Mahabusu nchini wamelaumu taarifa iliyotolewa hivi karibuni isemayo mashauri yaliyokuwa yamerundikana mahakamani yamemalizika kwa asilimia 98. Katika barua waliyoandika kwa Waziri wa Sheria na Katiba na nakala kwenda kwa Jaji Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mtendaji Mkuu wa Mahakama (nakala tunayo), mahabusu wa Gereza la Keko jijini Dar es Salaam wanaikosoa taarifa hiyo wakisema ni ya upotoshaji, kwa kuwa kesi bado zimerundikana katika mahakama kadhaa za wilaya na mikoa. Barua yenyewe inasomeka hivi:

Sisi ni mahabusu tuliopo magerezani tukikabiliwa na tuhuma mbalimbali. Mheshimiwa, tunasikitishwa sana na taarifa zako za kimahakama za majumuisho ya kesi zilizomalizika katika mahakama za Tanzania kuanzia Januari hadi Mei mwaka huu.

Taarifa hiyo tumeisoma kupitia katika gazeti moja la Kiingereza la Agosti 16, 2021, taarifa hiyo ikieleza kuanzia mahakama za wilaya, mkoa hadi Mahakama Kuu pia ukasema Mahakama Kuu umemaliza mashauri yote kwa asililimia 98.

Hii ni mara ya pili kutoa majumuisho yasiyo sahihi kiuhalisia tunakumbuka mwezi wa pili katika sherehe za siku ya sheria za mwaka huu, ulisema katika mahakama zako hakuna kesi yenye zaidi ya miaka mitano magerezani, nasi tulitoa majumuisho ya kesi zetu zilizodumu kati ya miaka mitano hadi kumi kupitia Gazeti letu la JAMHURI.

Baada ya taarifa hiyo kutoka, ghafla tulitembelewa na ugeni kutoka Ofisi ya Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Machi 18, 2021 ikiongozwa na Mheshimiwa Jaji Kulita na Naibu Msajili Mkoa wa Dar es Salaam.

Tulizungumza nao matatizo yetu yote yanayotukabili dhidi ya Mahakama kuhusiana na usikilizwaji wa mashauri yetu kwa kutokusikilizwa kwa miaka mingi pamoja na utaratibu wao wa upangaji wa tarehe za usikilizwaji wa mashauri kupitia ‘first in first out’ (FIFO); ikimaanisha ‘wa kwanza kuingia na wa kwanza kutoka’. 

Utaratibu ambao hatujaupenda na unanyima haki kwa watu ambao walikuwa wa kwanza kuingia pamoja na kusajiliwa kisha kesi zao zikaondolewa kwa kukosekana ushahidi.

Baadaye zikarudishwa tena mahakamani na kusomeka zikiwa na usajili mpya. Kwa mfano kesi ya Saidi Hamisi Lubuva zamani ilikuwa inasomeka kama PI/17/2014 – Session Case No.6/2017 Mahakama Kuu Dar es Salaam.

Ikaondolewa mahakamani Desemba 13, 2018 mbele ya Jaji Mlango kwa kukosekana ushahidi na kurudishwa tena mahakamani, na kusomeka kama PI/28/2018 – Session Case No. 10/2020 Mahakama Kuu Dar es Salaam.

Hivi kweli mtu wa mwaka 2019 aliyesajiliwa apate tarehe ya usikilizwaji kabla ya mtu wa mwaka 2014? Kesi hii ina miaka saba sasa bila kumalizika kisheria. Ugeni ule ulituahidi kuyafanyia kazi haya malalamiko yetu, pia kutuahidi kutuletea vikao 10 vya usikilizwaji wa mashauri yetu pamoja na kupunguza msongamano wa mahabusu magerezani.

Lakini mpaka sasa ni kikao kimoja tu ndicho kilichokuja (session) tena kikihitaji kesi 10 za usikizwaji katika zaidi ya kesi 150 zilizopo Mahakama Kuu Kivukoni.

Tofauti na zamani zilipokuwa zikiitwa kesi 30 mpaka 40 katika kikao kimoja. Na ukizingatia vikao ni viwili tu kwa mwezi; katika mwaka mzima kutakuwa na kesi 20 tu ambazo zitasikilizwa katika mwaka huo, hapo kweli kuna uwezekanao wa kupunguza msongamano mahakamani na magerezani?

Hili tatizo lipo Mahakama Kuu Kivukoni tu na si katika Mahakama Kuu ya Mafisadi, Ubungo. Mbona Mahakama Kuu Ubungo ina majaji watatu lakini kesi zinaenda bila malalamiko? Mahakama Kuu ya Kivukoni ina majaji zaidi ya tisa, lakini kesi haziendi. Kwa mfano, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ina uwezo wa kusikiliza mashauri ya mauaji tu na kesi zinasikilizwa.

Kwa nini zisipelekwe huko kesi zikasikilizwa kupunguza msongamano wa mahabusu magerezani?

