesema vita wanayopanga kuianzisha
Marekani dhidi ya Iran zamu hii itawatokea puani.
“Ikiwa Marekani itaivamia Iran, basi tutaharibu kila kitu
inachokimiliki duniani,

” amesema Meja Jenerali

Soleimani mwishoni mwa wiki.
Amesisitiza kuwa: “Marekani ikianzisha vita, basi Iran
itamalizia.” Haya ni kwa mujibu wa Shirika la Habari la
Iran, liitwalo Tasnim.
Hatua ya meja jenerali huyu imekuja baada ya Rais
Trump kutuma ujumbe kwa njia ya Twitter ukiwa katika
herufi kubwa akimwonya Rais wa Iran, Hassan Rouhani,
kuwa: “Kamwe, kamwe usithubutu kuitisha Marekani.”

Julai 21, mwaka huu, Rais wa Iran, Rouhani, alimuonya
Trump kuwa iwapo anawaza kupigana vita na Iran, basi
ajue hiyo ndiyo itakuwa “mama wa vita yote iliyopata
kutokea duniani na Marekani itajuta kwa uamuzi huo.”
Joto limepanda kati ya Marekani na Iran baada ya
uamuzi wa Trump kujiondoa katika mkataba wa mwaka
2015 uliofikiwa kati ya Marekani na Iran jinsi ya kuachana
na silaha za maangamizi na nyuklia.
Meja Jenerai Soleimani – anayeongoza vikosi vya
Wanapinduzi vya Iran amesema: “Kama askari, ni
jukumu langu kujibu vitisho vyako.”
Ameongeza: “Zungumza na mimi, si Rais (Hassan
Rouhani). Si jukumu la rais wetu kukujibu… tuko karibu
nawe, maeneo usiyotarajia. Njoo. Tuko tayari. Ikiwa
utaanzisha vita, tutaimaliza. Unafahamu vema kuwa vita
hii itaangamiza kila ulichonacho.”
Mwanajeshi huyo mwandamizi, amemshutumu Trump
kwa alichokiita kutumia “lugha ya kwenye baa na nyumba
za kamari.”
Majibu ya askari huyo yametokana na ujumbe wa twitter
wa Trump, aliyetumia herufi kubwa dhidi ya Rais
Rouhani, kwa kusema: “KAMWE, MILELE USITHUBUTU
KUITISHA MAREKANI TENA AU MATOKEO YAKE
UTAPATA MAUMIVU AMBAYO WACHACHE KATIKA
HISTORIA YOTE WAMEYAPATA MILELE. SISI SI NCHI
TENA ITAKAYOHIMILI MANENO YAKO YA UKICHAA
WA VURUGU NA VIFO. KUWA MAKINI.”
Hata hivyo, siku mbili baada ya Meja Jenerali Soleimani
kumpa onyo kali Trump, Trump amebadili msimamo
wake wakati anazungumza na maveterani wa vita wa
Marekani, aliposema: “Marekani iko tayari kuwa na

mkataba wa maana na Iran kuondoa vita isiyo ya lazima.”
Trump alikuwa amecharuka baada ya awali Rais wa Iran
kukaririwa na Shirika la Habari la Serikali la Irna akisema:
“Marekani inapaswa kufahamu kuwa amani na Iran ni
mama wa amani zote, na vita na Iran ni mama wa vita
zote.”
Mwezi Mei mwaka huu, Trump ametangaza kuiondoa
Marekani katika mkataba wa kusitisha uendelezaji wa
nyuklia ulioingiwa na Serikali ya Rais Barack Obama kati
ya mataifa hayo mawili na washirika wao, jambo ambalo
lilikuwa kinyume cha ushauri wa washirika wa Marekani
kutoka nchi za Ulaya. Amekuwa akisema makubaliano ya
Iran yalikuwa na upungufu mkubwa.
Katika kujibu mapigo, Iran ilitangaza kuwa inarejea
mpango wake wa kurutubisha madini ya uranium ili
kuendeleza utengenezaji wa mabomu ya nyuklia na
uzalishaji wa umeme wa kutumia teknolojia ya nyuklia.
Kutokana na kauli hii, Marekani sasa inarejesha vikwazo
vya uuzaji wa mafuta kwa Iran, uuzaji wa ndege kwa Iran,
vyuma vya thamani na vikwazo vingine vingi vya
kibiashara.
Hata hivyo, nchi za Uingereza, Ufaransa, China, Urusi na
Ujerumani ambazo zote mwaka 2015 zilitia saini mkataba
huo wa amani, zinasema Trump hawezi kuwa na akili
kuliko mataifa hayo yote kwa ujumla wake.
Kwa upande wake, Marekani inasema nchi za Iran na
Saudi Arabia zinaamini Iran inaendeleza urutubishaji wa
nyuklia, suala ambalo ni hatari kwa ustawi wa mataifa
hayo.
Kwa upande wake, Iran imesema mara kadhaa kuwa
urutubishaji inaoufanya ni wa kuzalisha umeme na

