Kwanza niwatakie Heri ya Mwaka Mpya wapendwa wasomaji, watangazaji wote wenye mapenzi mema na Gazeti la JAMHURI.

Kwa miaka mitano, mmekuwa bega kwa bega nasi; na wakati huo huo tumekuwa tukiwapata wasomaji na watangazaji wengine wapya. Jambo hili linatutia faraja kubwa mno. Tumeendelea kuamini kuwa penye nia pana njia, na kwamba watu wakiwa na dhamira na wakaisimamia dhamira hiyo, mabadiliko chanya ni jambo lisiloepukika. Tunawashukuruni sana.

Wakati mwingine inabidi niwaombe radhi wasomaji, hasa wa makala zangu kutokana na kushupalia kwangu baadhi ya mambo. Miongoni mwa mambo niliyoshupalia, ni suala la Loliondo.

Kuna dhana mbalimbali zinazojitokeza wakati mwandishi anaposhupalia jambo. Ipo dhana ya ‘kutumiwa’. Ipo dhana ya ‘chuki’. Ipo dhana ya ‘vita’, na kadhalika.

Haya yamesemwa kwenye habari na makala mbalimbali tulizoandika katika JAMHURI, lakini mwishowe ukweli uliweza kubainika. Mathalani, tuliposhupalia suala la Bandari, wapo walioibuka na dhana hizo nilizozitaja. Tuliposhupalia uongozi mbovu wa Lazaro Nyalandu katika Wizara ya Maliasili na Utalii, wapo waliohoji. Yapo mengi ya aina hiyo. 

Lakini bahati nzuri ni kwamba baada ya kushupaa kwetu, hatimaye ukweli uliweza kudhihiri; na kwa maana hiyo tukawa tumetekeleza wajibu wetu tuliouainisha katika tahariri yetu ya kwanza kabisa miaka mitano iliyopita.

Ni kwa sababu hiyo hiyo, nawaomba wasomaji walau kwa leo mniruhusu niuanze mwaka kwa makala ya uhifadhi, nikiamini bado nina wajibu wa muda mrefu wa kuulinda utajiri huu tuliojaaliwa na Mwenyezi Mungu.

Makala yangu ya ‘mambo aliyopotoshwa Waziri Mkuu Loliondo’, imepokewa kwa namna tofauti, lakini kubwa zaidi ni kwamba nilichosema ni kweli na kwa maana hiyo endapo kitazingatiwa, ndani ya miezi michache ijayo tunaweza kuiona Loliondo mpya.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani, ametua Loliondo na kufanya kazi kubwa mno. Kufika kwake huko mara ya pili ndani ya muda mfupi kumeelezwa kuwa ni kufuatilia utekelezaji maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa – kubwa likiwa kumaliza ‘mgogoro’ kati ya wawekezaji na wananchi (ambao kimsingi si wananchi, bali mashirika yasiyo ya serikali (NGOs).

Endapo mambo yataenda kama yalivyopangwa, Mei, mwaka huu inaweza kuwa ndiyo hitimisho la mgogoro katika eneo hilo. Hii ni nadharia tu. Naomba hapa rekodi iwekwe sawa kwamba kutulia kwa Loliondo, maana yake ni kuwakosesha mapato watu kadhaa – wamiliki wa NGOs – wanaoishi kwa kukusanya mabilioni ya shilingi kwa kivuli cha kuwatetea wananchi. 

Sijui kitu gani kitawafanya ‘watetezi’ hao waafiki kumalizwa kwa mgogoro huo? Sijui! Lakini kwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano, naamini suluhisho linaweza kupatikana hata kama ni kwa baadhi ya watu kuumia kwa kukosa fedha za wafadhili.

Nikiri kuwa nimepokea simu kutoka kwa viongozi kadhaa wakinishawishi niache, japo kwa muda, ‘kufukua’ mambo ili kutoa nafasi kwa majadiliano mapya yaliyoanzishwa na Injinia Makani. Naheshimu mwito huo.

