Balile

Balile
Deodatus Balile
Wiki iliyopita nilihitimisha makala yangu kwa kukueleza jambo muhimu mpendwa msomaji. Hitimisho langu lililenga katika kukujuza japo kwa ufupi Jaji Warioba ni nani.

Nianze tu kwa kurejea japo kwa ufupi kwamba mwaka 1977 Jaji Warioba ndiye aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Huyu ndiye aliyepokea rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1977 iliyoandikwa kwa mkono na tena kwa Kiswahili na Jaji George Liundi. Niliambiwa maneno haya na Jaji Liundi katika mahojiano maalum.

Leo ikiwa ni miaka 35 baadaye, Jaji Warioba amepewa jukumu la kuongoza Tume ya Kuandika Katiba Mpya. Hapana shaka ndani ya miaka 35 ameona mengi, amejifunza mengi na amebaini yanayochelewesha au kuwahisha maendeleo katika nchi zote duniani.

Mimi nilisema tangu awali kwamba nia yangu ni kutoa japo pendekezo la msingi, ambalo likiridhiwa nchi hii itapata maendeleo ya kasi ajabu.

Nimezungumza mada hii na watu wengi kabla ya kujitosa kuiandika. Wengi ukiwasikiliza wanatumia sababu moja tu kwamba Tanganyika kieneo ni kubwa hivyo itaimeza Zanzibar katika mfumo wa Serikali ya Shirikisho. Hapa ndipo ninaposema tunajichanganya. Muda wa kufunika kombe mwanaharamu apite umepita. Leo si jana.

Inawezekana waasisi wetu walikuwa sahihi katika hatua kama hii, lakini leo hili limepitwa na wakati. Ikumbukwe Muungano wetu ambao nauunga mkono kwa asilimia 100 na hata ikiwezekana tupanue mipaka hadi Afrika nzima iwe taifa moja kama zilivyokuwa ndoto za Kanali Muammar Gaddafi. Hili la ukubwa wa Tanganyika ndilo ninalotaka kulifafanua.

Inapaswa kufahamika bayana kuwa ubia wa Tanganyika na Zanzibar ni mfumo wa kuunganisha nchi mbili zenye hadhi sawa. Hapa hatuingii ulingoni. Hatupigi ngumi kusema Mike Tyson akipambana na January Makamba kwa maumbo yao atamng’oa meno Makamba. Hizi ni hisia na dhana mfu. Mfumo uliopo sasa nitaeleza jinsi unavyochelewesha maendeleo.

Zipo haki za msingi ambazo mfumo huu unazipuuza lakini ni kero. Kwa mfano, hakuna Mtanganyika anayeweza kwenda Zanzibar akagombea hata Usheha au akawa Katibu Kata. Watanganyika waliopo Zanzibar wanatumika katika wizara za Muungano tu. Hapa kwetu (Tanganyika) tunayo mifano mingi ya Wazanzibari wanaoshikilia nyadhifa za hadi uwaziri kwenye masuala yasiyo ya Muungano.

Sitanii, najua wapo watakaobishi. Orodha ni ndefu ila nitoe mfano mmoja tu. Dk. Hussein Mwinyi alikuwa Naibu Waziri wa Afya kwa muda mrefu. Kwa nini? Huyu ni Mzanzibari na hii si wizara ya Muungano. Wapo wakurugenzi kibao kutoka Zanzibar wanaoshikilia nyadhifa za Tanganyika kinyume cha sheria.

Ukiwauliza wenye kutetea mfumo wa sasa wanakwambia kuwa mfumo wa sasa wa Serikali mbili unapunguza gharama za uendeshaji. Binafsi hili silioni. Tena sasa hivi mfumo huu ndiyo unaoongeza gharama.

Tumefika mahala kwa kutaka kufunika mambo, tunaunda vyeo kufurahisha Wazanzibari wanaotumika katika Serikali ya Tanganyika a.k.a Muungano.

Kwa mfano, kuna sababu gani ya kuwa na waziri na naibu mawaziri wawili katika Wizara ya Fedha? Hii ni siasa. Tunaona tukiweka Mzanzibari na Mtanganyika, italeta sura ya Muungano hata kama kuwapo kwa wawili hawa ni mzigo usiobebeka kwa Serikali. Hali kama hii ipo kwa makatibu wakuu, makamishna na wakurugenzi. Vyeo vinagawiwa kuridhisha hisia za Muungano.

Zinapotungwa sheria tunaambiwa kuna mambo ya Muungano na yasiyo ya Muungano. Ila cha kushangaza, sheria hizi zinapotungwa ndani ya Bunge, wabunge kutoka Zanzibar huwa hawatolewi nje ya ukumbi wa Bunge na wanashiriki katika mijadala ya kutunga sheria za Tanganyika. Ni mbunge gani anayeweza kutoka Bara akaenda Zanzibar akashiriki mjadala katika Baraza la Wawakilishi?

Sitanii, angalia majimbo ya Zanzibar. Yapo yenye wapigakura hadi 4,000, idadi ambayo ni chini ya Diwani wa Kata kama Kashai ya Bukoba Mjini. Jimbo moja la Zanzibar kieneo na kwa idadi ya watu kuna yasiyolingana na baadhi ya vijiji vya Tanganyika, achilia mbali kata. Kijiji cha Twatwatwa cha Kilosa ni kikubwa kuliko majimbo ya Uzini na Mji Mkongwe yakichanganywa.