imekaguliwa mara nyingi na Wakala wa Mionzi wa
Kimataifa.
Katiba hotuba yake kwa wanadiplomasia nchini Iran, Rais
Rouhani, amesema: “Ndugu Trump, usicheze na mkia wa
simba, hii itakupeleka katika majuto.
“Marekani inapaswa kutambua kuwa amani na Iran ni
mama wa amani zote, na vita na Iran ni mama wa vita
zote.” Marekani imekuwa na mgogoro na Iran tangu
mwaka 1979 yalipofanyika mapinduzi ya Kiislamu nchini
Iran.
Ameongeza kuwa Marekani haina uwezo wa kuchochea
wananchi wa Iran wavichukie vyombo vya ulinzi na
usalama vya Iran.
Rais wa Iran ameongeza kuwa taifa hilo haliwezi
kutishiwa kwa kuwekewa vikwazo vya kuuza mafuta nje
ya nchi na kwa anayefahamu Iran ndiyo imekuwa mhimili
wa usafirishaji salama wa mafuta katika Ghuba ya
Uajemi.
Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei,
amemuunga mkono Rais Rouhani kwa kusema: “Iran
inaweza kuzuia mafuta yote ya Ghuba yasiuzwe nje ya
eneo hilo.”
Rais Rouhani awali alikuwa ametishia kuvuruga
usafirishaji wa mafuta katika eneo la Ghuba iwapo
Marekani ingeendelea kuelekeza uwekaji wa vikwazo
dhidi ya mafuta ya taifa hilo.
Mkuu wa Majeshi wa Iran, Jenerali Mohammad Baqeri,
amesema: “Tabia ya adui haitabiriki… ingawa Serikali ya
sasa ya Marekani haitoi vitisho vya vita, kwa hakika
imekuwa ikijitahidi kulishawishi Jeshi la Marekani
kuanzisha vita (dhidi ya Iran).”

Kwa tishio hili la Marekani kuiwekea vikwazo Iran,
kiwango cha mafuta linachouza nje ya nchi taifa hilo
kinaweza kushuka kwa theluthi mbili, hali inayoweza
kuathiri bei za mafuta duniani, kwani Trump anataka
ifikapo Novemba nchi zote duniani ziache kununua
mafuta ya Iran.
Hata hivyo, Marekani inasema inaweza kuyaruhusu
baadhi ya mataifa washirika kuendelea kununua mafuta
kutoka Iran, kwani yapo ambayo yanategemea asilimia
kubwa ya mafuta kutoka katika taifa hilo.
Katika hatua nyingine, majeshi ya Iran yameanza
mazoezi makali wakishirikisha vikosi vya maninja. Mmoja
wa makamanda waandamizi amesema: “Iran si kama
Korea Kaskazini, ina mkono mrefu kila kona ya dunia hii.”
Kauli hii ikiunganishwa na tishio la kuvuruga uuzaji wa
mafuta kwa nchi nyingine za Ghuba, inaiweka dunia
katika wasiwasi mkubwa.
Dunia ilitarajia kuwa salama baada ya Marekani kuwa
imemaliza mgogoro wa kidiplomasia na Kiongozi wa
Korea Kaskazini, Kim Jong Un, ambaye awali alikuwa
anafanya majaribio ya makombora ya nyuklia na kuionya
Marekani kuwa ipo siku ataifuta katika uso wa dunia,
lakini sasa Trump ameamsha upya dude na kuiingiza
dunia katika wasiwasi kutokana na mtifuano huu mpya
wa Marekani na Iran.