Lakini niseme wazi kuwa kuheshimu mwito huo hakuna maana ya kuacha kuainisha udhaifu wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha aliyeamua kuwa upande wa NGOs na rafiki zake AndBeyond; pamoja na kaka yangu,Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Mfaume, ambaye utii wake kwa Mrisho Gambo unaonekana wazi kuwa ni wa woga na wa kimaslahi.

Gambo ameandika kwenye mitando ya kijamii juu ya dhamira yake ya kunishitaki mahakamani kwa kile anachodai kwamba nimemchafua! Kama ameshauriwa, awarejee waliomshauri; la kama ni uamuzi wake mwenyewe, autafakari upya. Suala la Loliondo nalifahamu pengine kuliko yeye. Katika hili, mchango wangu kwa Taifa langu ni kusimamia ukweli bila woga na bila kumwonea mtu.

Naitikia mwito wa ‘kupunguza makali’ baada ya kuundwa kwa kamati halali inayowajumuisha watu wa kada mbalimbali’ tofauti kabisa na ile iliyoundwa na Gambo na washauri wake kwa maslahi yao.

Haya tunayafanya ili kutimiza wajibu wetu wa kikatiba. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatutaka tulinde mali ya umma. Ibara ya 27.-(1) inasema: “Kila mtu ana wajibu wa kulinda maliasilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya mamlaka ya nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine.

(2) Watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu, na kuendesha uchumi wa Taifa kwa makini kama watu ambao ndiyo waamuzi wa hali ya baadaye ya Taifa lao.”Ndivyo Katiba ya nchi yetu inavyotutaka. 

Wanyamapori na misitu ya Loliondo ni mali ya Watanzania kama ilivyo gesi mkoani Mtwara, almasi mkoani Shinyanga; dhahabu ya Tarime, Geita na kwingineko. Utajiri wa nchi sharti unufaishe nchi nzima. Hatuwezi kukaa kimya ilhali Loliondo ikiuawa kwa kigezo cha wanaoiua ndiyo wenye nayo! Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 90 ya mapato katika Wilaya ya Ngorongoro yanatokana na utalii – kwa maana ya wanyamapori na misitu! Asilimia 10 tu ndiyo iliyopo kwenye mifugo na shughuli nyingine. 

Kwa mapato hayo, ni dhambi kubwa kwa kila mwenye uwezo wa kusema, kushindwa kusema wakati akiona Loliondo au Ngorongoro ikiuawa! Kampuni kama OBC na AndBeyond zinaweza kuondoka, lakini Loliondo ikabaki. Ikibaki katika hali nzuri, watakuja wengine, lakini ikibaki jangwa tu hakuna atakayekuja kuwekeza. Uhai wa Loliondo ni wanyamapori, miti na maji.

Chimbuko la mgogoro Loliondo ni kuongezeka kwa idadi ya watu na mifugo inayotokana na wenyeji na wahamiaji haramu kutoka Kenya. Mifugo hiyo isiyodhibitiwa imeathiri maeneo muhimu kwa utalii katika Hifadhi ya Taifa Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, hasa eneo la  Ndutu. 

Kuongezeka kwa shughuli za kilimo na shughuli nyingine za kibinadamu; na kukosekana kwa mipango ya matumizi bora ya ardhi katika eneo lote la Pori Tengefu Loliondo, kumesababisha kuwapo kwa matumizi holela ya ardhi. Hii inajumuisha kuongezeka kwa vijiji vipya, vijiji kuingia mikataba holela na wawekezaji; mfano wa mkataba wa Ololosokwan na wawekezaji wa AndBeyond na Buffalo. Mapato yanayotokana na uwekezaji huo hayaiingii serikalini.

Shughuli za mifugo si tu zimeathiri uhifadhi katika eneo la Pori Tengefu Loliondo, bali pia katika eneo zima la Ngorongoro na Serengeti – kuliko na kitovu cha utalii nchini.  