Ajabu majimbo haya ya Zanzibar yana wabunge wawili wawili kwa kila jimbo. Kila jimbo lina Mbunge na Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi. Watu 4,000 wanawakilishwa na wabunge wawili, lakini Jimbo kama Ukonga lililokuwa na watu zaidi ya 1,000,000 linawakilishwa na Mbunge mmoja. Kisha unasema gharama za kuendesha Serikali ni ndogo kwa mfumo wa sasa.

Nigusie jingine. Leo ndani ya mfumo huu ninaoamini hata wanaoutumikia hawaufahamu vizuri, kama kukitokea mgongano kati ya masilahi ya Zanzibar na Tanganyia, wawili hawa wanakata wapi rufaa? Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndiye huyo huyo wa Tanganyika. Je, haiwezekani ukitokea mgogoro mkubwa Rais huyu atakosa miguu ya kusimamia?

Ninachoamini ni kwamba tukiamua kuwa na mfumo wa Serikali tatu, mambo yafuatayo yatatokea. Kwanza tutakuwa na aina ya Muungano unaoeleweka mfumo wake kuliko hali ya sasa ya kufinyanga.

Pili gharama za uendeshaji zitashuka. Zitashuka kwa maana Serikali Kuu itabaki na majukumu ya msingi kama ilivyo kwa Marekani ambayo ni Ulinzi na Usalama, Fedha, Uhusiano wa Kimataifa, Uhamiaji, Elimu ya Juu, Benki Kuu pengine na nyingine chache zisizozidi mbili.

Haya masuala yanayotugombanisha ya mafuta, umeme, madini, gesi, maliasili, afya, uvuvi, kilimo, elimu ya kati, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na utitiri mwingine, yote yanabaki mikononi mwa Serikali za Zanzibar na Tanganyika.

Tena hata hawa ili wapate ufanisi zaidi, inabidi waichukue Sera ya Majimbo inayohubiriwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Itakuwa ni miujiza Rais wa Tanganyika na Waziri Mkuu wake waweze kusafiri kutoka Nkasi hadi Newala, kisha waende Kyaka-Bukoba, baadaye Sirari na Horohoro utarajie ufanisi.

Hawa wanapaswa nao kuongoza hii kada yenye sura ya kitaifa kisha kanda zilizopo zigeuke majimbo. Kanda hizi ni Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kati, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kusini na Kanda ya Mashariki. Kwa Zanzibar wanaweza kuamua kuunda majimbo mawili – Unguja na Pemba.

Sitanii, najua hapa mmeshaanza kufikiria majina ya vyeo vya wakubwa hawa yatakuwaje. Mapendekezo ninayo. Tumeshaiga sehemu ya mfumo wa Marekani, basi tuanzie hapo.

Serikali ya Muungano itakayokuwa na wizara zisizozidi sita, iongozwe na Rais atakayekuwa Amiri Jeshi Mkuu akisaidiwa na Makamu wa Rais. Hapa tunaweza kwa makusudi tukasema kama Rais atatoka Tanganyika, Makamu wake atoke Zanzibar kama ilivyo sasa. Waziri wa Mambo ya Nje, awe na nguvu sawa na Waziri Mkuu, kama ilivyo kwa Marekani.

Hizi Serikali za Tanganyika na Zanzibar ikipendeza ziongozwe na watu watakaoitwa marais ili nao wasikonde. Maana tusipowapa wadhifa huo wataona wanazidiwa na akina Leogedar Chilla Tenga, Rais wa TFF.

Hawa nao wawe marais nao waunde mabaraza ya mawaziri wasiozidi 10 kila mmoja. Wizara hizi zifanye kazi ya uratibu tu. Msaidizi mkuu wa hawa wakubwa aitwe Waziri Mkuu. Vyeo ni majina tu, mbona Zanzibar leo kuna Makamu wa Rais wawili na mambo yanakwenda ingawa nchi hii ina wakazi wasiozidi 1,100,000?

Hawa wakuu wa Serikali za Majimbo waitwe Mawaziri Kiongozi. Hawa nao waunde mabaraza madogo yanayoendana na Kamati za Halmashauri za miji zilizopo sasa. Kila halmashauri iwe na kamati zisizozidi 10, ambazo kati yake ni Kamati ya Fedha, Maendeleo ya Jamii, Uchumi na Biashara, Miundombinu, Elimu na nyingine kadri itakavyofaa wakati wa mjadala huu. Hawa mawaziri viongozi nao waunde serikali ndogo zenye wizara zisizozidi 10 kila mmoja.

Najua hapa litaibuka swali lililoambatana na uvivu wa kufikiri. Wapo watakaosema gharama itakuwa kubwa kuendesha serikali hizi. Hili nitalifafanua katika makala yajayo na nitaeleza faida za mfumo huu unaotumiwa na nchi zote zilizoendelea duniani ikiwamo Afrika Kusini, Misri, Marekani, Canada na Uingereza kwa kuzitaja chache

Litaibuka pia suala la ukabila, nalo nitalijibu katika makala zijazo na naamini ukifuatilia kwa karibu hatupotea njia. Je, twende mkondo upi? Usikose nakala ya Gazeti la JAMHURI wiki ijayo upate sehemu ya tatu ya makala haya. Mungu ibariki Tanzania.

By Jamhuri