NA MWANDISHI WETU

Wiki kama mbili au tatu hivi zilizopita, mabingwa wa soka nchini, Simba Sports Club, wamelivunja benchi zima la ufundi. Wameachana na kocha mkuu, kocha wa viungo na kocha wa makipa. 

Kwangu hii si stori mpya, wala hata ilipotangazwa rasmi haikunishitua. Hii ni kwa kuwa hilo nililitarajia kutokea mara tu baada ya kushuhudia ‘Mnyama’ akilala mbele ya Jwaneng Galaxy ya Botswana jioni moja ya Jumapili katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. 

Uwanja ambao kwa miaka mingi umekuwa ukiaminika kuwa ngome imara ya Simba. “Kwa Mkapa hatoki mtu,” kauli ya mara kwa mara iliyokuwa ikitumiwa kwa mbwembwe na mashabiki wa Simba.

Lakini hali haikuwa hivyo Jumapili ile, kwa kuwa Simba walilala. Tena kwa mabao mengi. Matatu! Lazima hatua kali zingechukuliwa. Hilo halikuwa likiepukika.

Mara baada ya kipenga cha mwisho sikuona kama kutakuwa na usalama kwa Kocha Didier Gomez Da Rosa na benchi lake zima, lakini sikujua kama kocha wa viungo na kocha wa makipa wangekuwa sehemu ya waathirika wa matokeo ya mechi ile.

Kwetu sisi wafuatiliaji wa soka la Tanzania, huyu kocha wa makipa ameondoka nchini kama shujaa. Kuna sehemu amemtoa na kumfikisha kipa wetu namba moja wa timu ya taifa, Taifa Stars, Aishi Manula. 

Kocha huyo, Milton Nienov, mwenye umri wa miaka 52, alitua Simba mwanzoni mwa mwaka huu na kupewa jukumu la kuwanoa makipa wa klabu hiyo kubwa Afrika Mashariki.

Aishi amewahi kuwa chini ya makocha mbalimbali wa makipa wa ndani na nje ya nchi na kuna sehemu makocha hao walimfikisha, lakini huyu aliyeondoka Simba kwa uhakika amemfikisha mbali zaidi ya walikomfikisha wengine. 

Hajamuacha Aishi kama alivyomkuta. Achana na makosa yaliyofanyika au aliyoyafanya katika mechi dhidi ya Galaxy, kuna kazi kubwa kocha huyu ameifanya yeye pamoja na Aishi katika kiwanja cha mazoezi pale Bunju na viwanja vingine vingi walivyotembelea ndani na nje ya nchi; lakini zaidi Bunju. 

Kutajwa kwa Manula na kuwekwa katika kapu moja na makipa wakongwe na wakubwa Afrika kama akina Mohamed Elshanawy wa Al Ahly ya Misri, Dennis Onyango wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Sherif Ekramy wa Pyramids ya Misri na wengineo si kazi ndogo. Ni kazi ngumu. 

Kina Mwalami Mohamed ‘Shilton’, Iddy Abuubakar, Juma Pondamali ‘Mensah’, Saleh Machupa, Patrick Mwangata, Ivo Mapunda wamempa kitu Aishi, lakini huyu kocha aliyetimuliwa na Simba amemtoa Aishi eneo moja kwenye maisha yake ya soka na kumpeleka eneo jingine kabisa (hii haina maana kuwa akina Shilton hawajafanya kitu katika soka la Aishi). 

Lakini ni ukweli unaoonekana wazi kwa wengi kuwa chini ya kocha aliyekuwa naye Simba, raia wa Brazil, yule Aishi tuliyemfahamu kwa miaka mingi amebadilika na kuimarika kwa kiasi kikubwa sana. 

Siku hizi Aishi hana au hafanyi makosa ya kujirudia. Aishi wa sasa hadaki tena kizamani au kufanya ile tabia ya kudondoka dondoka tuliyoizoea kwa makipa wetu wengi wa ndani. 

Ukiona Aishi amedondoka chini, ujue hapo ilikuwa ni lazima au alikuwa anatakiwa kudondoka. Aishi chini ya kocha kutoka Brazil, hapotezi muda kipuuzi! Aishi huyu ameiva na ni wa kimataifa kwa kila hali. 

Kuna makipa wanaamini ili uonekane mahiri ni lazima ujidondoshe, huku wengine wakipenda kupoteza muda wakiamini kuwa hiyo ni moja ya mbinu muhimu za mchezo. 

Aishi ameshatoka eneo hilo la kuwa kipa wa kujidondosha hovyo na kupoteza muda kipuuzi puuzi. Hivi sasa amekuwa kipa mahiri; kipa mkubwa, kipa wa kimataifa.

By Jamhuri