Pori Tengefu la Loliondo lina vyanzo vya maji ya Mto Grumeti unaotiririka kuelekea mbuga ya Serengeti hadi Ziwa Victoria. Vyanzo hivi vinachangia asilimia 47.8 ya maji yote yanayotumiwa na wanyama ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti. Shughuli za kilimo na mifugo mingi katika eneohilo zisipodhibitiwa zitasababisha vyanzo hivyo kukauka na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti itaathirika mno au hata kutoweka.

Ni kwa maana hiyo, kuhifadhi eneo lenye vyanzo vya maji katika Pori Tengefu Loliondo kuna umuhimu mkubwa sana katika ustawi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Ikiwa mifugo na watu kutoka nje ya Tanzania watadhibitiwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi utaandaliwa na kutekelezwa na vyanzo mbadala vya maji kupatikana, eneo lililopendekezwa kubakizwa kama Pori Tengefu halitaathiri mifugo kwa kuwa eneo litakalobaki litakidhi mahitaji ya malisho ya mifugo na shughuli nyingine za kilimo na makazi.

Kwa sasa kuna mradi wenye thamani ya Sh bilioni 10.2 unaosimamiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Hifadhi ya Taifa Serengeti. Unalenga kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi na kuanzisha vyanzo mbadala wa maji kwa uchimbaji malambo.

Kuna umuhimu wa kuwa na ufugaji unaozingatia uwezo wa eneo la malisho, kudhibiti mifugo kutoka Kenya na kuboresha miundombinu ya  mifugo.

Sioni ni kwa nini kusianzishwe viwanda vya kusindika mazao ya mifugo ili kudhibiti mifugo kuvamia eneo litakalobakizwa kuwa Pori Tengefu.

Loliondo ina wanyamapori na ndege wa aina mbalimbali. Kiikolojia, eneo hilo ni muhimu kwa kuwa ni sehemu ya mapito ya nyumbu na pundamilia – kundi la wanyamapori wahamao kutoka Serengeti, Maasai-Mara (Kenya) na Ngorongoro. Mzunguko wa kundi hili kubwa la wanyamapori ndiyo pekee uliobaki katika sayari hii ya dunia.

Mzunguko huo ni kivutio cha watalii wengi mno wanaoliingizia Taifa fedha za kigeni nyingi.

Kutenga Pori Tengefu la Loliondo kutasaidia kupambana na magonjwa ya wanyamapori kwenda kwa binadamu.

Binadamu huathirika moja kwa moja na magonjwa yatokanayo na mwingiliano baina yao na wanyamapori. Magonjwa hayo ni kama homa ya Bonde la Ufa, kimeta, kichaa cha mbwa na homa za matumbo.

Taarifa za afya zinaonesha kuwa kati ya Oktoba 2015 na Oktoba 2016, watu 317 walithibitika kuugua ugonjwa wa kimeta. Baadhi yao walifariki dunia.

Uwepo wa mifugo kwenye maeneo ya wanyamapori hueneza magonjwa yanayoua wanyamapori. Mfano, ugonjwa wa kichaa cha mbwa na kichaa cha samba; magonjwa ambayo yameua wanyamapori wengi Serengeti. Uwepo wa mifugo hufukuza kabisa wanyamapori kwa sababu wafugaji huwa na makundi ya mbwa na wakati mwingine ng’ombe, mbuzi na kondoo huvikwa kengele.

Ni kwa sababu hiyo, unaona kabisa umuhimu wa kulitenga eneo la Loliondo katika makundi ya kuwezesha kufanyika shughuli za uhifadhi na zile za kibinadamu kama uchungaji na kilimo.

Kwa mara nyingine, napenda kumpongeza Waziri Mkuu Majaliwa pamoja na timu ya wasaidizi wake, hasa Naibu Waziri Makani; kwa kulivalia njuga suala la Loliondo na Ngorongoro kwa ujumla wake. Sote kwa umoja wetu tuna wajibu wa kuulinda urithi huu.

By Jamhuri