Kuna baadhi ya kesi matukio yake yametokea Mkoa wa Dar es Salaam na mashahidi wake wote wapo hapahapa Dar es Salaam, sasa kuna haja gani ya kupoteza pesa za serikali katika vikao vya mashauri ya usikilizwaji?

Mheshimiwa, haki na wajibu ni muhimu kwa mujibu wa kifungu cha 6 hadi cha 13 cha sheria namba 15 ya mwaka 1984, kwamba watu wote ni sawa mbele ya sheria na wana haki ya kulindwa na kupata haki mbele ya sheria.

Pia Mahakama ya Kisutu kuna kesi zina zaidi ya miaka mitano bila mashauri hayo kumalizika, wala hayahitaji kikao cha usikilizwaji, kwani kesi zinakwenda kila baada ya siku 14 kama sheria inavyoelekeza, lakini tatizo lipo bado la ucheleweshwaji wa kesi bila sababu za msingi.

Sasa tunamuomba Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na vyombo vyote vinavyohusika na malalamiko haya kuanzia Waziri wa Sheria, Jaji Mkuu, Mwanasheria Mkuu, Jaji Kiongozi, Mtendaji Mkuu wa Mahakama na Msajili Mkuu wa Mahakama Tanzania, kuitupia jicho Mahakama Kuu ya Kivukoni kwani ndiyo yenye msongamano mkubwa wa mashauri mengi ya magerezani.

Sisi mahabusu hatuna uwezo wa kukufikishia ujumbe wetu kiongozi wetu zaidi ya msaada tunaopata kutoka Gazeti letu la uchunguzi wa wanyonge la JAMHURI.

Mungu aubariki sana uongozi wa gazeti hili (amina), pia sisi mahabusu ndio wateja wakubwa wa kuliunga mkono gazeti letu la wanyonge, nikimaanisha hakuna mahabusu asiyenunua Gazeti la JAMHURI.

Kuhusu upande wa TEHAMA (teknolojia ya habari na mawasiliano) wamesema imekuwa ikitumika tofauti na matarajio tuliyotegemea. Imekuwa ndiyo chanzo kikubwa cha msongamano magerezani, kesi hazimaliziki, hasa mahakama za wilaya na Mkoa wa Dar es Salaam. Hakimu mmoja amekuwa akiahrisha kesi zote za siku hiyo bila wahusika kuitwa ingawa wapo hapohapo mahakamani.

Mbaya zaidi, mashahidi wapo, mahakimu wapo, lakini kesi hazisikilizwi bila sababu za msingi. Tunakuomba Jaji Mkuu kuliangalia hili, huenda haulifahamu (nikimaanisha mahakimu hawafanyi kazi).

Ndugu mwandishi, hizi ni baadhi ya kesi chache tu zilizopo Mahakama kuu ya Kivukoni zenye zaidi ya miaka kumi bila mashauri hayo kumalizika kisheria. Naomba uzichapishe gazetini kama sehemu ya ushahidi wa haya tunayosema.

1. Jumanne Adeade;  PI/24/2010/Session Case NO. 84/2013/ – Sasa inasomeka kama PI 31/2017/Session Case No. 67/2019. Kesi hii ni ya mauaji.

2.  Asha Saidi Kungwi PI-27-2011-Session Case No. 9/2014

3.  Judith Marco Kusekwa PI/17/2012-Session No. 71/2016

4.  Hadija Hasani Luanga PI/5/2013-Session No. 72/2016

5.  Pendo Stanrey Msaki PI/15/2013-Session Case No. 147/2015

6.  Antonio Ajo PI/17/2013 Session No. 122/2017

7. Pamera Kiamania Kibaya PI/14/2014 Session No 173/2016

8.  Salama Ramadhani Juma CC154/2013 Sasa inasomeka kama PI 1/2018/Session No. 10/2018

9. Olibisi Ibudu Gole PI/22/2014 Session No 124/2016

10.  Rehema Anrehem Ndunguru PI/7/2015

11.  Nasra Hamisi Hasani PI/5/2013-Session No 59/2015

12. Moyo Ramadhani Aneir PI/10/2014-Session Case No 58/2017

13.  Rebeca Vicent Madinda PI 7/2014-Session 90/2017

14.  Husna Majani Afa PI/9/2015

15.  Masesa Andrew Joseph PI/2013

16.  Mary Mvora CC 123/2012

17.  Ani Lawrenta Chioma PI/96/2012-Session No 177

18.  Halmata Tayo Isado PI/21/2015 Session No 20/2017

19.  Peter Joseph Mushi PI/16/2014 Session No 110/2016 Kwa sasa inasomeka kama PI/6/2019-Session No. 240/2019

20.  Saidi Hamisi Lubuva PI/17/2014 Session No 6/2017 Kwa sasa insomeka kama PI/28/2018 Session No 10/2020

Ni mimi mahabusu

Saidi Hamisi Lubuva.

Rais wa tano, Dk. John Magufuli, akizungumza na wafungwa na mahabusu wa Gereza la Butimba, Mwanza alipowatembelea kusikiliza kero zao.

By Jamhuri